JINA la Rebecca Malope si geni masikioni na machoni mwa wengi, hasa kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa Injili.
Rebecca aliyezaliwa mwaka 1968, yu miongoni mwa waimbaji wa kimataifa wa muziki wa Injili kutoka nchini Afrika Kusini, aliyewahi kuja nchini mara moja kwa mwaliko wa Kampuni ya Msama Promotions kupamba Tamasha la Pasaka.
Kupitia tamasha hilo ambalo lilifanyika jijini Dar es Salaam Aprili 8, Rebecca akishirikiana na wengine mahiri wa ndani na nje ya Tanzania,
walikuwa baraka katika tamasha hilo lililofanyika mara ya kwanza
Uwanja wa Taifa mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Umahiri wa Rebecca katika uimbaji na uchangamfu jukwaani, umewafanya
wadau wengi watamani awe miongoni mwa waimbaji katika Tamasha la Pasaka
la mwaka huu Aprili 20, jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia katika
mikoa itakayopata kura nyingi za wadau.
Shauku ya
kumtaka Rebecca ni ishara ya wazi ya wadau hao kuvutiwa na waimbaji wa
Afrika Kusini kwani mbali ya mwanadada huyo, wengine waliowahi kualikwa
na Msama Promotions ni Sipho Makhabane (Pasaka ya 2013) na Solly
Mahlangu (Krismasi ya 2013).
Pamoja na wadau wengi kutamani kumwona mwanadada huyo kama Anna Ferdinand wa Yombo Vituka, Innocent
Gregory wa Pugu-Kwa Mustapha, Mkomwa Meshack na Dotto Mnyemvua wa
Lumo-Machimbo, kwa mujibu wa waratibu wa tamasha hilo, waimbaji
wataalikwa kwa kigezo cha wingi wa kura.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama,
alisema
kuwa kama Rebecca atapata kura nyingi za wadau wataketi kujadili jambo hilo kama inawezekana au vipi, kwani ni miongoni mwa waimbaji mahiri aliyewahi kupamba tamasha la mwaka 2012.
Rebecca ni nani?
Mwanadada huyu shupavu anayejulikana kwa wengi kama malkia wa muziki
wa Injili Afrika, ni mzaliwa wa Kijiji cha Lekazi, nje kidogo ya mji
wa Nelsprut, Mpumalanga, nchini Afrika Kusini.
Ukiangalia historia yake, Rebecca ni kipaji kilichochomoza katikati
ya maisha na mazingira magumu kiasi cha kushindwa kupata elimu ya
kutosha, lakini Mwenyezi Mungu akimuinua kupitia kipaji cha uimbaji wa
nyimbo za Injili akitamba kimataifa.
Katika mazingira hayo magumu kimaisha, Rebecca akiwa mtoto alipatwa
na ugonjwa uliomfanya ashindwe kutembea kiasi cha madaktari kudhani
kuwa asingetembea tena katika maisha yake.
Kutokana na ufukara wa familia yake, yeye na dada yake (Cynthia)
walikimbilia katika kitongoji cha Everton, nje kidogo ya Jiji la
Johannesburg kwa lengo la kutafuta kazi ya kujikimu kimaisha.
Mwaka 1986, wakati huo Rebecca akiwa na umri wa miaka 21, alishiriki
shindano la kutafuta vipaji vya uimbaji maarufu kama ‘Shell Road to
Fame,’ lakini alishindwa kwa mbali.
Lakini hakukata tamaa kwani mwaka uliofuata alishiriki tena na
kuibuka mshindi kupitia wimbo wake wa ‘Shine On,’ ukiwa mwanzo wa
mwanga wa mafanikio yake kwani kibao hicho kilimsogeza mbali.
Kibao hicho ndicho kilimwezesha kukutanishwa na muandaaji mashuhuri
wa muziki, Sizwe Zako na kupata meneja wake wa kwanza aliyejulikana kwa
jina la Peter Tladi.
Albamu yake ya kwanza ya Rebecca ambayo ilikuwa na nyimbo za kidunia,
haikufanya vizuri sokoni, hivyo akageukia muziki wa Injili
kudhihirisha kuwa karama yake ni katika muziki huo na si vinginevyo.
Kutokana na mvuto wa vibao vyake vya awali, Rebecca akajikuta akipata sapoti kubwa kutoka kwa radio mbalimbali kwa kupiga vibao vyake, kitu ambacho kwa Afrika Kusini hakikuwa cha kawaida.
Mwaka 1990, Rebecca alishinda tuzo ya mwanamuziki bora wa kike wa
Afrika Kusini na hadi kufikia mwaka 1993, ilikadiriwa kuwa watu zaidi
ya milioni moja walimpigia kura kama mwanamuziki bora wa kike katika
shindano la Coca Cola Full Blast Music Award Music Show na kushinda tena
mwaka 1994.
Kwa upande wa mauzo, albamu zake zote kumi za kwanza zilikuwa moto wa
kuotea mbali sokoni zikiingia kwenye hadhi ya dhahabu, ambapo kwa
kipindi hicho alikuwa ameuza nakala zaidi ya milioni mbili.
Mwaka 1995 kupitia CD yake ya Shwele Baba, aliuza nakala zaidi ya
milioni moja ndani ya wiki tatu tangu ulipozinduliwa, ikiweka rekodi ya
aina yake katika historia ya soko la muziki Afrika Kusini.
Mwaka 1996, haukuwa mwaka mzuri kwa Rebecca kwani alimpoteza baba
yake mzazi, kaka yake na dada yake. Wote walifariki dunia kwa
kufuatana, tena katika mazingira ya kutatanisha, jambo ambalo
lilimtikisa kwa kiasi kikubwa mwanadada huyo.
Lakini, Rebecca alijipa moyo mkuu akimwachia Mwenyezi Mungu kwa yote
yaliyotokea na kamwe hakutoa nafasi mkasa huo uwe kikwazo kwake cha
kumtumikia Mungu kwa karama ya uimbaji.
Mwanadada huyo anakiri kuwa, siri ya mafanikio yake ni kujituma, kuwa
na malengo na kufanya kazi kwa bidii, akimshirikisha Mungu, kiasi cha
kutawazwa kuwa malkia wa muziki wa Injili Afrika, huku wengi
wakimfananisha na Brenda Fassie, ambaye kwa sasa ni marehemu..
Kati ya mwaka 1995 na 2004 Rebecca amezunguka ulimwenguni akiwa na bendi ya Pure Magic akimtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.
Mwaka 2003, Rebecca alitunukiwa udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu
cha Natal kutokana na mchango wa kutukuka kwa jamii na muziki nchini
Afrika Kusini na Desemba mwaka huo alishinda tuzo ya Kora kama
mwanamuziki bora wa Injili.
Katika wanamuziki ambao alishirikiana nao kwa karibu sana na wamekuwa
na mchango mkubwa kwake ni pamoja na marehemu Vuyo Mokoena.
Mwaka 2004, Rebecca alianzisha kipindi chake katika runinga kikiitwa ‘Gospel time’ ambacho kinafanya vizuri.
Februari 25, 2012, Rebecca amerekodi nyimbo za ‘live’ katika Jiji la Pretoria, hiyo ikiwa ni albamu ya 32.
Baadhi ya tuzo ambazo Rebecca Malope amewahi kutunukiwa ni mwaka 1994
mwimbaji bora, mwaka 1997 albamu bora sokoni iliyoitwa ‘Uzube Nam’,
mwaka 1998 muimbaji bora wa nyimbo za Injili Afrika na albamu bora
katika mauzo iliyoitwa ‘Angingedwa.’
Nyingine ni mwaka 1999 mwimbaji bora wa kike na mwimbaji bora wa
Injili Afrika kupitia albamu ya ‘Somlandela’, mwaka 2002 msanii bora wa
nyimbo za Injili akishinda na wimbo wa ‘Sabel Uyabizwa’, mwaka 2003
msanii bora Afrika kupitia wimbo wake wa ‘Iyahamba Lenqola’ na mwaka
2004 msanii bora wa mwaka kwa wimbo wake, ‘Hlala Nami’.
Rebecca aliyekuwa kipenzi cha Rais wa kwanza wa Afrika Kusini,
marehemu Nelson Mandela na Rais wa sasa, Jacob Zuma, amepitia maisha ya
taabu, dhiki kubwa na changamoto nyingi.
Cha kufurahisha kwa mwimbaji huyu nguli, ni kuwa mpaka sasa ameachia albamu zipatazo 32 ndani ya miaka 27.
“Watu hawana amani, kuna vita kila sehemu, hata kanisani, nataka watu
wawe pamoja tena cha muhimu wawe na amani katika maisha yao, ili tuwe
na amani duniani, anasema Rebecca.
ORODHA YA ALBAMU
Ma G Man (1986); Six of the best (1989); Saturday Nite (1990);
Buyani (1991); Rebecca Sings Gospel (1992); Ngiyikeleni (1993); Umoya
Wami (1994); Shwele Baba (1995); Uzube Nam (1996); Live at the State
Theatre (1996) na Angingedwa (1997).
Nyingine ni Free at Last (1997); Somlandela (1998); Ukholo lwam
(1999); Siyabonga (2000); Christmas with Rebecca and Friends (2000);
Sabel’Uyabizwa (2001); Iyahamba Lenqola (2002); Hlala Nami (2003); The
Queen of Gospel and the Village Pope (2004); Qaphelani (2005) na The
Greatest Hits (2005).
Albamu nyingine ni Umthombo (2006); Live in Soweto (DVD) (2006); Live
in Soweto (CD) (2007); Amakholwa (2007); Ujehova Ungu’madida (2008);
African Classics (2009); My Hero (2009); Live at the Lyric Theatre
(DVD); (2010) Uzohamba Nami (2010); Ukuthula (2011); Rebecca Live
Concert ft Tshwane Gospel Choir (CD)(2012); Rebecca Live Concert ft
Tshwane Gospel Choir (DVD)(2012); na Bayos’ khomba (2013).
CHANZO:TANZANIA DAIMA
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni