Ijumaa, 9 Januari 2015

FAHAMU UNDANI WA VITA KATI YA ISRAEL NA PALESTINA KIBIBLIA. ISRAEL ALIPEWA YAKOBO NA SI YAKUB. MPENDWA ENDELEA KUIOMBEA ISRAEL part 3


Na Douglas Majwala
Zek.2:5 tunaona MUNGU akiazimia kulinda Yerusalemu aliyowapa wana wa Israel akisema yeye MUNGU atakuwa ukuta wa moto kuuzunguka maana yeye ndiyo huo utukufu [yaani yeye ndiye utukufu uliokuwa juu ya wana wa Israel]. Zek.12:3 Mataifa yanayotaka kuutwaa Yerusalemu yatapata majeraha maana umefanywa jiwe litakalowaelemea [yaani watashindwa vita na chumi zao zitaporomoka kwa vita na kwa kutoibariki Israel maana imeandikwa atakayekulaani atalaaniwa, atakayekubariki atabarikiwa Mwa.27:29, pia “Mwa.12:3 Nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”].

MUNGU anasema katika “Zek.12:9 Hata itakuwa siku hiyo ya kwamba atatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu.” Tunaona jinsi ambavyo mataifa yanayojiingiza kwenye mgogoro huu chumi zao zikiingia gharama kubwa ama kwa njia ya vita kuathiri bidhaa ya mafuta na kuteteresha chumi za dunia nzima, hii ni njia ya MUNGU kutimiza ahadi yake kuwa atatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu [ikiwemo kupingana na Agano la MUNGU juu yake], hivyo siyo lazima waangamie kwa vita, gharika wala moto wa Sodoma na Gomora bali hata kiuchumi kama nilivyofafanua. Marekani anayejuwa siri hii huwa anaingia kwenye mgogoro kwa tahadhari kubwa sana iliyokokotolewa [highly calculated risk] na uangalifu wa ziada [extra caution]. Tanzania yenyewe baada ya kuvunja uhusiano na Israel bado hadi leo ina maombolezo ya umasikini huku rasilimali zake [ngano yake na divai yake iliyozitolea jasho na ilizopewa na MUNGU] zinaliwa na nondo, kutu, madumadu, tunutu, parare, nzige, mchwa yaani mafisadi wa kitaifa na kimataifa na kubaki na laana ya rasilimali [resource curse], naamini serikali ya Tanzania na Kanisa la Tanzania kama zikifanya marejeo ya uhusiano na Israel na kutangaza hadharani kuwa iko nyuma ya Israel kwenye mgogoro huu ambao siyo wa kidini wala kisiasa [maana serikali ya Tanzania haina dini bali ina imani na imani siyo dini na inatumia imani kwenye viapo vyake] natamka kwa ujasiri kuwa dira ya taifa ya 2025 itawezekana kabla ya 2025 kufika na Tanzania kuwa uchumi wa kati Mini Tiger kwa spidi hiyo. Jiulize swali hili, kwa nini mafia wa kiuchumi wa kimataifa hawaingii Israel iliyojaa maziwa na asali? Wastani wa pato la kila mtu Israel GDP per capita ni dola za Marekani 36,151.21 [2013], ikiwa na idadi ya watu 8,296,000 ml [2014] wakati Tanzania ni dola za Marekani 502.08 [2013] kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Pato-ghafi la Israel GDP ni dola za Marekani 291.4 bl [2013], ukizidisha GDP ya Israel katika dola za Marekani na GDP ya Tanzania kwa bei ya soko la dola ya USD 1 = Tzs.1750 hutaamini kalkuleta yako [jaribu kukokotoa uone], na hapo sasa uone bajeti ambayo Israel inatumia kwa watu 8,296,000 ml tu, dhidi ya bajeti ya Tanzania kwa watu 44,928,923 ml [Sensa ya 2012]. Wastani wa maisha [life expectancy] ya Muisrael ni miaka 84.0 kwa wanawake na miaka 80.02 kwa wanaume [2014], Tanzania wastani wa jumla wa maisha ni miaka 61 [2012]. Waisrael wanaishi kwa mbali zaidi miaka ya Biblia. Kama sera ya diplomasia yetu inalenga uchumi zaidi kwa nini tuendelee kuvunja uhusiano na taifa kama Israel?

Unabii wa Zek.12:9 kuwa mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake, umetimia ambapo tunashuhudia mataifa kupitia jumuiya za kimataifa kama UN [ikiwemo Arab League] ambayo ndiyo imebeba mataifa ya dunia hii; ambayo yanakusanyika juu ya Israel kupitia UN, lakini tunaona ni kwa namna ambayo haiko sawasawa na Agano la MUNGU na wana wa Israel, maana UN inatoa haki pasipo haki na kunyima haki panapo haki, inaweka huruma mahala ambapo MUNGU mwenyewe ameishatangua huruma yake hapo na kuweka ghadhabu na kuondoa baraka kwa kizazi cha Kanaani na kizazi cha Misri ambao wote hawa walimuasi MUNGU na kugeukia miungu, UN inaweka siasa mahala ambapo MUNGU ameweka imani, inawezekana vipi jambo hili la UN? Inawezekana vipi jambo hili la mataifa ya dunia kupitia mwamvuli wa UN? Je, chini ya jua yupo mwanadamu awezaye kubishana na MUNGU? Au awezaye kutangua Agano ambalo hakuliweka wala yeye siyo sehemu ya Agano hilo, tena la Kimbingu? Mamlaka hayo anayapata wapi? Kwa MUNGU yupi? Au ni ibada ile ile ya sanamu kwamba mataifa kupitia UN hayamtambui MUNGU wa Israel kama ambavyo Wakanaani na Wamisri na vizazi vyao walivyoabudu sanamu [miungu]? Yafuatayo ni ushahidi wa maandiko jinsi ambavyo MUNGU aliwapa wana wa Israel nchi ya ahadi. Wana wa Israel pia kwa nyakati tofauti tofauti walifika kiwango cha mateso na mapito ambacho kilitindisha imani zao kwa MUNGU na wakawa kama waasi pia sawa na Wakanaani na ndugu zao, tofauti na Wakanaani na ndugu zao waliomuasi MUNGU, wana wa Israel walimrudia MUNGU wao baada ya kugundua kuwa hakuna msaada kwa miungu na kwamba salama yao iko katika kuheshimu Agano na kuambatana na MUNGU wao pekee anayeweza kuwaokoa mikononi mwa Wakanaani na ndugu zao. Wakafanya rejea jinsi ambavyo MUNGU huyu aliwaokoa utumwani Misri kwa ishara za ajabu ambazo haziwezikufanywa na miungu. Walifanya toba wakarejea kumuamini MUNGU na Agano lao MUNGU aliendelea kuliheshimu bila kulitangua.

Soma jinsi ambavyo Nehemia anavyoomboleza kwa MUNGU ili aendelee kushika Agano lake la kuwapa wana wa Israel mahali katika nchi ya Wakanaani kama alivyoahidi. Hapa pia unagundua kuwa utumishi wa Musa haukutofautiana sana na wa Nuhu katika kuwahimiza watu wao kuendelea kumuabudu MUNGU wao wa kweli japo watu hao hawakushika mashauri ya viongozi wao [Musa na Nuhu] kwa maana waliasiasi kwa vipindi tofauti tofauti lakini wana wa Isarel wakamrudia MUNGU wao lakini Mamori, na Mahiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi wakaangamia. Neh.1:6-10; 6tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi. 7Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako. 8Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa; 9bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo. 10Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari.

Sasa soma jinsi ambavyo Nehemia [Mhandisi/Mkandarasi wa ujenzi/Civil Engineer/Contractor] amepewa ruhusa na MUNGU kwenda kuujenga upya Yerusalemu iliyobomoka ambapo huko pia kulikuwa na makaburi ya baba zake. Nehemia amepata kandarasi hii kwa ajili ya wana wa Israel kujengewa Yerusalemu yao upya, tena MUNGU sasa anaweka walinzi kulinda Yerusalemu [Isa.62:6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku] Neh.2:16, 19-20 16Wala mashehe hawakujua nilikokwenda, wala nilivyotenda; wala sijawaambia Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala mashehe, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo. 19Lakini waliposikia Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Mtaasi ninyi juu ya mfalme? 20Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu. Kwa hiyo msitari huo wa mwisho unathibitisha kuwa Yerusalemu siyo yao, hata haki na kumbukumbu lao vimeondolewa.

Sasa unaona maadiko yalivyowazi ndugu msomaji!!! Ndiyo maana Israel haiwezikukubali kuiachia Yerusalemu na japo Palestina inakalia sehemu yake lakini Muisrael lazima atakuja kuikomboa tu maana kuiachia Palestina ni kuasi Agano la MUNGU aliloweka na wana wa Israel kuwa amewapa mji huo, naamini hata Marekani ambayo nayo kama Israel ilipigana vita vingi sana katika karne ya 18-19 kuikomboa ardhi yake, wanayaelewa maandiko haya bila shida na ndiyo maana kama mimi, na wao pia wanachukuwa upande wa Israel katika mgogoro huu. Sasa, mimi naamini kuwa Mwarabu na Mashehe waliotajwa hapo juu siyo waislamu, kwa maana wakati huo japokuwa hawa walikuwa katika kundi lililomuasi MUNGU wa kweli lakini uislamu haukuwepo kipindi hicho, uislamu umekuja karne ya 7 AD, baada ya YESU kumaliza kazi duniani na muanzilishi wa uislamu [ambao maana ya uislamu ni “jisalimishe kwa mungu” na uislamu nao pia ni Monotheistic] mtume Mohammed hakuwepo enzi za Manabii [siyo Nabii] bali ni mtume na amekuja baada ya YESU. Kwa mantiki hiyo basi, mashehe na mwarabu waliotajwa hapo mzizi [origin] wao ni katika kizazi cha Misri mwana wa Hamu ambaye Hamu ni mtoto kwa Nuhu, na Misri ndiko alikotoka kijakazi Hajiri mama wa Ishmail kwa Ibrahimu. Kipindi hicho hakukuwa na uislamu wala Kanisa halikuwepo kwa sababu Kanisa limeanza mwaka wa 30 baada ya YESU ila Ukristo kama imani [Ukristo siyo dini] ulikuwepo, kwa hiyo kwa maneno mengine ni kuwa mwarabu na mashehe walitokana na Ukristo [ambao siyo dini] pia maana ndiyo imani iliyokuwepo na ndiyo iliyofanya uumbaji; kabla hawajamuasi MUNGU kupitia vuguvugu la uasi uliozikumba koo za Kaanani na nduguze Misri nk. Ndiyo maana nimesisitiza kuwa mgogoro huu siyo wa kidini. Wapalestina, waislamu, Wadruze, Wakurdi, Jewish, Judaism, Wabahai, Waarmenia, Waaramean na Wakristo wasiuchukulie kuwa ni wa kidini. Dini asili yake ni dunia ila imani asili yake ni Mbingu japo inafanyakazi hadi duniani lakini dini haina nafasi Mbinguni. Narejea kwamba, bila msaada wa Roho wa MUNGU, mafundisho haya ni magumu sana kueleweka japo yamefunuliwa kwetu sawa na Kumb.29:29. Ni wazi kabisa kuwa tunaangamia kwa kukosa maarifa.

Amosi pia anathibitisha MUNGU kuwapa wana wa Israel nchi aliyowaahidia, Amo.9:14-15  14Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake. 15Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu wako.

Tazama ushahidi mwingine kuthibitishakuwa MUNGU aliwapa wana wa Israel nchi hiyo ya ahadi. Pia unagundua kwamba hata Yoshua naye aliambiwa asitangue Agano hilo, kama ambavyo Manabii wote hawakutangua akiwemo YESU Nabii wa mwisho katika safu ya Manabii wa MUNGU wa nyakati za Biblia. Soma hii:  Yos.1:1-8 1Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, 2Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli. 3Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa. 4Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu. 5Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. 6Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. 7Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. 8Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
Lakini kwa nini Israel inashutumiwa na mataifa duniani kwa operesheni za kimedani dhidi ya maadui zake? Kibali hicho cha mashambulizi Israel inapata wapi? Hii ndiyo sababu iliyofanya Tanzania ikavunja uhusiano na Israel kwa kigezo hiki cha vita ikihisi mahasimu wa Israel wanatendewa visivyo na Israel kupitia vita kati yao, naona kama Tanzania ilichukuwa uamuzi wa kupotoka kabisa kwa sababu siku zote vita vikipiganwa lazima awepo wa kuumia hata kama ni kiuchumi. Hata katika vita ya Mbinguni shetani alishindwa Ufu.12:7. Lakini ukisoma maandiko vizuri na kama wewe una Roho wa MUNGU ndani yako kukuongoza kuielewa vizuri Biblia na imani nzima ya Ukristo na muktadha wa Agano la MUNGU kwa wana wa Isarel, hutapata taabu kuelewa hatua za kijeshi za Israel kwa maadui zake ambao ni kizazi cha ukoo ulioasi tangu Nuhu ambao ni uasi wa pili huu wa mwanadamu baada ya ule wa Adamu. Israel ina kibali kamili cha kimaandiko kufanya mashambulizi, na kibali hicho kimemuonya Israel kuwa asishambulie hadi ameshambuliwa kwanza, hivyo Israel hakulupuki tu kushambulia lakini anajibu mashambuli kwa mujibu wa maandiko ambayo yako wazi wazi kabisa. Ebu soma hii: Kut.21:23-25 23Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai, 24jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, 25kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko. Huyu ni MUNGU mwenyewe anaonya na ametoa kibali kwamba adui zako wakitoza uhai nawe toza uhai, wakiteketeza na wewe teketeza, wakisababisha jeraha nawe sababisha jeraha, wakichubua nawe chubua, tena katika msitari wa 23 MUNGU ameiagiza Israel kuwa mpaka pawepo na madhara kwako kwanza uliyosababishiwa ndipo na wewe ujibu. Sasa mashutumu kwa Israel yanatoka wapi?
Hakuna mwanadamu chini ya jua angeweza kwenda kinyume na amri hii MUNGU aliyowapa wana wa Israel kutekeleza, vivyo hivyo kwa sababu Agano bado linasimama [hata YESU alilikazia litime/hakulitangua] Israel haina chaguo mbadala bali inahakikisha inatekeleza amri halali ya MUNGU wao kama ambavyo mtu mwingine awaye yote angeweza kutekeleza amri ya bwana wake yeye akiwa kama mtumwa/mtumishi wake. Soma hii uone maagizo halali ya MUNGU kwa wana wa Israel [nasema halali kwa sababu yeye MUNGU ni mtakatifu na hakosei na hatendi dhambi] kuimiliki nchi ya ahadi. Kut.23:23-33 23Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali. 24Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. 25Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. 26Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. 27Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao. 28Nami nitapeleka mavu [nyigu mkali] mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako. 29Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. 30Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi. 31Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hata bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako. 32Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. 33Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako. Kwa amri hiyo kali yenye matishio ya adhabu endapo Israel isingeyatekeleza, mwanamume gani aliyezaliwa na mwanamke angeweza kujiepusha na mkono wa MUNGU? Je, ni UN? Je, ni Arab League? Je, ni mataifa yanayopingana na Israel? Hatuoni Tanzania ilivyoathirika na kusitisha mahusiano ya kidiplomasia na Israel?

Kumb.29:12-13 12 ili uingie katika agano la Bwana, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe Bwana, Mungu wako, hivi leo; 13apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Hii ina maana ili Israel iweze kuwa taifa na ili MUNGU awezekuwa MUNGU kwake inaibidi aingie katika Agano la Bwana MUNGU wake na kiapo chake pia. Sasa kama Israel ilipewa sharti hilo kali, nani leo anaidanganya ivunje/iende kinyume na kiapo kwa ushawishi wa kisiasa tu? Je, MUNGU wakati anafanya Agano na kuilisha kiapo halali Israel, alifanya hivyo kisiasa? Je, wanasiasa wanajuwa kwamba viapo vya kisiasa vikivunjwa huwa adhabu hata ya mauti kama kunyongwa au kupigwa risasi huwa inatekelezwa? Je, wanasiasa hao hao wanataka viapo vyao vya kisiasa vilindwe na kiapo cha MUNGU kivunjwe na mvunjaji aendelee kustarehe tu?

Hapa pia tunaona MUNGU akimtumia Yoshua kutimiza dhamira yake ya kuwamilikisha wana wa Israel ile nchi ya ahadi akiwang’oa waliokuwa wakiiishi. Yos.3:9-10 9Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu. 10Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi. Pia Kumb.7:1 1Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe. Kama mataifa haya yalikuwa na nguvu kumpita Israel, je, nguvu hiyo imekwenda wapi hata leo? Ndiyo maana nilisema mwanzoni kuwa kabla ya kuasi, makabila haya yalikuwa na nguvu na yalipoasi nguvu yao ikaondolewa na kupewa wana wa Israel.

Ona sasa ghadhabu ya MUNGU inavyowaka moto dhidi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi, Kumb.7:2-5 2wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; 3binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. 4Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi. 5Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. Kuasi kuliwapa maadui za Israel kuwa najisi kabisa kwa MUNGU. Kumuasi MUNGU ni kubaya kuliko ubaya wowote uujuawo ule. Wewe unayesoma mafundisho haya kama umeasi, fanya haraka kabla jua halijazama urejee kundini. MUNGU ana wivu unaowaka moto kwa habari ya kumuasi.

Yoshua aendesha medani usiku na mchana [afunga jua na mwezi visitembee] kwa amri ya MUNGU aliyeghadhabika kutokana na yeye kuasiwa na kuabudiwa miungu ya uongo, mbinu hii imewachanganya maadui wa Israel wakifadhaika, wale waliokuwa kule Gibeoni wanaona jua halitembei na mchana umerefuka na wale waliokuwa bondeni Aiyaloni wakipigana usiku wanaona mwezi hausogei pia, yote haya yanatendeka katika sehemu/nchi moja ambayo haikuwahi kuwa na mabadiliko hayo ya majira tangu kuumbwa kwa dunia, wamejawa uchovu na hofu kuu ya kupoteza vita maana wamechoka sana, Yos.10:10-14 10Bwana naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda. 11Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga. 12Ndipo Yoshua akanena na Bwana katika siku hiyo ambayo Bwana aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. 13Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao. 14Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye Bwana kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa Bwana alipiga vita kwa ajili ya Israeli. Hii ndiyo inayotokea hata leo kuwa Israel inao uwezo wa kupambana na maadui hata kama watakuwa wamemzunguka nyuzi 360.

Amo.2:1-4 1Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Moabu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu aliichoma moto mifupa ya mfalme wa Edomu hata ikawa chokaa; 2lakini nitapeleka moto juu ya Moabu, nao utayateketeza majumba ya Keriothi; na Moabu atakufa pamoja na mshindo, na kelele, na sauti ya tarumbeta; 3nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema Bwana. 4Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata.
 
                                 -Tunaangamia kwa kukosa maarifa-
 
                                                    MWISHO
 
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: