“Basi
Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu
wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi
majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je!
Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini
yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo”
(Ayubu 2:7-10).
Katika kufuatilia kwangu habari za
Ayubu, kuna jambo limenishangaza sana. Mke wa Ayubu alipoonekana kwenye kitabu
cha Ayubu mlango wa 2, wakati anakemewa na mumewe, hakuonekana tena hadi
milango ya mwisho ambapo tunasikia Ayubu alizaa tena wana na mabinti. Jambo
jingine, katika habari zote za Ayubu, hakuna mahali nimeona akisimulia MATENDO
ya mkewe kwake au kwa Mungu ila nimesikia akisema habari za WATOTO, MALI zake na
watu wengine.
Wakati Ayubu anakumbukia maisha yake ya
zamani kabla ya pigo la adui, ametaja mambo mengi anayoya-miss ila hakutaja
mkewe! Ayubu anakumbuka jinsi watoto wake walivyozunguka meza yake (Ayubu 29:5),
jinsi alivyokuwa na heshima yake kwa jamii inayomzunguka (Ayubu 29:7-10) na
jinsi alivyotembea na Mungu wake (Ayubu 29:2-6), hakuna mahali ameeleza kwa
UZITO jinsi alivyoishi kwa FURAHA na mkewe! Najiuliza, je! Ayubu alisahau
kusema habari NZURI za mkewe au hazikuwepo?
Je! Kama alisahau, mbona hatuoni huyu mama akiketi majivuni na mumewe na
kumkuna mgongoni kwa kucha zake hadi Ayubu anajikuna kwa kigaye? Je! Huyu mama
hakuwa mfariji wakati wa MAPITO haya au alizira kwa sababu aliitwa ananena kama
mwanamke mpumbavu huku mwanzo?
Nikatafakari tena nyakati na majira
nikaona jambo jingine. Fikiri katika nyakati zetu (Ayubu angekuwepo sasa), baba
anamwambia mkewe, “wewe umenena/tenda
kama mmoja wao wa hao wanawake wapumbavu” kwa sababu kweli mkewe amenena jambo
la kipumbavu lisilopaswa kunenwa au kutendwa kwa jamii ya waaminio! Fikiri huyu
mama angejibu au kufanya nini? Kwa wakati wa Ayubu, kutafuta mwanaume mwingine
maana yake ni kusaini hati ya kifo, yaani kupigwa mawe hadi kufa. Kwa hiyo, yamkini
kilichomshika huyu mwanamke “mpumbavu”
sio hofu ya Mungu wala upendo kwa mumewe ila ni hofu ya kupigwa mawe hadi kufa!
Fikiri mke wa Ayubu wa sasa, piga picha ndani ya kanisa, wala usiangalie nje.
Je! Unaona nini?
Ukitaka kujua habari ya nyakati na
majira, angalia hapa, kuna kundi kubwa jingine la wapumbavu, ambao wana mfano wa utauwa, “ 1 Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako
nyakati za hatari. 2Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye
kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi
wao, wasio na shukrani, wasio safi, 3wasiowapenda wa kwao, wasiotaka
kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda
mema, 4wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda
Mungu; 5wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao
ujiepushe nao. 6Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba
za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi,
waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi; 7wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli. 8Na
kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa
wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa
mambo ya imani. 9Lakini
hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile
na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri” (2 Timotheo 3:1-9).
Nimeangalia na kujifunza makundi mawili
ya watu, wapo wamtafutao Mungu katika shida zao (wenye hekima na ufahamu)
(Ayubu 28:28) na wapo wamwachao Mungu katika shida zao (wapumbavu) (Ayubu
2:7-10). Wakati Ayubu anazungumza juu ya hekima, alisema, “Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu”
(Ayubu 28:28). Je! Umeona janga kwenye kizazi hiki? Naam, bila shaka kama
Mtume Paulo alivyosema juu ya nyakati, hizi ni siku za mwisho, utawaona siku
zote wakijifunza habari za Mungu ila hawafikilii UJUZI WA KWELI! Je! Mtu aweza
kufikilia ujuzi wa kweli bado akawaza kama mke wa Ayubu? Je! Mtu aweza
kufikilia ujuzi wa kweli, akawa HURU na akaendelea kutenda DHAMBI hasa za
makusudi? (Yohana 8:31,32).
Upumbavu maana yake ni kufanya jambo
ambalo mtu ANAJUA kwamba ni MAKOSA na ANAFANYA kwa MAKUSUDI tu, huyu ni mpumbavu. Je! Umeona
upumbavu katika jamii ya waaminio? Paulo anasema, “hawataendelea sana kabla upumbavu wao haujadhirika”. Huna haja ya
kupambana na gugu, wewe mtu wa Mungu shika njia za BWANA na uzidi kuimarishwa
kwa maana “waovu watazidi kuwa waovu na
watakatifu watazidi kutakaswa” (Ufu. 22:11; 2 Tim. 2:16), haleluya!
Ukiona waovu wanazidi kuwa waovu, na
uasi unaongezeka, hata wajuapo au waonywapo, jua saa imefika ya kuchunga roho
yako na imani yako, usije ukakasirishwa na kutahayari na kisha kuharibu uhusiano
wako na Mungu, kwa maana BWANA alituambia dalili za siku za mwisho, “Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo
wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia
hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mathayo
24:12, 13). Upendo kupoa
ni dalili mojawapo ya kurudi nyuma. Bila shaka UVUMILIVU wako ndio utakuokoa!
Bwana anarudi,
kwa hisani ya Frank Philip Seth.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni