Kwa kiasi kikubwa ni bara la Afrika ambapo pana msuguano mkubwa kati ya
dini na siasa kuliko bara la Ulaya ambalo ndilo lina kiwango cha juu cha
ustaarabu lakini misuguano baina ya viongozi wa dini na wale wa siasa ni nadra
sana kutokea. Kijapo kipindi cha uchaguzi ndipo misuguano hii huwa inakolezwa
sana kuliko kipindi kingine kiwacho chote kile. Kama kuna sababu kubwa
iliyofanya Mungu akaadhibu wafalme na falme zao basi ni kukataa maagizo ya
Mungu aliyowafikishia Wafalme kupitia makuhani wake.
Kimsingi nahisi ni suala la kukosa maarifa ya Neno la Mungu kwa upande wa
wanasiasa ambao nao wanatoka kwenye nyumba hizi hizi za ibada ambazo zinatumia
misaafu kufundishia Neno la Mungu, lakini inaonekana wanasiasa wakiishatoka
kwenye nyumba za ibada na wakiishatumia misaafu hii kula kiapo basi wanaachana
kabisa na habari ya imani hadi pale wanapohisi wameingia kwenye matatizo ya
kisiasa ndipo wanakimbilia tena nyumba za ibada kuomba maombezi ya kuokoa
mustakabali wao. Hii ni sanamu!
Biblia iko wazi kabisa jinsi ambavyo
Watumishi wa Mungu walikuwa na kibali cha kuingilia kati siasa [political
intervention] kwenye falme za nyakati za Biblia na wakafanikiwa sana kuokoa hali
ambazo zilikuwa zinaenda ndivyo sivyo na hata kuokoa uongozi wa wafalme hao
kama siyo kuokoa ufalme mzima.
Hapa ndipo pana msingi na kibali cha
viongozi wa leo wa dini kuingilia siasa na kwamba Neno la Mungu lililowapa
Watumishi wake wa nyakati za Biblia kuingilia siasa halijabadilika hata leo,
bado ni hilo hilo linalowapa kibali Watumishi wa Mungu/viongozi wa dini wa leo
kuingilia kati siasa ili kuokoa mustakabali wa nchi zao.
Ebu tuone ushahidi wa kimaandiko wa
Watumishi wa Mungu wa nyakati za Biblia walioingilia siasa ili kuokoa hatma ya
watu katika falme hizo: Yusufu aliingizwa kwenye siasa kwa amri ya Farao
mwenyewe na kuiokoa Misri Mwa.37:21-36; 39:40; 41:41-45. Danieli
aliokoa ufalme wa Dario kutoka utawala wake kufitinika na mfalme akaagiza kuwa
watu wote wa ufalme watetemeke mbele za Mungu wa Danieli Dan.6:26.
Daniel akafanikiwa sana katika enzi za wafalme Dario na Koreshi Mwajemi Dan.6:28.
Watumishi wa Mungu Nabii Eliya
Mtishbi na Gideoni walipindua miungu ya falme kwa kuwachinjilia mbali kondeni
manabii 450 na kuthibitisha kuwa Mungu wake ndiye Mungu wa kweli 1Fal.18:21,
22-40; Amu.6:27. Wafalme
waliabudu miungu hii ndiyo maana waliruhusu manabii hawa wa uongo kuwepo
miongoni mwao kwenye falme zao na huenda waliwapa usajili wa kiserikali kufanya
shughuli zao za kinabii zilizoegemezwa kwa miungu ya uongo. Sijajuwa
ilimgharimu Nabii Eliya siku ngapi kumaliza kuwaua wale manabii wote 450? Na nachelea
kutafakari jinsi ya huo mstuko wa msiba mkuu namna hiyo kuipata dunia.
Mtumishi
wa Mungu Yona alisafirishwa tumboni mwa samaki kwa amri
ya Mungu bila
kufa hadi Ninawi na akafanya huduma yenye upako mkuu Yon.1-4 na kuifanya Ninawi
kuweka rekodi duniani na kwa Kanisa; ya mfungo ambao haujawahi kutokea mfano wake
isipokuwa ule mfungo wa YESU tu. Mfalme hakuwataka kabisa viongozi wa dini
[watumishi wa Mungu], na Yona alipokwenda kwa mara ya kwanza alitishiwa kuuawa
au kufungwa jela kwa sababu anakosoa siasa za Mfalme na kuleta mafundisho
mageni ambayo siyo ya ufalme lakini mfumo [siasa] wa uendeshaji ufalme ulimkwaza
Mungu, ndiyo maana Yona alipoambiwa na Mungu arudi mara ya pili Ninawi akaogopa
matishio ya Mfalme na kuamaua kutoroka kwa merikebu.
Lakini
kwa kuwa Mungu hakwepeki, Yona hakuwa na namna bali kwenda kuingilia siasa za
Ninawi ili iokoke na ghadhabu ya Mungu ya kutaka kukizamisha kisiwa cha Ninawi
chini ya bahari kwa kukumbatia uasi kwa Mungu wa kweli. Mfalme alibaini kuwa
Yona amepewa kibali kuingilia mfumo wa utawala wa Mfalme na ujumbe wa Mungu
kupitia kwa Yona ukamuingia Mfalme na kutoa amri [decree] ya ufalme wote kufunga
kwa maombi tena akaenda mbali zaidi kwa kuamuru hata mifugo nayo ifunge, hakuna
kula wala kunywa, kisiwa chote kikawa kinanyeshewa tu mvua ya machozi kwa siku
tatu mfululizo na ufalme na utawala wa Mfalme vikasalimika.
Yesu
Kristo Nabii wa mwisho katika safu ya Manabii wa Mungu wa nyakati za Biblia,
alifanya huduma yake kwa kuzishauri falme e.g. wakati anawaambia watu wampe
Kaisari yaliyo yake maadamu sura yake iko kwenye sarafu. Ingekuwa ni leo Yesu
anaingilia serikali za falme/nchi za nyakati za leo je, wanasiasa wangefanyaje?
Je, wangemtundika msalabani? Biblia inasema kazi alizoacha Yesu ndizo hizo
wanazofanya Watumishi wa Mungu wa leo na hii inamaanisha kazi ya kuzishauri na
kuingilia kati inapobidi; utendaji wa serikali na wanasiasa.
Sasa wale
wanaojaribu kuwafunga midomo viongozi wa dini wa leo kutokuingilia siasa hata
kama nchi inateketea kwa kigezo kuwa wanaingilia eneo lisilo lao nawaona kama
wana tatizo la ombwe kubwa sana la maarifa ya Neno la Mungu na wanastahili
msaada wa dharura kuwaokoa ili waendelee kustahili madaraka yao. Tena ni
afadhali viongozi wa dini kukemea siasa na uendeshaji mbovu wa mifumo ya
serikali wakiwa kwenye huduma zao kuliko wakiingia ndani ya siasa na serikali
ambako tumeona wakibezwa sana na mamlaka zao za kihuduma zikisongwa/zikitingwa
na sintojuwa za mifumo iliyopo ya kuendesha nchi. Naamini watafanikiwa zaidi
kuzishauri serikali wawapo kwenye huduma zao madhabahuni kuliko wakiwa ndani ya
serikali hizo, bungeni na kwenye vyama vya siasa.
Ebu sasa tuone ushahidi wa nyakati
hizi ambapo viongozi wa dini wameweza kwa ujasiri mkuu kuingilia kati na kuokoa
hatima za nchi zao: Nchini Kenya Ask. John Henry Okulu wa CPK [Anglican] Dayosisi
ya Maseno na Ask. Alexander Muge wa CPK Dayosisi ya Eldoret walivyotumia
madhabahu zao vizuri kukemea na kusahihisha mwenendo wa siasa katika nchi yao.
Mch. Canaan Banana alipigania uhuru
wa Zimbabwe hadi akaja kuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe huru, Ask. Pius Ncube amejitokeza
hadharani na kusimama kidete kukosoa njia ambayo siasa za nchi yake zilichukuwa
na kuifanya Zim kuwa kisiwa katika nchi kavu duniani na kuporomosha uchumi wa
taifa [The highest inflation in the world “Hyperinflation”] na raia kuogelea
kwenye umasikini.
Ask. Desmond Tutu sote tunajuwa mchango
wa color yake ya kiaskofu na Biblia yake vilivyoleta ukombozi Afrika Kusini. Mchango
wake uliongezea nguvu kubwa jitihada zilizopwaya za wanasiasa wapigania
ukombozi. Kwa hivyo Watumishi wa Mungu wana kibali kuingilia masuala ya siasa
kukosoa, kukemea, kuhoji, kurekebisha, kushauri na kuokoa pia. Tena wao ni bora
zaidi kwa sababu hawafanyi kwa akili zao wenyewe bali wanafanya kwa karama
zilizo ndani yao na kwa kumuuliza Mungu kwanza juu ya hali ya nchi/ufalme ili
Mungu awape cha kufanya kwa hekima itokayo kwake.
Haiwezekani watu wanachunwa ngozi na
kukatwa viungo na wengine wazee kuuawa kwa kudhaniwa ni washirikina eti tu kwa
kuwa macho yao yamekuwa mekundu alafu viongozi wa dini wakijaribu kutathmini
utendaji wa dola katika kuzuia uhalifu huu na mwingine uwao wote ule waambiwe
kuwa wanaingilia siasa. Katiba ndiyo inalinda haki ya kila mtu kustahili kuishi
wakiwemo watu wenye ulemavu wa ngozi, sasa viongozi wa dini wakijaribu kudurusu
katiba ili iweze kuwa bora zaidi yenye kuwakilisha maslahi mapana ya jamii
nzima wanaambiwa wanaingilia siasa. Labda tuaminishwe kwamba tunaishi zama za
Herode na Pilato!
Wanasiasa wajuwe kuwa Mungu amewaagiza
viongozi wa dini wahubiri watu kutoua, kutochuna ngozi, kutokata viungo na
ukatili wa kila namna na Mungu atakuja kuwadai kuwa walihubirije agizo lake
katika Mik.3:2-3 2Ninyi
mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi yao,
na nyama mifupani mwao. 3Naam mnakula nyama ya watu wangu, na kuwachuna
ngozi zao, na
kuvunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa kutiwa chunguni, na
kama nyama sufuriani.
Pia tunasoma katika Mit.23:22 “Msikilize baba yako
aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako akiwa mzee.” Sasa wazee wanapouawa kwa
tuhuma za macho kuwa mekundu kuwa ni wachawi na wanasiasa wapo lakini jitihada
zao hazizai matunda kutokomeza ukatili huu, kwa nini viongozi wa dini
wakiingilia kuhoji ufanisi wa utendaji wa wanasiasa wanatishiwa?
Ninawatia moyo viongozi wa dini kuwa
wajichukulie kuwa wametumwa kuhubiri habari za Mungu kama kondoo katikati ya
mbwa mwitu. Eze.2:6 “Na
wewe, mwanadamu usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na
michongoma i pamoja nawe, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao,
wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.” Tunaangamia kwa kukosa maarifa Hos.4:6.
Mbona viongozi wadini wanapojenga
miradi ya maendeleo ya Kanisa kwa ajili ya jamii nzima huwa wanasiasa hawahoji
kuwa kwa nini wanawaingilia kwenye kazi zao? Mbona hawahoji kuwa viongozi wa
dini wanatekeleza ilani ipi ya uchaguzi? Mbona miradi ya maendeleo ya Kanisa
ndiyo iliisimamisha nchi hata leo tangu uhuru? Wanasiasa hawa hawa wamejengwa
kwenye shule za Kanisa. Wanasiasa wajuwe kuwa viongozi wa dini siyo wapinzani
ambao hata wakifanya cha maendeleo ya umma katika majimbo yao bado watasukumwa
sana. Bado tunakumbuka neti za hospitali ya Temeke zilivyopata tabu kukubalika miaka
ileee zilipotolewa kama msaada na kiongozi mmoja wa upinzani katika jimbo hilo.
Je, wanasiasa wa Afrika wana utandu
ulioziba mboni zao zisione hata mema? Mbona mauaji yanaposhindikana kutokomezwa
kwenye jamii wanasiasa hao hao wanawaomba viongozi wa dini kuongeza bidii ya
kufundisha Neno la Mungu ili jamii isiangamie na kuwa kama namna ya kujisafisha
kwa wafadhili?
Bara la Afrika lisipothamini nafasi ya
viongozi wa dini kama wadau wa msingi na muhimu sana katika kuendesha nchi na
lisipofanya marekebisho ya mwenendo wa uendeshaji wake basi nachelea kusema
maandiko haya yaweza kutimia:
Maombolezo.4:17 “Macho yetu
yamechoka kwa kuutazamia bure msaada wetu; katika kungoja kwetu tumengoja taifa
lisiloweza kutuokoa.”
Mhubiri.10:5-7 “5Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo
ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye: 6ya kuwa upumbavu
huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi hukaa mahali pa chini. 7Mimi
nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama
watumwa.”
Kwa hisani ya Majwala.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni