“Kwa
maana huku ndiko kumpenda Mungu,
kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito. Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu
huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo
imani yetu. Mwenye
kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana
wa Mungu? [... ]
Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi;
bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda,
wala yule mwovu hamgusi”
(1 Yohana 5:3-5, 18).
Kanuni ya kuushinda ulimwengu ipo
katika mambo matatu: kuzaliwa na Mungu
(yaani kuzaliwa mara ya pili kwa kumpokea Yesu kama BWANA na Mwokozi wa maisha
yako), kumpenda Mungu (yaani kushika
amri zake), na kujilinda (yaani
kuangalia kwa BIDII kufanya sawa na Neno la Mungu pamoja na kusali na kuomba).
Kumekuwa na JITIHADA nyingi za watu
kuepuka dhambi ambazo mwisho wake ni KUSHINDWA kila siku na kujiletea majuto na
maumivu. Wapo wengi wamejitahidi kuwa WEMA kwa nguvu zao, kujiepusha na mambo
fulani kwa nguvu nyingi, na hata wamejiwekea masharti fulani ili wasitende
dhambi, mwisho wa siku wanajikuta wamefanya jambo lile lile wanalopingana nalo
akilini mwao. Ukiona hali hii
inajitokeza, tena mara kwa mara, anza kujiuliza maswali, je! Umezaliwa na
Mungu? Je! Unamtafuta Mungu kwa BIDII katika kusoma Neno & kutafakari,
kusali na kuomba? Je! Unampenda Mungu?
Kwa bahati mbaya sana, kumpenda Mungu
hakupo katika maneno, ila matendo yako. Angalia hapa “Yeye asemaye,
Nimemjua, wala hazishiki amri zake,
ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo
upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa
tumo ndani yake” (1 Yohana 2:4-5). Jiulize maswali haya: je! Unachukia
uovu? Je! Unajiepusha na uovu? Kama majibu yako ni ndio, basi kwa kifupi wewe
unampenda Mungu. Angalia mfano wa Yusufu akiwa kwa Potifa kule Misri (Mwanzo
39). Yusufu alijua kwamba angeweza kuzini na yule mama, mke wa Potifa na bwana
wake asijue, ila alisema “nimtendeje
Mungu dhambi kubwa namna hii?” Yusufu alijua shida sio kufumaniwa wala watu
kujua, shida ni kumtenda Mungu dhambi. Kwa sababu Yusufu alimpenda Mungu sana,
akashinda ile dhambi.
Sasa kuna jambo hili nataka ujifunze.
Sio kwamba kila atendaye makosa au dhambi hampendi Mungu. Kuna tofauti ya
kutenda dhambi na kuipenda dhambi.
Angalia hapa tena, “Msiipende dunia, wala mambo
yaliyomo katika dunia. Mtu
akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila
kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha
uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita,
pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”
(1 Yohana 2:15-17). Hali ya moyo wako ndiyo itakupelekea kujua kwamba unaipenda
dhambi au la, usijidanganye na maneno matupu, kagua moyo wako na jiulize “hii
kiu ya dhambi fulani inatoka wapi?”
Dalili ya mtu “anayependa dunia na
mambo yake” ni KUDUMU katika dhambi fulani na KUIFURAHIA, na
maana yake ni KUTOKUMPENDA Mungu. Ukiona unafanya dhambi, halafu haukwaziki
wala kuumia ndani yako (hali ya majuto), inaonesha UNAIPENDA hiyo dhambi; ni
vigumu kuiacha au kuiepuka, unahitaji msaada wa Mungu. Nikatazama tena jambo
hili, “…. bali
yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda,
wala yule mwovu hamgusi” (1 Yohana 5:18). Pamoja na neema, nakwambia kuna
BIDII ya kumtafuta Mungu na mambo yake, na hiyo itakuokoa na mengi. Kadri unavyomtafuta
Mungu na mambo yake unazidi kuonekana kwake. Wakati huo ukimtafuta Mungu kwa
BIDII unajikuta na utu wako wa ndani unabadilishwa taratibu. Ghafla! Unajikuta
unachukia dhambi, na unasikia kukosa amani ukifikiri tu habari ya kutenda
dhambi hata kabla ya kuitenda, ukifikia hatua hiyo jua umeanza kumpenda Mungu.
Hatua za KUJILINDA ni hatua za MAKUSUDI
kabisa na wala sio za kukaa tu, huku unatenda dhambi kwa kisingizio cha neema.
Hizi hatua ndio zinaonesha KIASI cha imani yako, kwa maana imeandikwa “imani bila matendo imekufa nafsini mwako”.
Hayo matendo ufanyayo katika harakati za kujilinda
(kuepuka uovu), kama ilivyokuwa kwa Yusufu, inaonesha kiwango chako cha kumpenda
Mungu wako na kumtii.
Inasikitisha sana kuona jinsi ambavyo
watu wanahubiri, kufundisha na kushawishi watu kwa BIDII sana juu ya sadaka,
ila ni wapole sana, au wanazungumza kwa ulegevu habari ya dhambi! Je! Kuacha
kutoa fungu la kumi na uzinzi kanisani ni kipi cha kukemea zaidi? Au kwa sababu “atendaye dhambi anawajibika
kwa Mungu yeye binafsi, ILA atoaye fungu la kumi anawajibika kwa Mungu na kwetu
pia?” na kwa maana hii, tumeweka BIDII katika sadaka kwa sababu nasi
twafaidika? Angalia jambo hili, usiache kutoa sadaka zako, ila jilinde na uovu
ili sadaka zako ziwe na maana mbele za Mungu, angalia mfano wa Korinelio
(Matendo ya Mitume 10). Sadaka zako bila kuacha uovu, bado haimaanishi
unampenda Mungu! “Tena nikitoa mali zangu
zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina
upendo, hainifaidii kitu” (1 Wakorinto 13:3).
Frank Philip.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775
AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni