Jumanne, 6 Januari 2015

PATA HISTORIA YA UTUNZI WA WIMBO NI SALAMA ROHONI MWANGU. When Peace Like a River. Tenzi 23.


 
Mtunga Liriki/Maneno: Horatio Gates Spafford 1828 - 1888.
Mtunga Vokali/Sauti: Philip Paul Bliss 9 Julai 1838 – 29 Desemba 1876

Mwandishi wa wimbo huu Horatio Gates Spafford alizaliwa yapata mwaka 1828 na kutwaliwa mwaka wa 1888 akiwa ameishi duniani kwa miaka ipatayo 60 tu. Mtunzi wa vokali/sauti/tuni anaitwa Philip Paul Bliss ambaye aliishi kwa miaka 38 tu hadi anatwaliwa Mbinguni. Wimbo huu hata hivyo kwa jinsi ya upako wake, umepewa sauti tofauti tofauti na zote zikiwa zina mguso ule ule zinapoimbwa.
Mtunzi wa wimbo

Mtumishi wa MUNGU Horatio Spafford, alikuwa mwanasheria na alikuwa tajiri sana. Aliishi na kufanya biashara zake huko Chicago Marekani. Alikuwa na familia ya watoto watano, mabinti wanne na mvulana mmoja. Pia alikuwa ni mkristo na mwanafunzi mzuri wa maandiko matakatifu. Katikati ya mafanikio yake, Horatio alimpoteza kijana wake mwaka 1870 aliyefariki kwa ugonjwa uitwao kwa lugha ya kiingereza scarlet fever unaosababishwa na bakteria. Akiwa bado anaendelea kuomboleza kifo cha mtoto wake mpendwa, tarehe 08 Oktoba 1871 siku ya Bwana [Jumapili] majira ya saa tatu usiku, moto mkubwa uliopewa jina la moto mkubwa wa Chicago [The Great Chicago Fire] ulianza na chanzo chake inasemekana ni ng'ombe aliyepiga teke taa ya mafuta iliyokuwa katika banda lake.
 
Moto huo ulisabisha vifo vya watu takribani 300 na uliteketeza eneo la karibu kilomita za mraba 9 na uliacha watu zaidi ya 100,000 bila makazi. Ni katika ajali hii ya moto, Mtumishi wa MUNGU Horatio alipoteza mali zake nyingi sababu aliwekeza sana katika eneo hilo la Chicago. Wakati biashara za Mtumishi Horatio Spafford zinaanza kufanikiwa, janga lingine likampata. Yapata mwaka 1873, biashara zake zikakumbana na anguko kubwa la uchumi [Great Economic Depression] lililoendelea hadi mwaka 1879. Anguko hili la uchumi lilisababishwa na sababu nyingi ikiwemo Moto mkubwa wa Chicago wa mwaka 1871. Kutokana na matatizo hayo yote ambayo familia yake ilipitia, Mtumishi wa MUNGU Horatio Spafford aliamua kuipeleka familia yake nje ya Marekani kwa ajili ya mapumziko na kujaribu kupunguza msongo wa mawazo [stress] kufuatia matukio hayo mawili ya ajali ya moto na anguko kubwa la uchumi vilivyowaathiri kama familia.
 
Wakaamua kwenda Uingereza ambako pia rafiki zake Moody na Sankey walikuwa wanafanya huduma ya kuhubiri Injili wakizunguka dunia nzima kupitia huduma ya utalii wa kiinjili ulioratibiwa na Pastor John Wilbur Chapman. Kama vile Roho Mtakatifu alikuwa anamzuia, muda mfupi kabla ya safari yao, alipata udhuru na ikambidi abaki ili kushughulikia masuala yaliyokuwa yamejitokeza katika biashara zake. Kwa kuwa muda wa safari ulikuwa umekaribia sana, aliiruhusu familia yake itangulie na kwamba yeye angefuata baadaye. Yapata tarehe 15 Novemba, 1873, familia yake wakiwemo mke na watoto wanne walianza safari kutoka New York kuelekea Ufaransa na meli iliyoitwa Ville du Havre.
 
Mnamo tarehe 22 Novemba, 1873, majira ya saa nane za usiku mnene, wiki moja tu baada ya kuanza safari, wakiwa ndani ya bahari ya Atlantiki, meli ya Ville du Havre iligongana na meli nyingine iliyoitwa Loch Ear. Takwimu za kikosi cha uokozi zilisema kiasi watu 226 kati ya 313 waliokuwa ndani ya meli ya Ville du Havre, walipoteza maisha na kusalimika watu 87 tu. Miongoni mwa waliopoteza maisha  walikuwemo watoto wote wanne wa Mtumishi Horatio Spafford. Mnamo Tarehe 1 Desemba, 1873, Mtumishi Horatio Spafford alipokea ujumbe toka kwa mkewe ambaye alinusurika katika ajali hiyo akimweleza, “...Ni mimi tu nimesalimika...”, “Ijapokuwa nimepata majaribu kiasi hiki [akirejea ajali ya moto iliyoteketeza mali zake, anguko kubwa la uchumi na ajali ya meli iliyoua watoto wake wote], nina furaha kwa sababu bado namwamini MUNGU”.

Haya ndiyo yalikuwa maneno ya Mtumishi Horatio baada ya yale ya mke wake. Wiki chache baadaye akiwa njiani kuelekea Uingereza alikokuwa mke wake, nahodha wa meli aliyokuwamo aliwataarifu kuwa eneo walilokuwa wanapita, ndipo ilipotokea ajali ya meli iliyouwa watu 226 wakiwemo watoto wake Horatio. Kwa majonzi na uchungu mwingi, Mtumishi wa MUNGU Horatio alichukua kalamu yake na karatasi, akaandika utenzi ambao baadaye ulikuja kuwa wimbo uitwao “Ni Salama Rohoni Mwangu”

Baadaye tena MUNGU aliikumbuka nyumba ya Mtumishi wake Horatio na akaibariki na watoto wengine watatu, wa kiume mmoja ambaye alikuja kufariki akiwa na umri wa miaka minne na mabinti wawili. Yapata mwaka 1881, familia ya Mtumishi Horatio ilihamia Yerusalemu, Israel na wakajihusisha na harakati za kusaidia wahitaji/masikini. Kikundi ambacho uasisi wake ulitokana na mwandishi Selma Lagerlof kushinda tuzo ya nishani ya Nobel mwaka 1909 kupitia kitabu chake cha hadithi kijulikanacho kama Jerusalem.


KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Maoni 6 :

Unknown alisema ...

Weka historia za nyimbo nyingine nyingi

Unknown alisema ...

Barikiwa sana

Bila jina alisema ...

Barikiwa sana

Bila jina alisema ...

Inatia moyo Kumtegemea Mungu Kuna faida

Bila jina alisema ...

Historia ya wimbo wa Tufani inapivuma

Bila jina alisema ...

Mungu kwetu nipendo anatujali