“5Na tazama, Sauli akaja akifuata ng’ombe
kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia?
Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi” (1 Samweli 11:5).
Kila mtu
amezaliwa na KUSUDI tayari, ila HATMA yako ni wajibu wako kuiFIKILIA kwa bidii
zako, KAMA ukiweza KUVUMBUA kusudi lako na KULITIMIZA. Kwa lugha nyingine
kusudi limeitwa WITO.
Kwa bahati
mbaya, majina yetu, kwa watu wengi sana, hayataji KUSUDI ndani yao! Sijui kama
unajua kwamba kila KUSUDI lina jina, na hilo jina atapewa AFANYAYE mambo katika
kusudi hilo. Kwa mfano, kama wewe unaitwa Mary, na ni nabii, lakini hutabiri,
jina lako litakuwa Mary, kwa sababu ulipewa utotoni. Utaitwa Mary hadi kufa
kama hutavumbua KUSUDI lako na kulitenda.
Lakini, kuna
jina ulipewa KABLA ya kuzaliwa, hilo jina LINATAJA kusudi lako. Kwahiyo, kama
huyo Mary ataanza KUTABIRI, na watu WAKAKUBALI hiyo huduma yake ya unabii, jina
lake litakuwa ‘nabii Mary’. Je! Wewe unaitwa nani?
Hebu angali
hii,
“Kabla sijakuumba katika
tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa
nabii wa mataifa” (Yeremia 1:5).
Ukifuatilia
habari za Yeremia, utagundua kwamba jina “Yeremia” alipewa baada ya kuzaliwa,
lakini jina “nabii” alipewa kabla ya kuzaliwa. Jina Yeremia ni jina kama kila
mtu alivyo na jina, ila jina “nabii” ni jina la KUSUDI la Mungu maishani mwake.
Kwenye maandiko
utaona watu wachache sana walipewa majina yao ya ‘KAWAIDA’ kabla ya kuzaliwa. Ila
ukifuatilia, utaona Mungu akisema KUSUDI la mtu bila jina la kawaida.
Haijalishi kwamba ‘jila la kawaida’ ni Yakobo au Esau, Mungu alitaja KUSUDI la
hao wawili wakiwa tumboni. Mungu hakusema wataitwa Yakobo na Esau, majina haya
walipewa na wazazi wao! (Mwanzo 25:22-26)
Hata hivyo,
bado sipuuzii UMUHIMU wa ‘kuchagua’ jina LIFAALO. Ndio maana baada ya miaka
mingi, Yakobo alibakia na jina lake hadi alipopewa jina jingine na Mungu;
akaitwa Israel. Angalia, Jina Israel lilikuja wakati Yakobo AMEFANYA jambo
fulani katika lile KUSUDI lake. Angebweteka, angekufa akiitwa Yakobo!
Sizungumzii majina, mimi nasema habari za KUSUDI.
Ukisoma 1
Samweli 11:5, utaona Sauli akiendelea na shughuli zake za kawaida, japo
AMEPAKWA mafuta kuwa mfalme! KUSUDI la Sauli kupakwa mafuta ni kuwa MFALME na
kisha kuwaokoa wana wa Israel na Wafilisti. Hadi kwenye sura ya 11, 1 Samweli
5, bado Sauli hakuitwa ‘jina’ mfalme kwa sababu bado alikuwa hajaSIMAMA kwenye
KUSUDI hilo.
Sauli
alipopakwa mafuta, alirudi nyumbani kwakwe na kuendelea na biashara zake za
ng’ombe kama kawaida! Mpaka Nahashi, Mwamoni alipokuja kutaka kufanya kazi ya
KUWAKOA Israel, ambayo ni kazi ya Sauli, kwa makubaliano ya wana wa Israel kung’olewa
jicho la kuume (1 Samweli 11:1-3), ndipo Sauli akakurupuka na kuanza kufanya
KUSUDI lake.
Hebu fikiri
kama Nahashi angefanya kimya kimya bila kudai jicho la mtu; Kisha akawaokoa
Israel na Wafilisti, na wao wakamtumikia kama walivyoapa! Ndivyo ilivyo hata
leo, wengi wetu tumejiapisha (saini mikataba) ya kuwatumikia watu ambao, kwa
kweli siko KUSUDI letu liliko. Na, inetughariumu vibaya. Je! Kwa namna hiyo
tutafikilia HATMA zetu?
Haya ni mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu kusudi ndani
yako:
i.
Neno la Mungu
“Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya
BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa
imara juu ya Israeli milele. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA
amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu
juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru”(1 SAM. 13:13-4).
Nimekutana
na watu wengi sana ambao wanasema, “mimi sijui wito wangu”, “mimi sijui kusudi
la Mungu maishani mwangu”, “mimi sijui Mungu anataka nifanye nini hasa”, nk.
Nikiwatazama
hawa watu wote, sio kwamba hawafanyi kitu, wako busy na kazi zao, huduma, nk.
Wengine wanafanya kazi chini ya watumishi wengine wa Mungu, nk.
Kinachonishangaza, je! Hao watumishi wanaofanya nao kazi pia hawajui kwamba
watu waliopo chini yao ndio WENYEWE au ni VISHOKA tu? Nitakwambia jambo, Mungu
anaangalia ALIYEKO tayari, potelea mbali kama ni KISHOKA au ni mfanyakazi
RASMI! Kazi itafanyika.
Nitakupa
siri moja, kama watu wangesimama kwenye NAFASI zao vizuri, hakika kusingekuwa
na KISHOKA! Ni sawa na mahali ambapo kila mtu ana USAFIRI binafsi, je! Mpiga
debe atafanya nini? Bila shaka mahali kama hapo hapatakuwa na wapigadebe!
Ndivyo
ilivyo hata kwenye ufalme wa Mungu. Walioalikwa (walioitwa) hawapo, wako busy
na mambo mengine! Basi, watakusanywa waliopo kwenye njia kuu, waje badala yao (Mathayo
22:1-10). Na, wasipofanya liwapasalo, basi mawe yataamshwa kufanya kazi ipasayo
kwenye nafasi zao!
“8Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. 9Wala
msijidhanie mnaweza kujiambia, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu, kwa maana
nawaambia kuwa Mungu anaweza kumuinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe
haya. 10Hata sasa shoka limekwisha kuwekwa tayari kwenye mizizi ya mti. Kila
mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni” (Mathayo 3:8-10).
Umewekwa duniani KUZAA matunda, tena matunda fulani mahusus, si alimradi tunda
ni tunda tu! la sivyo, ni AHERI ukatwe!
Wakati
Bwana anaangalia MAVUNO na kuona yameiva, alisema, “Mwombeni Bwana wa mavuno
apeleke watendakazi shambani mwake” (Luka 10:2). Inahitahika MAOMBI ili UWEZE
kuingia shambani kufanya SEHEMU yako. Watu hawafanyi kwa sababu ni watendakazi,
ila kwa sababu WAPO TAYARI na kuna NGUVU za Mungu za kuwaweka kwenye hilo
kusudi. Usipoomba, ujue kwa hakika, utatumika KUSIKO KWAKO na utapata HASARA
mwishowe, kwa sababu nani ATAKULIMIA shehemu yako wakati wewe unalima kwa
wenzako?
Hatua
za kukaa kwenye KUSUDI zinaanza na kukaa kwenye NENO pamoja na MAOMBI. Pasipo
neno, hakuna imani; Pasipo imani, maombi hayana nguvu hata kama yapo!
Hebu
soma habari za mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, UZAAO matunda yake
kwa MAJIRA yake, wala jani lake halinyauki, (Zaburi 1:1-6). Mti huu ni mfano wa
mtu anayesoma NENO na kulitafakari USIKU na MCHANA! Atakaa MAHALI anapopaswa na
ATAZAA sana, na “kila alitendalo litafanikiwa”! Hii inaanza na kusoma na
kutafakari neno la Mungu.
Kadri
UNAJAA neno, utagundua kuna mambo yanabadilika taratibu, NENO litakusafisha,
pia na MACHO yako ya rohoni yataondoka tongotongo. Utaanza kuona mambo kwa
MTAZAMO tofauti. Hilo neno litakumulikia NJIA ikupasayo kupita! (Zaburi 119:105);
Utaanza KUGUNDUA kikupasacho kufanya, taratibu, hilo neno litazungumza na wewe
wakati unalisoma. Utapata MWANGA wa kuona LIKUPASALO! Ule mwanga UTAIBUA kusudi
lililoFICHIKA ndani yako.
Kwa
mfano, angalia zile huduma tano, kuna namna ambavyo mwalimu akisoma neno ataona,
na mwinjilisti ataona kwa namna nyingine, nabii, mchungaji, mtume, nk, wote
wataona kwa namna WALIVYO, japo wamesoma kitu kile kile. Ndio maana mwalimu akisema
neno lile lile, hata kama hajajitambulisha, utagundua huyu ni mwalimu, na
mwinjilisti akisema, atatambulika tu. Hii ni tofauti ya kuona kulingana na WITO
au KUSUDI ndani yako. Lakini pia neno hilo litawajenga MUSULI zao kwa namna
tofauti ili waweze KUTIMIZA kusudi ndani yao; kila mmoja kama ALIVYOITWA.
Kwa
hiyo, kadri unajifunza neno, na kusoma kwa bidii, lile neno litakuchonga wewe illi
uzidi KUFANANA na kile kitu Mungu alichokitarajia kwako. Hata hivyo, inaanza na
kuwa NDANI ya Yesu (kuwa tawi la mzabibu); Ndipo UKISOMA neno na kufanya kazi
sawa na hilo neno UTASAFISHWA “ili” UZAE zaidi. Kuzaa maana yake ni KUTOA
MATUNDA yaliyokusudiwa sawa na WITO wako.
Kwa
bahati mbaya watu wanadhani kuzaa ni kuzaa tu! Ndio maana wale watu walimwendea
Yesu wakisema “tulitoa pepo kwa Jina lako”, Naye akawaambia, “ondokeni kwangu
ninyi mtendao maovu”. Unadhani ni kwanini? Angalia mfano wa mfalme Sauli, unadhani
alizini, aliua, aliiba, nk.? Kosa lake ilikua KUTOA SADAKA ISIVYO SAHIHI!
Yaani, hakufuata NENO LA MUNGU ili atende SAWA na WITO wake! Nabii Samweli
akamwambia, umefanya upumbavu!
“21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana,
atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba
yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana,
hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako
kufanya miujiza mingi? 23 nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe;
ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” (Mathayo 7:21-23).
Sasa
zingatia jambo hili, je! Unajua kazi zako (kusudi), nyakati, mahali pa kuishi,
nk., Viliumbwa kabla HUJAZALIWA? Yaani uliwekewa MIPAKA tayari. Hebu linganisha
vifungu hivi miwili, (Matendo ya Mitume 17:24-28) na (Yohana 15:1-5).
“24 Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote
vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu
zilizojengwa kwa mikono; 25 wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana
kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi
na vitu vyote. 26 Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika
mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha
kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; 27
ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi
mbali na kila mmoja wetu. 28 Kwa
maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama
vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake”
(Matendo ya Mitume 17:24-28).
Kisha
angalia, “1 Mimi ndimi mzabibu wa kweli,
na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila
tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha,
ili lizidi kuzaa. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno
nililowaambia. 4Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi
lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi,
msipokaa ndani yangu. 5 Mimi ni
mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana;
maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote” (Yohana
15:1-5).
Kwenye
Matendo ya Mitume wanazungumzia “wanadamu”,
kwenye Yohana wanazungumzia “tawi la mzabibu”. Wanadamu unaowaona kwenye
Matendo ya Mitume, wameumbiwa majira na nyakati na mipaka ya makazi tayari.
Majira na nyakati, maana yake ni vipindi mbalimbali ambavyo vinaendana na
majukumu fulani mahusus. Kwa mfano, wakati wa mvua kuna kupanda; kuna shughuli
zake hapo tofauti na wakati wa kiangazi.
Ukiangalia
Yohana, utaona “tawi la mzabibu”. Inamaana kuna kazi mahusus ya kufanya, ambayo
ni KUZAA zabibu sio machungwa! Kuna mahali hilo tawi lipo! A specific location kwenye
mzabibu na halisogei hapo! Kazi yake ni kuzaa tu! Na, kazi ya Bwana ni kulisafisha
kwa NENO ili lizae zaidi.
Sasa angalia
jambo jingine,
Kwenye
Mdo 17:18, tunasoma “Kwa maana ndani yake yeye tunaishi,
tunakwenda, na kuwa na uhai wetu”, na BWANA anasema kwenye ,Yoh. 15:5 ,
“…akaaye
ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi
kufanya neno lo lote “.
Kuweza
kufanya KUSUDI, huanza na KUKAA ndani ya Yesu, na kumsikiliza Yeye (neno la
Mungu/biblia). Hakuna mtu atafanikiwa kufanya kusudi la Mungu bila mambo mwili
kutokea: 1. Kuwa tawi la Mzabibu (kuokoka), na 2: Kutembea na Bwana [ndani yake
tunaishi na tunakwenda (Mdo.17:8)], kwa maana PASIPO yeye HATUWEZI neno LOLOTE!
(Yh. 15:5).
Kilicho
mvuruga mfalme Sauli, ilikuwa ni kufanya HUDUMA pasipo kujua NENO la Mungu la
wakati huo! Akafukuzwa kazi.
ii. Je! Unajua Vipawa Vyako?
Kwenye
mfululizo wa somo hili, tumeona kwamba KUSUDI linaumbwa kabla hujazaliwa. Huji
duniani halafu ndio Mungu atafute kazi ya kukupa, umekuja duniani kwa sababu kuna
kazi yako maalumu iliyofichika katika ulimwengu wa roho. Hiyo kazi ndio inaitwa
KUSUDI au WITO.
Sababu
za KUFICHA kusudi ndani yako ni ili “umtafute Mungu, hata kwa kupapasa-papasa”
na umwone kwakuwa hayuko mbali nawe (Matendo ya Mitume 17:28). Kwa hiyo Mungu amekuwekea
tayari KUSUDI na MIPAKA ya makazi yako. Ukitaka kujua, jenga UHUSIANO mzuri
Naye, kaa ndani Yake (Yohana 15:5) na tembea ndani Yake (Matendo ya Mitume
17:26), utajua hilo kusudi na wito wako.
Watu
waliowahi kuniuliza swali kwamba, Je!
Nitajuaje wito wangu? Wengi nimewauliza swali pia, Je! Unajua VIPAWA vyako?
Kwa
bahati mbaya sana, wengi wa wanaouliza hili swali, hawana uhakika kwamba VIPAWA
vyao hasa ni nini!
Kwa
lugha nyingine, VIPAWA vimeitwa VIPAJI. Sasa uwe makini, sio kila UNACHOWEZA
kufanya ni KIPAWA chako. Unaweza kupenda kufanya kitu katika FANI fulani, na
ukaweza kweli, lakini sio KIPAWA/KIPAJI chako.
Kwa
lugha nyingine, unaweza KUTAMANI kipawa na UKAJIENDELEZA kwa kusoma na kufanya
KAZI kwa bidii na ukaweza! Sio kosa. Swali ni Je! Unafanya hivyo ili utimize
KUSUDI la Mungu?
“Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia
iliyo bora” (1 Wakorintho 12:13).
Lakini,
kuna watu wanajikuta WANAWEZA kufanya kitu fulani kwa namna TOFAUTI na
wanafanya kwa WEPESI sana kitu hicho; Kwa sababu WAMEPEWA KUWEZA kukifanya.
Kimo ndani yao! Hicho ni kipawa/kipaji.
Wengi
hawajui kwamba hicho wafanyacho ni kipaji kwa sababu wakifanya, wanafanya kwa
URAHISI hadi hawaoni kwamba ni kitu MAALUMU sana. Hawatoi jasho kufanya, hawajakitesekea
sana! Basi thamani huwa chini sana kwa mwenye KIPAJI chake, ndio maana wengi
hawavioni!
Ukiwauliza
watu wengi wenye VIPAJI fulani vikubwa, watakwambia kwamba kuna MTU aliwaambia
kwamba WANAWEZA jambo fulani, wakatiwa MOYO au wakaSAIDIWA kwa namna fulani.
Walipoona THAMANI ya VIPAJI vyao, hawakuwa tena kama walivyokuwa! Kipaji kina
mwinua yeye alichonacho na kumkutanisha na wakuu!
“8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni
pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa” (Mithali 17:8).
Kumbuka,
umepewa KIPAJI/KIPAWA kwa sababu ya KUSUDI fulani maalumu. Kipaji ni kama
KITENDEA-KAZI cha kutimiza hilo KUSUDI uliloitiwa na Mungu. Je! Unajua VIPAJI
vyako? Hapo ndipo KUSUDI lilikoJIFICHA.
Bado
namtazama mfalme Sauli kujifunza habari za KUSUDI, japo nitatumia na mifano ya
watu wengine.
Angalia
VIPAWA vya Sauli kabla hajaitwa;
“1 Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini,
jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi,
mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu.2 Naye alikuwa na
mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa
Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa
mrefu kuliko watu wote” (1 Samweli 9:1, 2).
Wakati
wana wa Israeli wanafikiri kuwa na mfalme, ilikuwa ni vipindi vigumu kwa
USALAMA wao na nchi yao. Kwenye mataifa mengine kulikuwa na wafalme. Moja ya
kazi za wafalme ilikuwa KUPIGANA vita na KUTWAA nyara za vitu, watu na ardhi,
kwa sababu za kiuchumi au za kiusalama.
Katika
hali ya kukosa usalama, wana wa Israeli nao wakatamani wawe na mfalme wao kama
mataifa walivyo na wafalme. Walitaka mtu atakayesimama katika nafasi ya juu ya
uongozi, ambaye pia atawaoka na adui zao.
Basi
Mungu akatafuta mtu ambaye ndani yake kuna KIPWA cha KUPIGANA vita.
Alipoangalia familia mbalimbali, mtu mwenye SIFA kwa KAZI iliyopo mbele, akamwona
mzee Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa
Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa,
mwenye nguvu. Alipotazama tena, akamwona kijana wake, Sauli!
Biblia
haituonyeshi Sauli akijifunza vita, bila shaka alipata SHULE ya kupigana kwa
baba yake, mzee Kishi. Kwahiyo, wakati Sauli anapakwa MAFUTA, alipewa kazi
mbili moja kwa moja: kumiliki watu wa
BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui
zao! Mungu alijuaje kwamba Sauli anaweza? Aliangalia VIPAWA vyake ndani
yake!
“1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta,
akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! BWANA hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe
utamiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara
kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake” (1
Samweli 10:1).
Angalia
sifa za Daudi kabla hajapakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli.
“18Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema,
Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita,
anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye. 19Basi
Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja
na kondoo. 20Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai,
na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. 21 Daudi
akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa
mtu wa kumchukulia silaha zake” (1 Samweli 16: 18-21).
Wakati
Sauli anashindwa KUTIMIZA kusudi la Mungu kwa sababu ya kushindwa KUTII neno (1
SAM. 13:13-4), Mungu
akaona mtu mwingine mwenye SIFA (VIPAWA) (1 Samweli 16: 18-21) kama vya Sauli,
lakini MWELEKEVU wa moyo! Daudi, mwana wa Yese, (Zaburi 89:20,21).
“Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo
wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe
hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru” (1 Samweli 13:14).
Unapoona
UNALAUMIWA kwenye nafasi yako ya kazi kwa sababu ya UTENDAJI wako mbovu, halafu
ukaona tangazo la nafasi ya kazi (vacancy) la kutafuta mtu mwenye sifa zako, wakati
wewe upo kazini, jua wakati wa KUPUNGUZWA kazini umefika! Sauli hakuweka hilo moyoni wakati nabii
Samweli alipompa ‘barua ya’ ONYO! (1 Samweli 13:14).
Kwa
wanaofuatilia maandiko, watakwambia kwamba tangu nabii Samweli asema kwamba
Sauli hafai, kwenye 1 Samweli mlango wa 13; Daudi alipakwa mafuta baadae sana,
kwenye 1 Samweli mlango wa 16. Hapo katikati na baada ya hapo, Sauli aliendelea
na kazi zake za KUPIGANA na maadui wa Israeli na alishinda vita kama kawaida.
Lakini, alikuwa AMESHAFUTWA kazi! Na nafasi yake katika ulimwengu wa roho
alikuwepo Daudi tayari kama mfalme (1 Samweli 13:14).
Katika ulimwengu wa mwili, pale ikulu, Sauli
alikuwa mfalme bado, tena mwenye nguvu, ndio maana wakati Mungu anamtuma
Samweli kwenda kumpaka Daudi mafuta, alihofia USALAMA wake; Yaani, aliona
HATARI ya kutangaza mfalme mwingine (Daudi) wakati mfalme Sauli bado yupo
kitini! (1 Samweli 16:1, 2a).
“1 BWANA akamwambia Samweli, Hata lini
utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako
mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia
mfalme katika wanawe. 2Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata
habari, ataniua” (1 samweli 16:1, 2a).
Angalia
jambo jingine, Daudi alikuwa na VIPAWA vya KUPIGANA tayari wakati akipakwa
mafuta. Lakini alihitaji UJUZI wa kuwa JUU ya watu wa Mungu (Leadership skills).
Mungu akampa NAFASI ya kujifunza KAZI za Sauli kwa Sauli wakati Sauli hajui
kwamba anamfundisha kazi mrithi wa nafasi yake!
Licha
ya kupewa AJIRA kule ikulu, ili ajifunze kwa VITENDO, Daudi alipelekwa VITANI
pia, tena mstari wa mbele kwa JEMADARI wa vita, mzee Sauli (mfalme), akawa
mbeba silaha za Sauli vitani, ili AJIFUNZE jinsi ya kupambana na ADUI za Mungu,
japo alikuwa HODARI tayari na KUFAULU mitihani yake ya kupambana na DUBU na
SIMBA kule kondeni. Safari hii alitakiwa KUJIFUNZA vita vya aina nyingine (1
Samweli 16: 18, 19 & 21).
Kilichompa
Daudi nafasi na kazi kule ikulu ilikuwa ni VIPAWA vyake vya kupiga kinubi.
Kilichompa kazi ya kuwa mbeba silaha wa mfalme Sauli ni VIPAWA vyake vya
kupigana.
Angalia
tena hapa,
“18Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake
akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni
mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu
pamoja naye. 19Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee
Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo [.……..]. 21 Daudi akamwendea Sauli,
akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye
akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake” (1 Samweli 16: 18, 19
& 21).
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni