MASHABIKI WAMHITAJI MALOPE TAMASHA LA PASAKA 2014
JINA la Rebecca Malope si geni masikioni na machoni mwa wengi, hasa kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa Injili. Rebecca aliyezaliwa mwaka 1968, yu miongoni mwa waimbaji wa kimataifa wa muziki wa Injili kutoka nchini Afrika Kusini, aliyewahi kuja nchini mara moja kwa mwaliko wa Kampuni ya Msama Promotions kupamba Tamasha la Pasaka. Kupitia tamasha hilo ambalo lilifanyika jijini Dar es Salaam Aprili 8, Rebecca akishirikiana na wengine mahiri wa ndani na nje ya Tanzania , walikuwa baraka katika tamasha hilo lililofanyika mara ya kwanza Uwanja wa Taifa mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Umahiri wa Rebecca katika uimbaji na uchangamfu jukwaani, umewafanya wadau wengi watamani awe miongoni mwa waimbaji katika Tamasha la Pasaka la mwaka huu Aprili 20, jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia katika mikoa itakayopata kura nyingi za wadau. Shauku ya kumtaka...