Jumanne, 21 Julai 2015

MTUNZI WA "NAMSHANGAA BWANA YESU KILA NIENDAKO NAMKUTA" AMETOKA KWENYE UKOO WENYE KARAMA YA UIMBAJI NA KICHUNGAJI.
Peterson Hermas ni mzaliwa wa kijiji cha Bungoi Kata ya Mlalo Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga yapata miaka 45 iliyopita. Ameoa mke aliyefunga naye ndoa ya madhabahuni mwaka 1995 na Mungu amewajalia watoto watatu Hans, Paschal na Laura. Kwa sasa anaishi jijini Dar es Salaam, Kata ya Kibamba, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Mtumishi Peterson anatoka katika familia ya Kichungaji pia ya kimuziki, kwani mwaka 1952 marehemu babu yake Mch. Joshua Hermas ni kati ya Wachungaji walioteuliwa kwenda Ujerumani kupata kozi ya Uchungaji. Babu yake huyu alipokuwa Ujerumani katika kozi yake hiyo ya Uchungaji, alibahatika pia kujifunza somo la muziki kwa ajili ya kufundisha katika Usharika pindi arudipo kutoka masomoni Ujerumani.  Baada ya kurudi toka Ujerumani akiwa amebobea katika fani ya muziki akiwa na uwezo wa kutumia kinanda, tarumbeta, violin, aliona umuhimu wa kurithisha kizazi chake kipawa hicho cha muziki na akaamua kuifundisha familia yake (wazazi wa Peterson) muziki ambapo nao wakaja kuwa na upako na weledi katika tasnia ya muziki.
Mwaka 1982 baba yake Peterson mzee William Hermas (marehemu) naye akabahatika kupelekwa Ujerumani kufuatia kutunga wimbo na kuutuma Ujerumani na Wajerumani walipoupokea walistaajabu, hawakuweza kuamini jinsi muziki ulivyoandikwa kwa ustadi tena kwa mkono tu bila mashine ya chapa na ulivyopangiliwa kwa kila chombo cha muziki kama tarumbeta, kinanda, violin, gitaa, ngoma n.k. ndipo walipomtumia baba yake Peterson mzee William Hermas tiketi ya ndege ili aende Ujerumani wakamuone uso kwa uso. Mzee William Hermas akaenda na kupokelewa vizuri. Katika ibada ya siku ya Bwana, mzee William Hermas alipoitwa kuuimba wimbo wake huo, aliomba wapiga vyombo wote na kwaya zote ambapo jumla yao ilipata watu 80; ziimbe pamoja wimbo huo wakiufuatisha kwenye maandishi yake [noten] na kusisimua Washarika waliohudhuria ibada hiyo na kuleta maadhi ya tofauti kabisa kuwahi kutokea katika uimbaji Kanisani pale, ikawa furaha kuu katika Usharika ule aliofikia baba yake Peterson uitwao Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Minden, habari hii ikawa gumzo kiasi cha Meya wa jiji kuomba mzee William Hermas apelekwe kuonana naye, mzee William Hermas akapelekwa kuwa mgeni maalum wa Meya na habari zake zikaandikwa katika gazeti likiwa na kichwa “Mtanzania aliyetunga wimbo uliopigwa na watu themanini pia aliyetufundisha kula ugali.”
Pindi mzee William Hermas alipofika Ujerumani alikuta wamelima na kuvuna mahindi ambayo yalikuwa wanapewa mifugo kama ng’ombe, punda na farasi. Mtumishi William Hermas akawaambia “sisi kwetu Tanzania hiki ni chakula cha binadamu walakini ninyi hapa mnawapa mifugo?” Akawaambia waandae mahindi yakasagwe, akawafundisha jinsi ya kupika chakula cha ugali, ukapikwa ugali ulioliwa na wale watu wote pale Usharikani siku ya Jumapili. Wajerumani wakapenda sana chakula cha ugali na hiyo ikawa habari gazetini na akawafumbua macho Wajerumani wale kujua kuwa kumbe wao walijua ni chakula cha mifugo lakini kwa wengine ni chakula cha binadamu!, wakajifunza jambo jipya na Mtumishi wa Mungu William Hermas akafanyika baraka kwao kwa namna mbalimbali na sio tu ule wimbo aliotunga ulioitwa “Mungu Aliupenda Ulimwengu” aliourejea katika kitabu cha Yn.3:16  “kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee ili kila amwaminie asipotee bali awe na uzima wa milele”
Mkurugenzi wa muziki katika chuo cha muziki cha jiji hilo la Ujerumani aitwaye Reinhard Neuhaus ambaye naye ni Msharika wa Minden akabarikiwa sana na Mtumishi William Hermas kiasi cha kumjumuisha William Hermas katika chuo chake cha muziki na akaamuru William Hermas pekee kati ya wanachuo wote akae nyumbani kwake. Wakaja kuwa marafiki wakubwa kiasi cha kutembeleana Tanzania na Ujerumani kwa vipindi tofauti.
Baada ya William Hermas kufuzu mafunzo yake alirejea nyumbani Tanzania kuendelea na huduma, naye kama baba yake Mch. Joshua Hermas akaja kuwafundisha watoto wake muziki wakiwemo Dickson, Witness, Regina, Janeth, Rehema, Grayson, Upendo na Peterson aliyepata mafanikio katika tasnia ya muziki kwa kuwa maarufu kwa wimbo wake wa pambio wa “Namshangaa Bwana Yesu Kila Niendako Namkuta.” Mwaka 1977 Mtumishi William Hermas aliwakusanya watoto wake na majirani wachache akaunda kikundi cha kwaya alichokipa jina “Kwaya ya Mahubiri(C.Y.M)” kwaya ambayo ilikuwa maarufu pale Usharikani Mlalo-Hoheni ambapo Mtumishi William alikuwa na upako na uwezo wa kughani wimbo mpya kila Jumapili akirejelea somo la mahubiri la siku hiyo na kwaya hii ikawa inaimba somo hilo la mahubiri pale Usharikani na ukawekwa utaratibu kwamba kabla ya mahubiri kwaya ile lazima iimbe kwanza wimbo wenye somo la mahubiri.
Kwaya ya C.Y.M ikaja kuwa gumzo pale Usharikani kwani ilikuwa kwaya iliyojumuisha familia nzima ya baba, mama na watoto. Mtumishi William Hermas hakuwa na mzaha katika suala la kuhudhuria mazoezi kwa watoto wake kitu kilichowajengea nidhamu njema katika suala la kumtukuza na kumwimbia  Mungu. Mtumishi Peterson Hermas anasema kipekee anamtukuza Mungu kwa ajili ya baba yao William Hermas kwa msingi mzuri aliowawekea na kuwarithisha watoto wake kipawa hiki cha muziki ambao mbegu aliyopanda baba yao kwao sasa imeota kwa mafanikio makubwa sana kama tunavyoona hivi sasa watoto wa William Hermas wakihudumu kwa kufyatua nyimbo zenye upako na mvuto sana. Kwaya ya C.Y.M ilikuja kutia nanga ya huduma kufuatia waimbaji wake kuwa watu wazima waliolazimika kuanza maisha yao sehemu mbalimbali japokuwa hawajaacha kutumika hata huko walikotapakaa katika Sharika mbalimbali.
Peterson Hermas aliyetoa ushuhuda huu sasa yuko jijini Dar es Salaam akihudumu katika Usharika wa Kurasini Lutheran. Pale ana huduma ya kinanda cha Usharika na kufundisha kwaya ya Nuru ya wamama. Kaka yake Dickson Hermas yeye yuko pale Hai Moshi Sanya Juu, akihudumu kama Mwalimu wa kwaya, tarumbeta na kinada cha Usharika. Mdogo wake Grayson Hermas yeye yuko Usharika wa Kisosora Tanga naye akiwa katika huduma hiyo hiyo ya uimbaji katika nafasi ya Mwalimu wa kwaya na pia tarumbeta na kinada. Familia hii inamtukuza Mungu kuwaweka shambani kwake kulisha kondoo zake.
Ushuhuda ufuatao unahusu namna Mtumishi wa Mungu Peterson Hermas alivyoibua wimbo wa “Namshangaa Bwana Yesu Kila Niendako Namkuta.”
Ilikuwa Jumapili moja nilikuwa napiga kinanda Usharikani kwetu kule Mlalo Lushoto Tanga, alialikwa baba yangu mdogo kuja kuhubiri pale Usharikani. Kama nilivyokwisha kuelezea juu ya familia yetu kuwa ni ya Kichungaji na kimuziki, tukajikuta katika ibada ile baba ni mhubiri, mimi mtoto wake ni mpiga kinanda. Hali ile ilimfurahisha sana baba yangu mdogo Mch. Richard Hermas. Mara baada ya Ibada, akanitaka nijiandae niondoke naye nikahudumu Usharikani kwake Irente nje kidogo ya mji wa Lushoto. Nikatii wito ule nikatoka pale Usharikani nikamwacha baba yangu mzazi mzee William Hermas  akichukuwa nafasi yangu ya mpiga kinanda pale Usharikani akisaidiana na mzee aitwaye  Nkanileka Shekolowa (marehemu).

Pale Usharika wa Irente nikapewa jukumu la kufundisha kwaya kuu na tarumbeta. Usharika ule wa Irente ulikuwa na vituo vitatu vya huduma; kituo cha watoto yatima, kituo cha watoto wasioona na kituo cha wagonjwa wa akili. Baba yangu mdogo Mch. Richard Hermas alikuwa pia mkuu wa Kituo cha wagonjwa wa akili akaniomba nijiunge na wenzangu 9 niliowakuta pale katika huduma ya wagonjwa kwani wagonjwa walikuwa wengi zaidi ya 90, nikajiunga katika huduma hiyo ngumu, nikajiuliza nitamudu vipi kazi ile ngumu ya kusimamia na kuwaongoza watu wale? Wenzangu niliowakuta pale namshukuru Mungu kwa ajili yao kwani walinitia moyo sana ukichukulia nilikuwa kijana mdogo. Kipekee ninamshukuru baba yangu mzee Tahona Shemkole aliyekuwa bega kwa bega nami katika huduma ile ya wagonjwa wa akili.
 
Nikiwa pale, mkuu wa kituo cha watoto yatima mama Betty Hozza alikuja kuniomba nikawafundishe wanafunzi (Wadada) waliokuwa wanajifunza mafunzo ya uuguzi pale kituoni huku wakiwahudumia/wakiwalea watoto yatima, nikaombwa nikawafundishe nyimbo kwa ajili ya mashindano ya Ukwata yaliyotakiwa kufanyika Tanga mjini. Kilikuwa kikundi kidogo cha wasichana 16 tu. Ikafika siku ya mashindano, tukasafiri kuelekea Tanga mjini tayari kwa mashindano. Tulipofika kule tukakuta wenzetu nao wamewasili kwaya mbalimbali na idadi ya kwaya ilikuwa 14. Wenzetu walikuwa wamekamilika kila idara, walikuwa na majoho mazuri, walikuwa wamekamilika wavulana na wasichana.
Wale wasichana wachache (wanafunzi) nilioenda nao wakaingiwa hofu wakajiona si kitu kwa jinsi walivyoona wenzao walivyo wengi na walivyojipanga, nikawaambia “msihofu Yesu wetu haangalii wingi wala mbwembwe” ninyi imbeni kama nilivyowafundisha na Bwana Yesu akawe mwamuzi. Nikajihudhurisha pembeni nikajitenga nao kwa kitambo nikamwomba Bwana Yesu atupiganie, kweli mwisho wa uimbaji kikundi hiki kidogo cha wadada (wanafunzi) wakawa wa kwanza, wakajawa na furaha kubwa. Tukiwa njiani ndani ya gari wakati tunarudi, wakaniambia Mwalimu sasa tunga wimbo twende tukiwa tunaimba. Nikawaambia “Mimi namshangaa Yesu kila ninapoenda namkuta na ananijibu.” Na huo ukawa mwanzo wa wimbo huu Namshangaa Bwana Yesu kila niendako namkuta.” Wimbo huu niliutunga mwaka 1995. Zipo nyimbo nyingi nilizotunga na kufundisha kwaya mbalimbali. Nimeisha hudumu kwa kufundisha kwaya Sharika zifuatazo:-
Kwaya kuu Usharika wa Huduma Irente Lushoto 1989 – 1995, Kwaya kuu Usharika wa Kariakoo 1996 – 1998, Kwaya kuu Usharika wa Kimara 1998 – 2001, Kwaya kuu Usharika wa Kawe 2001 – 2003, Kwaya kuu Usharika wa Kiluvya 2003 – 2006, Kwaya ya wamama ya Nuru Usharika wa Kurasini na huduma ya kinanda cha Usharika ninapohudumu hadi sasa.
 
Mji wangu ninamoishi, niliupata baada ya kupanda mbegu kwenye semina ya kupanda mbegu iliyoratibiwa na New Life In Christ Ministry na kuhudumiwa na huduma ya MANA ya Watumishi wa Mungu Mwl. Christopher na Diana Mwakasege Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam baada ya jasho jingi, kusubiri kwingi na muda mrefu sana wa kutamani kumiliki makazi yangu binafsi. Ndani ya mwaka mmoja wa kupanda mbegu, namshukuru Mungu aliziotesha na kuzikuza ambapo nilipata kiwanja na kukamilisha ujenzi na kuhamia ndani ya mwaka huo huo mmoja. Mwisho.
 
Babu yake Peterson Hermas Mch. Joshua Hermas alikuwa mwanamuziki aliyerithisha watoto wake kipawa cha muziki na karama ya Kichungaji na watoto wake Richard Hermas akaja kuwa Mchungaji na William Hermas akaja kuwa Mwanamuziki wa Injili ambaye naye baada ya kwenda Ujerumani kama baba yake Mchungaji Joshua Hermas; akaja akawarithisha watoto wake wote wanane na mke wake kipawa cha muziki na akaunda kwaya ya familia yake aliyoiita C.Y.M na sasa watoto wake hawa wote wanane wakike na wakiume wanahudumu kwenye uimbaji wengine wakiwa kwenye nafasi za ualimu wa kwaya na vyombo ambapo wameunganisha vipawa vyote viwili vya nyimbo na vyombo. Huu ni ushuhuda wenye uvuvio zaidi ambapo kizazi chote tangu babu hata wajukuu wote wako kwenye huduma ya Mungu ya Uimbaji na Kichungaji.  

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Chapisha Maoni