“Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni
yeye na wanafunzi wake, akawaambia,
Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. Nao walipokuwa
wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa
maji, wakawa katika hatari.
Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia.
Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari. Akawaambia, Imani yenu iko wapi?
Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru
upepo na maji, navyo vyamtii?” (Luka 8:22-25)
Kuna
jambo limekaa moyoni mwangu siku nyingi, nalo ni habari ya majaribu au vita
katika maisha ya imani. Jambo la msingi sana kujua ni kwamba “ulimwenguni tunayo
dhiki”, BWANA anajua, na akasema “tujipe moyo kwa maana Yeye ameushinda
ulimwengu” kwa hiyo “Aweza kuwasaidia na kuwaokoa
wote wajaribiwao kwa sababu BWANA pia alijaribiwa
katika KILA jambo” kama ilivyo sisi leo.
Mtume Paulo aliposema, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya
haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu,
bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake” (2 Timothy 4:6,7), inaonesha
kabisa kwamba Mungu aliruhusu VITA kwa makusudi ili PAULO apambane, na kuna
TAJI baada ya USHINDI. Kwa upande mwingine, Paulo hakusema “ni kwa neema tu”,
ila anasema “mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda”, hii inanipa picha ya
DHAMIRI ya dhati ndani ya Paulo ambayo ALIKUSUDIA kusimama katika MAPENZI ya
Mungu kwa hali zote, “akifa ni faida, akiishi ni kwa sababu ya kazi ya injili”.
Sihubiri kinyume na neema ya Mungu, ila nataka nikuoneshe umuhimu wa kutambua
kwamba kila mmoja wetu anawajibu wa kusimama katika zamu zake na kufanya yampasayo japo hatuishi
kwa sheri, na haki yetu haitahesabiwa kwa sheria, ila kwa imani. Ona mfano wa
BWANA na wanafunzi wake chomboni, BWANA hakushangaa TUFANI kwa sababu imeleta
vurugu pale, Aliwashangaa wanafunzi wake kwa kushindwa KUPAMBANA na tufani. Ona
tena, BWANA akauliza, “imani yenu iko wapi?” Je! Utasema unaimani pasipo
MATENDO? Kwanini basi kusema na kusingizia “neema tu” huku unishi maisha ya
aibu na hutaki kubadilika? Je! Maneno yako matupu na “Bwana asifiwe” nyingi
zaweza kukuokoa? Je! Uzidi kutenda dhambi ili neema iongezeke? La! Hasha. Acha
njia zako mbovu na mrudie BWANA.
Ni kweli “tunalindwa na
nguvu za Mungu kwa imani”, lakini imekupasa “kuomba bila kukoma” (yaani KUFANYA
jambo), imekupasa “kumtafuta Mungu kwa bidii, na tukimtafuta kwa BIDII ndipo
tunamwona JAPO hayuko mbali na yeyote kati yetu”.
Ona
tabia hii, “Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si
kitu kwako kuwa tunaangamia?” (Marko 4:35-41). Tabia ya kulaumu wengine au
Mungu kwa kushindwa kwetu kusimama kwa imani. Ikitokea tufani watu wanaanza
KUMLAUMU Mungu bila kujua kwamba huwezi
kuwa mshindi kama hakuna mashindano! Vita
sio jambo la kushangaa, kwa maana Mungu wetu jina lake ni “BWANA wa vita”, na
yeye hutuacha tuingie vitani ili tuuone mkono wake ukituokoa huku “akijionesha
mwenye nguvu kama mioyo yetu
imemwelekea”, jicho la BWANA linakimbi-kimbia duniani mwote kwa kusudi hili, “kujionesha mwenye nguvu”, Je!
Yupo mmoja aliye na uelekevu kwa BWANA asimwone
mwenye nguvu? Kama Bwana ni mwokozi jua unahitaji akuokoe, na wokovu hauishii siku ile umesema sala ya toba,
wokovu ni jambo la kuendelea, “kila atakayeliita jina la BWANA ATAokoka”. Mwite BWANA kwenye
mambo yako akuokoe.
Lipo
jambo jingine nimeliona, likanisumbua sana. Je! Umewahi kusikia mtu akisema,
“nikihama mtaa huu, nitaweza kusimama katika wokovu”, au “kama isingekuwa huyu
mke/mume, kiroho changu kisingekuwa hovyo namna hii”, nk., je! Umewahi
kujiuliza kama waovu wote wanaondolewa duniani, changamoto zote zingeondolewa,
Ibilisi amefungwa kamba milele, hakuna shida, pepo wala majaribu, je! Kungekuwa
na haja gani ya kuwa na BWANA ambaye ni MWOKOZI? Je! Imani yako si itakuwa bure
tu? Kwani watu au Mungu atajuaje kwamba unamwamini kama hakuna changamoto pande
zote? Je! Unataka kusema “umeweza kusimama kwenye wokovu kwa sababu shida zako
na changangamoto zimekwisha”? nataka
nikwambie jambo hili, BWANA hashangai changamoto zako, ila anakushangaa wewe
UKISHINDWA kusimama katika hizo changamoto na kuzishinda; kila ukijikwaa
anakuuliza “imani yako iko wapi?”.
Jifunze
jambo hili, hilo jaribu lako LITARUDIA na KUDUMU sana, hadi utakapolishinda,
ndipo utavuka hatua zingine za imani; yaani ufike mahali pa KUMTII Mungu katika
hiyo “tufani” yako, ndipo utasikia BWANA akisema juu yako, “watakatifu alioko
duniani ndio wanaonipendeza”, kwa maana wanasimama katika njia za BWANA japo
katika dhiki zao Ukisubiri Mungu aondoe changamoto zako ndipo usimame katika
wokovu, hiyo siku iko mbali nawe kwa maana ni mapenzi ya Mungu tuingiapo katika
majaribu na changamoto mbali mbali
na imetupasa kumshukuru Mungu kwa mambo yote; na kushinda kwetu kunampa BWANA
heshima na utukufu wa pekee, Anapenda kutuona tukishinda, ndio maana ameandaa
taji kwa washindi wote.
Frank
Philip.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni