Na Douglas Majwala
Hii nguvu ya medani ya Israel ni ya kimaandiko, haishindwi
na silaha za kivita, haishindwi na uchawi, wala haishindwi na uganga ebu soma
jinsi ambavyo Balaamu mwenyewe kwa maneno ya kinywa chake aliyopewa na MUNGU
anavyomshuhudia Balaki mwana wa Sipori kuhusu nguvu za Israel katika
Hes.23:22-23
22Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye
ana nguvu kama nguvu za nyati. 23Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo,
Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa,
Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! MUNGU aliwahidi Wana wa Israel kuwa vita si
yao, 2Nya.20:15 msiogope maana vita si yenu bali ni ya MUNGU.
Jambo ambalo dunia inapaswa kujuwa ni kuwa Wayahudi
hawakupewa Israel kwa mkataba wa kisiasa bali walipewa Israel kwa Agano la
Kimbingu. Kwa maneno mepesi ni kuwa kutafuta muafaka wa mgogoro huu katika
siasa ni kupoteza muda tu, rasilimali na kuendelea kuhatarisha amani na
utangamano kama siyo wa Israel na Palestina basi wa dunia nzima, tena mgogoro
ambao unalazimishwa uwe wa kidini wakati MUNGU hakutoa eneo hilo kwa Waisrael
kwa misingi ya kidini maana yeye MUNGU hakuwahi kuwa na dini hata sasa.
Utaratibu huu wa kuendelea kutegemea siasa kwa miongo mingi kuleta muafaka au
jawabu la mgogoro huu ni sawa na kutafuta kitu kisichoweza kupatikana asilani,
Waingereza wanasema indulging in a wild goose chase. Kwa nini dunia isigutuke
kuwa siasa imeshindwa na kuwa njia ya imani kwa maandiko ipewe nafasi nayo
itumike?.
Hakuna
nguvu ya kisiasa chini ya jua inayoweza kutangua Agano la Kimbingu, hata YESU
mwenyewe hakupewa amri/kibali cha kutangua Agano la MUNGU bali zaidi alipewa
kulikamilisha [Agano la Kale lilijengeka katika msingi wa Torati ambayo YESU
hakuitangua Mt.5:17]. Jambo wasilolijuwa watu ni hili: Wakati Wakaanani
wanamuasi MUNGU wa kweli, hawakufanya hivyo kwa misingi ya siasa, bali imani
[japo potofu] na kwa mantiki hiyo iweje leo waamini katika nguvu ya siasa katika
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro ambao hauna msingi wake kwenye siasa tangu mwanzo?
Warudi kwenye imani [ambayo waliiasi kwa mapokeo ya miungu mingine] na wakirudi
kwenye imani maandiko yako wazi kwa mfano huu ninaoutoa: kama Rais wa nchi
anavyotwaa ardhi toka kwa mmiliki wake kwa matumizi mengine yenye maslahi kwa
umma basi MUNGU naye alikuwa sahihi bila kuhoji uamuzi wake wa Kiagano la
Kimbingu kutwaa ardhi ile na kuwapa Wana wa Israel kwa maslahi mapana ya
Kimbingu, na hivyo Wapalestina wanatakiwa kurudi kwenye misingi ya imani [siyo
siasa] iliyobomolewa na mababu zao na kuwafanya kuwa wageni kwenye ardhi ile
badala ya kuwa wenyeji wake. Ni bahati mbaya kwao kuwa MUNGU ni Alfa na Omega
na utukufu wake na utendaji wake havipimiki kwenye mizania ya kisiasa
inayotumika kutatua mgogoro huu, wala yeye hana asili [Azali] wala huwezi kuona
mwanzo wake wala mwisho wake kwa maana yeye hakuwahi kuumbwa [kama Baali
waliyemuabudu alivyoumbwa] ijapokuwa yeye aliumba hata na visivyoonekana pia
ameviumba Kol.1:16, vivyo hivyo imani aliyoumba MUNGU haina mwanzo wala mwisho
kama ambavyo siasa ina mwanzo na mwisho wake na pia dini ilivyo na mwanzo na
mwisho wake na ndiyo maana MUNGU hana dini na wala hasimami kwenye dini bali
ana imani ambayo imo Mbinguni na duniani pia bali dini haikuwahi kuwepo
Mbinguni.
Hivyo
basi, Wapalestina kudai ile ardhi kisiasa na kidini [Waisrael wao wanaidai
Kiimani siyo kidini wala kisiasa; tazama hata tangu enzi za Yehoshafat Mfalme
wa nne wa ufalme wa Yuda ambaye alipigana vita kwa njia ya imani, siyo dini,
akitanguliza kwaya kama kikosi cha msitari wa mbele kabisa kwenye uwanja wa
medani/vita 2Nya.20:1-37; 2Nya.5:13-14; 2Fal.3:15-27. Lakini pia 2Nya.1-6
anaitangazia Yuda yote kufunga na kusali maana nchi inaingia vitani. MUNGU
kwenye 2Nya.20:15 amesikia maombi yao na anawatuliza wasiogope maana vita si
yao bali ni ya MUNGU mwenyewe. Tena katika 2Nya.17 anawaambia hawahitaji
kupigana vita bali wajipange, wasimame wakauone wokovu wa BWANA, tena
anawahakikishia kuwa watauona wokovu wa BWANA ulio pamoja nao. Hata Daudi
hakupigana vita na kumshinda Goliath kwa njia ya kidini wala kisiasa bali ya
kiimani] ni kuzidi kuasi kama ambavyo mababu wao waliasi na kupoteza uhalali wa
milki ya ile ardhi kwa Waisrael, “Mt.15:6, Basi asimheshimu baba yake au mama
yake. Mkalitangua Neno la MUNGU kwa ajili ya mapokeo yenu. Mk.7:13 Huku
mkalitangua Neno la MUNGU kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo
mengi yaliyo sawasawa na hayo.” “Isa.31:2 Naye ataleta uovu, wala hatayatangua
maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada
wa hao watendao maovu.” MUNGU hakuona uasi na uovu kwa Yakobo wala ukaidi kwa
Israel kama ambavyo aliuona katika nyumba ya Wakaanani “Hes.23:21 21Hakutazama
uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu
pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao.”
Ieleweke
kuwa Waisrael walimheshimu sana MUNGU huyu aliyeasiwa na Wakaanani, Sidoni,
Hethi, Myebusi, Mwamori, Mgirgashi, Mhivi, Mwarki, Msini, Mwarvadi, Msemari na Mhamathi
akiwemo Mmisri chimbuko la Mpalestina. Wana wa Israel walimhofu huyu MUNGU,
walimpenda kwa kiwango ambacho hawakutaka kumuasi. Ewe msomaji, ujuwe kuwa
Utukufu wa MUNGU wa Israel uliheshimiwa na Waisrael kwa kiwango ambacho
waliogopa hata kulitamka jina lake wakihisi watakuwa wamemtenda dhambi mbaya
kuliko, ndipo walipatana kutafuta kiwakilishi cha jina lake; kiwakilishi
ambacho kitakuwa rahisi kutamka badala ya jina lake halisi lililotukuka sana,
wakaagana kumuita Yawhe, tena wakaja kumuita majina mengine kuelezea mibaraka
waliyokuwa wakipata wakitanguliza jina Yehova likifuatiwa na: Adonai [mwenye
mamlaka], El-shadai [mtoshelevu/asiye mpungufu], Rafa [mponyaji], Jire [utupaye
tunapokuomba], Ninsi [beramu/bendera yetu], Sabaoth [Bw wa vita], Rohi [Mchungaji
wetu], Shalom [utupaye amani], Shama [uliyepo/unayepatikana], El-Gibor [mwenye
nguvu], El-Ohinu [wa pekee/huna wa kufanana naye], El-Ohimu [muumbaji wa pekee]
nk. Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha mwanadamu kumuheshimu na kumtukuza
MUNGU. Ni sawa na jinsi ambavyo wewe leo huwezi kudiriki kumuita baba yako kwa
jina lake, badala yake utamuita kwa msamiati wa baba, father, dady, papaa,
thatha nk. Na hii ndiyo maana hata makabila yametafuta majina ya kumuita badala
ya jina lake halisi e.g. Mungu, God, Omukama, Mruwa, Nyasaye, Omongo, Eli nk.
Kwa Wakaanani, Sidoni, Hethi, Myebusi, Mwamori, Mgirgashi, Mhivi, Mwarki,
Msini, Mwarvadi, Msemari na Mhamathi akiwemo Mmisri chimbuko la Mpalestina
haikuwa hivi bali waliasi na kutafuta miungu mingine tena wakawatafuta kwa
makabila, lugha na mataifa yao baada ya kutawanyika baada ya gharika. Hawa ama
waliona au walisikia habari za gharika kupitia kwa babu/baba yao Nuhu aliyepewa
kufikisha ujumbe wa MUNGU wa kutoa notisi halali ya miaka 120 ya kuleta gharika
juu ya nchi kama watu wasingetubu [wasingemrudia MUNGU wa kweli]; notisi
iliyopitishwa kwa Nuhu. Ni kipindi ambacho Baali, Dagoni na Ashtorethi
waliabudiwa na kizazi kiovu Amu.16:23. Lakini licha ya ama kushuhudia au
kusikia kwenye historia habari za gharika, bado walikuja kumuasi MUNGU wao
wakaambatana na miungu ambayo Torati ilionya juu yao wasiabudiwe.
Neno la
MUNGU lililowapa Wayahudi Israel litasimama milele yote lakini mikataba ya
kisiasa inayowekwa mbele haitasimama na imeishashindwa kusimama hata sasa.
“Mk.13:31 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu [yakiwemo yaliyowapa
Waisrael Kaanani] hayatapita kamwe.” Kama MUNGU ndiye Neno lenyewe sawa na
“Yn.1:1 naye Neno alikuwa MUNGU”, basi ina maana kuwa Neno la MUNGU lililowapa
Wayahudi Israel/Kaanani ni MUNGU mwenyewe huyo ndiye aliwapa Wayahudi Israel
[siyo UN wala siyo Arab League]. Lakini Biblia ina maajabu makubwa sana, ebu
soma hii tena “Yn.1:1 Naye Neno alikuwako kwa MUNGU.” Ina maana Neno la MUNGU
lililowapa Waisrael Kaanani liliishakuwepo [MUNGU aliishaazimia] kabla ya dunia
kuumbwa, kabla siasa kuwepo, kabla League of Nations kuwepo, kabla Mkoloni
kuwepo, kabla UN kuwepo, kabla Arab League kuwepo, kabla Nuhu na kizazi chake
kuwepo, kabla Yakobo kuwepo na pengine kabla Yakub kuwepo. Na MUNGU alivyowapa
Waisraeli ardhi hiyo aliweka wazi kabisa kwenye kumbukumbu ya maandiko tena
Matakatifu [yasiyotanguka] kuwa atawafukuza hao waliomuasi [Wakaanani, Sidoni,
Hethi, Myebusi, Mwamori, Mgirgashi, Mhivi, Mwarki, Msini, Mwarvadi, Msemari na
Mhamathi akiwemo Mmisri chimbuko la Mpalestina] katika mwaka mmoja nchi isiwe
ukiwa, na wanyama wa bara wakawasumbua Kut.23:29.
Wote wanasiasa wanaokaa mikutano kutatua suala la Israel vs Palestina
kwa mantiki na mitazamo ya kisiasa, wanajaribu kubishana na MUNGU na wanajaribu
kutangua Agano la Kimbingu badala ya kulitekeleza, kinyume na hapo watakuwa
wanafanya ibada ya sanamu ambayo wafalme wote waliofanya ibada ya sanamu, MUNGU
aliondoa ufalme wao. Kama tulivyoona awali, kwa nini Marekani katika jambo hili
huwa anaogopa sana kupingana na Neno/MUNGU je, ni kwa sababu taifa la Marekani
linamuamini MUNGU [In God they Trust?] na ndiyo maana dunia inaona kama vile
Marekani inalalia upande wa Israel? Ikumbukwe kuwa kuikana Israel ni sawa na
kuilaani na kuilaani Israel ni kujitwalia laana yako mwenyewe. Ni katika
mantiki na muktadha huu kwamba tunagundua kuwa ustawi wa Marekani umejiegemeza
kwa asilimia kubwa kwenye mafungamano yake na Israel na hivyo kuitenganisha
Marekani na Israel ni sawa na kuishusha Marekani kurudi kundi la dunia ya tatu
kimaendeleo; kwa nguvu ya kinywa cha MUNGU kilichotamka baraka na laana kwake
yeye atakayehusiana na Israel “Mwa.27:29 Mataifa na wakutumikie na makabila na
wakusujudie, uwe bwana [angalizo: hapa neno bwana halijaandikwa kwa herufi
kubwa kwa sababu bwana ya herufi kubwa ni MUNGU mwenyewe] wa ndugu zako na wana
wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe”
Kwa wale ambao hatuna muda wa kusoma Biblia, nimeamua niwawekee hapa
maneno ya Biblia kuonyesha jinsi MUNGU alivyowainua Wana wa Israel,
alivyowatetea, alivyowapa nguvu na kuweka utisho mbele yao dhidi ya maadui zao,
soma Hes.22:6-41 6Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie
watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga,
niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye
hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa. 7Wazee wa Moabu, na wazee
wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia
Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. 8Akawaambia, Kaeni hapa usiku
huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu
wakakaa na Balaamu. 9Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani
hawa ulio nao pamoja nawe? 10Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana
wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, 11Tazama,
kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu
hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. 12Mungu akamwambia
Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa. 13Balaamu
akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa
maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi. 14Wakuu
wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi. 15Basi
Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale
wa kwanza. 16Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa
Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie; 17maana
nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda;
basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa. 18Balaamu akajibu
akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha
na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu, kulipunguza au
kuliongeza. 19Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate
kujua Bwana atakaloniambia zaidi. 20Mungu akamjia Balaamu usiku,
akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno
lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. 21Balaamu akaondoka
asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. 22Hasira
ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili
kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa
pamoja naye. 23Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama
njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande
ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza
njiani. 24Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde,
katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande
huu. 25Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani,
akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. 26Malaika wa
Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya
kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. 27Yule punda
akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu
ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. 28Bwana akakifunua kinywa
cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara
tatu hizi? 29Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki;
laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. 30Yule
punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako
yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La! 31Ndipo Bwana
akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana
upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka
kifudifudi. 32Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako
mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako
imepotoka mbele zangu, 33punda akaniona, akageuka upande mbele zangu
mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe,
nikamwacha yeye hai. 34Balaamu akamwambia malaika wa Bwana,
Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga;
basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena. 35Malaika wa Bwana
akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile
nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa
Balaki. 36Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda
kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika
upande wa mwisho wa mpaka huo. 37Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi
sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi
kukufanyizia heshima nyingi? 38Balaamu akamwambia Balaki, Tazama,
nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile
Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema. 39Balaamu
akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi. 40Balaki
akachinja ng'ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa
pamoja naye. 41Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha
hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za
mwisho.
Hes.23:1-23 1Balaamu
akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe
waume saba, na kondoo waume saba. 2Balaki akafanya kama Balaamu
alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume
mmoja juu ya kila madhabahu. 3Balaamu akamwambia Balaki, Simama
karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo
lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima. 4Mungu
akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba,
nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
5Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie
Balaki; ukaseme maneno haya. 6Akarudi kwake, na tazama, amesimama
karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye. 7Akatunga
mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka
milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli. 8Nimlaanije,
yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu? 9Kutoka
kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu
wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa. 10Ni nani
awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na
nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake. 11Balaki
akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na
tazama, umewabariki kabisa kabisa. 12Naye akajibu, akasema, Je!
Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu? 13Balaki
akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza
kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao
kutoka huko. 14Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha
Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume
mmoja juu ya kila madhabahu. 15Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu
na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na Bwana kule. 16Bwana
akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki,
ukaseme hivi. 17Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka
yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, Bwana
amenena nini? 18Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki,
ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori; 19Mungu si mtu, aseme
uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena,
hatalifikiliza? 20Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki,
nami siwezi kulitangua. 21Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala
hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu
ya mfalme i katikati yao. 22Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana
nguvu kama nguvu za nyati. 23Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo,
Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni
mambo gani aliyoyatenda Mungu!
Israel
imenasa kwenye mgogoro huu kwa miaka kwa sababu wanasiasa na wanajumuiya za
kimataifa ikiwemo Kanisa pia vimeshindwa kusimama katika zamu zao za kusema
ukweli wa kimaandiko na wa Kiagano hata kama unauma na hata kama ni mchungu
[ndiyo maana hapo mwanzo nilisema kuwa najitoa muhanga na nikadiriki kusema
kuwa natangaza kuwa nina upande katika hili jambo na upande wangu ni Israel].
Taasisi zote hizo zimekosa ujasiri hata kama ule wa Balaamu ambaye licha ya
kutamani malipo ya kazi aliyopewa na Balaki ya kwenda kuwalaani Waisrael
waliokuwa wakiijia nchi ya Balaki kama nzige kutokea Misri [walienda utumwani
Misri wakiwa 70 na walirudi Kaanani wakiwa takriban laki 6 na thelathini
na…hivi] na kuleta hofu kuu; tena Balaamu akitumwa kuifanya kazi hiyo hata mara
tatu, huku akifanya jambo la msingi sana la kumuuliza MUNGU kwanza [kitu
ambacho jumuiya za kimataifa, Kanisa na wanasiasa wa leo hawafanyi] ampe maneno
ya kumuendea Balaki maana Balaamu alikwishajuwa tahadhari ya MUNGU ya madhara
ya kuilaani Israel [ya kutokuwa upande wa Israel] na MUNGU alipompa maneno na
kurudi kwa Balaki, kwa kumuonea aibu Balaki aliyemuahidi malipo mazuri
makubwa], Balaamu aliamua kutumia maarifa ya kufikisha ujumbe wa MUNGU kwa njia
ya fasihi ya mithali badala ya maneno ya moja kwa moja.
Nadhani hii ndiyo staili ambayo Marekani inatumia kwenye mgogoro huu na
mwisho wa siku inajulikana kuwa yuko upande wa Israel na hii imefanya Marekani
imebarikiwa katika uso wa dunia hii tunayoishi sasa kuliko dola yoyote ile; ikimiliki
pato la wastani wa asilimia 14 ya mapato yote ya dunia nzima ikiwa na takriban
zaidi ya dola za Marekani trilioni 30 kwa mwaka kama pato-ghafi lake lote la
ndani (GDP); wakati katika nchi zingine ili mtu aweze kupata mkate wa siku
analazimika kuuza mwili wake au kumiliki bunduki ndiyo mkono uweze kwenda
kinywani. Kama kuna taifa linafaidi matunda ya kuibariki Israel [kuwa na
mahusiano mazuri nayo mbele ya adui zake, basi ni Marekani pekee]. Sasa Kanisa
limekuwa na ujasiri wa kwenda kuhiji Israel lakini limekosa ujasiri wa kusimama
madhabahuni kuisemea Israel hata kwa mafumbo tu ya mithali kama alivyofanya
Balaamu; kutamka hadharani mbele ya umma kuwa sehemu inayogombewa ni ya Israel
[Wazayoni] kwa mujibu wa maandiko ambayo kamwe hayatanguki. Kanisa halina
upande japo linayo maandiko mikononi mwake na hii nachelea kuamini kuwa ni
sababu ya kufanya Kanisa linakosa baraka na linatembea chini ya viwango vya
Roho Mtakatifu katika kutenda kazi yake ya huduma iliyoitiwa. Kwa Kanisa la
Tanzania ninawajuwa Watumishi wawili tu ambao ndiyo wamejitoa kuhubiri na
kufundisha kwa nguvu zao zote, kwa akili zao zote na kwa uwezo wao wote kuhusu
mahusiano ya Kanisa/nchi na taifa la Israel, mmoja ni Mwalimu na mmoja ni
Askofu na huduma zao zimefanikiwa sana. Hawa hawakutanguliza uwoga wala soni
kwa habari ya kuhubiri na kufundisha juu ya Baraka ambazo MUNGU anaachilia kwa
Kanisa, taifa au mtu ikiwa atajitoa kuiombea Israel baraka.
Jumuiya za kimataifa na wanasiasa wanaoonea aibu Agano la MUNGU la
kuwapa Waisrael eneo lao wanapata kibali kutoka kwa nani? Na kutoka kwa MUNGU
yupi? MUNGU wa Israel au Baali? Tazama Balaamu anavyomshuhudia Balaki mwana wa
Sipori mfalme wa Moabu kwa ujasiri bila kutafuna maneno “Hes.23:20, 20Tazama,
nimepewa amri [siyo ombi] kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua.”
Balaamu anaogopa kutangua Agano la MUNGU licha ya ahadi ya malipo makubwa
manono toka kwa Balaki kama angewalaani Waisrael ili washindwe kuitamalaki nchi
waliyopewa na MUNGU. Madalali wa amani [Peace Brokers] ambao ni viongozi wa
jumuiya za kimatafa, wanasiasa maarufu wenye hekima katika dunia ya leo na
Makuhani wa Mahekalu ya leo wanatakiwa kuchukua nafasi ya punda wa Balaamu
mwenye sifa kuu zifuatazo: kwanza alikuwa na utayari wa kusafiri kwenda ufalme wa
Moabu kufikisha ujumbe maalum wa MUNGU, pili alikubali kufanyika chombo cha
kubeba mjumbe wa MUNGU, tatu alivumilia mateso ya bwana wake Balaamu katika
safari ile ngumu iliyojaa mashaka njiani, nne alijuwa kuwa MUNGU mtetezi wake
yu hai angetuma hata Malaika njiani kumtetea na kuhakikisha kuwa ujumbe wa
MUNGU hauchakachuliwi njiani labda na tamaa ya Balaamu ya ahadi ya malipo
manono yaliyomfanya asitesite kati ya mawazo mawili ya malipo manono au ujumbe
wa MUNGU, na kwa kuogopa Mjumbe wa Mbingu Malaika mwenye upanga mkali aliyesema
na punda kwanza kabla ya bwana wake [aliona punda ni bora kuliko kwa sababu
hawezi kuhongeka] basi ni vivyo hivyo wote wanaohusika kutatua mgogoro wa
Muisrael na Mpalestina wanatakiwa kuwa punda wa Balaamu kwa sifa hizo kuu kuhakikisha
kuwa ujumbe wa MUNGU usiochakachuliwa kisiasa na kidini unafika kwa Wamoabu
[Wapalestina wa leo] kwa njia za mahubiri na mafundisho madhabahuni na kwa njia ya mikutano ya kutafuta amani
majukwaani na kuhakikisha pia kuwa mpango wa MUNGU wa kuimilikisha Israel
unabaki palepale bila kuchakachuliwa kwa roho za uwoga wala tamaa za kisiasa na
kiuchumi za kuchochea vita vya kudumu ili soko la zana za kivita liendelee
kuwepo kwa maslahi yao huku matarishi wa amani [peace messengers] nao amana zao
za kibenki ziendelee kunona kwa malipo ya perdiem na posho [masurufu ya safari
za hapa na pale za kutafuta amani ambayo kamwe naapa hawataipata nje ya mpango
wa MUNGU ambao tayari uko kwenye maandiko kwa miaka mingi sana kabla na baada
ya YESU, yaani tangu pale Neno liliposhushwa kwa vinywa vya manabii ingawa Neno
lilikwishakuwepo hata kabla ya manabii].
Narejea tena kuwa suala la umiliki wa Kaanani ni suala la kiimani na siyo suala la kidemokrasia ya kisiasa. Utangamano wa mgogoro huu unategemea kwa 100% kuheshimu Agano la MUNGU aliloingia na wana wa Israel, yaani ni jambo la kiimani na imani ikumbukwe ni mpango wa MUNGU kumtafuta mwanadamu [akiwemo Muisrael], tofauti ya dini na imani ni kuwa dini ni mpango wa mwanadamu kumtafuta MUNGU. Kuna tafsiri au maana mbili katika falsafa hii: moja, ni dhahiri kwa ufafanuzi huo kwamba suala la Israel ni suala la kiimani na siyo la kisiasa wala dini kama nilivyosisitiza katika aya za awali. Mbili, pana tofauti kubwa sana kati ya imani na dini kama ambavyo pana tofauti kubwa sana pia kati ya Mbingu na dunia au giza na nuru. Tumeona kwamba dini ni mpango wa mwanadamu kumtafuta MUNGU na imani ni mpango wa MUNGU kumtafuta mwanadamu, hivyo basi MUNGU hakumtafuta Muisrael ili ampe Israel kwa njia ya dini bali kwa njia ya imani na moja ya sifa za msingi za imani ni kuwa lazima itafsirike katika matendo [lazima itimie katika uhalisia wake] maana isipotimia katika matendo inabaki kuwa uongo na ndiyo maana hata leo Wana wa Israel wanayakalia yale maeneo ambayo hii ni tafsiri kuwa imani iliyowapa hayo maeneo imetimia; na lazima bado watayatwaa/watayarejesha mengine yenye mgogoro iwe kwa njia ya amani au upanga, maandiko yako wazi kabisa kwa habari hii kama ambavyo tutaona katika aya zijazo mbele ya mafundisho haya.
Kwa hiyo kwa ufafanuzi huo hapo juu, tunagundua kuwa ni imani kwa njia
ya Neno la Agano ndiyo iliwapa Waisrael Israel. Hivyo basi, Mpalestina
hawezikudai sehemu ya Israel kwa njia ya dini kama ambavyo siasa haiwezi
kumpora Muisrael Israel yake na kumpa Mpalestina. Ili Mpalestina aweze kutambua
uhalali wa Muisrael kumiliki Israel, analazimika kuachana na dini na siasa na
kuingia kwenye imani ili aone kuwa MUNGU ni Alfa na Omega kwenye maamuzi yake
juu ya jambo lolote liwalo lile na juu ya ahadi yoyote iwayo ile. Hivyo basi
Mpalestina atakapogundua siri kubwa kuwa akiheshimu Agano la MUNGU na
kuambatana na Israel, basi baraka zile alizotamka MUNGU kwake yeye
atakayeibariki Israel, zitaambatana na Wapalestina pia na watawezakupaa
kimaendeleo hadi kuifikia dunia ya kwanza. Uamuzi na uchaguzi ni wao
Wapalestina. “Kut.12:3 Jamaa zote za dunia [wakiwemo Wapalestina watabarikiwa].
Hapa MUNGU hajawabaguwa Wapalestina katika baraka hizi na ndiyo maana nikasema
hapo nyuma kuwa uamuzi na uchaguzi ni wao wenyewe Wapalestina, maana MUNGU
amesema jamaa zoote za dunia.
Biblia inasema Yakobo ndiye Israel, haisemi Yakubu ndiye Israel. Kama
jina la Kiarabu la Yakubu linamaanisha Yakobo Muisrael kama ambavyo Ibrahim na
Abraham, basi wamekubali kuwa Israel alipewa Yakobo Muisrael [Mzayoni kama
wanavyoita]. Ebu tutumie mfano wa Musa kuelezea uhalali wa wana wa Israel
kupewa nchi ambayo haikuwa yao hapo awali [ya ahadi tu] lakini kupewa huko
kunawapa uhalali wa Kiagano [siyo wa kisheria ya wanadamu] maana sheria ya
wanadamu inatanguka lakini Agano la MUNGU halitanguki maana lina gharama kubwa
kulitangua na isitoshe kulitangua kunategemea kibali cha MUNGU mwenyewe. Musa
mwana wa Amram alikuwa ni Prince/Mwana-mfalme wa Misri kwa Faraoh, katika
nyumba ya mfalme ambaye hakumzaa yeye Musa [alilelewa katika kasri la Faraoh].
Na kama Yusufu pia, Musa kuwa Prince, hakukumzuia kutamalaki Misri kwa kinywa
cha MUNGU na kwa Agano la MUNGU na kabila la Waebrania waliokuwa utumwani Misri
kuwa na nguvu dhidi ya Wamisri, mfano huu unafafanua uhalali wa Wayahudi kupewa
Israel ambayo kama Waebrania kule Misri, walikuta Israel ikikaliwa na makabila
mengine ambayo yalimuasi MUNGU na kujenga na kuabudu katika madhabahu za miungu
ya uongo.
Aidha narejea kwamba mgogoro huu siyo wa kidini maana hata MUNGU hana
dini bali zaidi mgogoro ni wa kiimani. Nasema hivyo kwa sababu Palestina kuna
dini za Uislamu, Ukristo na Druze, hali kadhalika Israel kuna dini kuu ya taifa
ya Judaism, dini zingine ni Jewish, Ukristo, Uislamu, Druze na Bahai. Sheria za
Israel zinatoa uhuru wa kuabudu na serikali ina wizara maalum ya kuratibu
masuala ya kidini kama kukarabati nyumba za ibada na kuzilinda zote kwa ajili
ya watalii na watu wanaokwenda hija, lakini pia serikali ya Israel inaziruzuku
toka bajeti ya taifa dini/madhehebu yote yaliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Sasa kama mgogoro ni wa kidini je, ni dini ipi kati ya hizo ina maslahi na
mgogoro huu? Nijuavyo mimi Ukristo siyo dini bali Ukristo ni imani, dini ina
asili yake duniani lakini Ukristo kama imani asili yake ni Mbinguni na ndiyo
maana yangu kusema kuwa lile Agano la MUNGU na wana wa Israel kuhusu Kaanani
asili yake ni Mbinguni na ndiyo maana nikasema kuwa Agano lililowapa wana wa
Israel Kaanani ni Agano la Kimbingu na siyo la kidunia, siyo la kisiasa na
hivyo basi siyo la kidini. YESU Kristo alitabiriwa na Yohana ujio wake toka
Mbinguni lakini ili akubalike kwa wanadamu ilibidi azaliwe kwa sura zetu kasoro
utakatifu wake, YESU ni MUNGU kwa nafsi yake ya pili, na MUNGU anakaa Mbinguni,
neno Ukristo ambayo ni imani siyo
dini limetokana na Kristo.
Na ndiyo maana mgogoro huu unaegemezwa kwenye utaifa [ambao unajumuisha
dini na imani ya Ukristo pia
vinavyopatikana pale] maneno ya MUNGU wakati anawapa wana wa Israel ile ardhi
alimwambia Yakobo utakuwa baba wa taifa la Israel, MUNGU alitaja neno taifa hakutaja neno dini, hivyo dini
zinazopatikana mle zinafaidi tu kwa mgongo wa kuwa ndani ya taifa ambalo MUNGU
alilitoa kama ahadi na ni kwa jinsi hiyo hiyo Musa alikuwa Prince katika nyumba
ambayo hakuzaliwa kibaiolojia lakini akaja kuwa na nguvu kumzidi hata mfalme
aliyemlea na Musa akafanikisha Agano la MUNGU la kuwatoa Waebrania toka
utumwani Misri. Niliahidi mwanzoni kabisa kuwa nitafundisha mambo magumu sana
ambayo bila msaada wa Roho Mtakatifu kwa njia ya maombi ili akufunulie unaweza
usielewe chochote na unaweza ukaingia katika lawama dhidi yangu kuwa kwa nini
nina upande katika mgogoro huu kama nilivyotangaza hapo awali kuwa nina maslahi
na Israel. Nikuhakikishie kuwa hata mimi ninajishangaa namna ambavyo Roho
amenifunulia haya mafundisho magumu kwenye akili zangu, mwanzoni pia nilisema
kuwa mafundisho haya nimeyaatamia kwa maombi kwa muda mrefu sana kabla sijaanza
kushika kalamu na note book yangu, haleluya! Haleluya! Utukufu kwa MUNGU!
ukitaka kusoma part 1
http://martmalecela.blogspot.com/2015/01/fahamu-undani-wa-vita-kati-ya-israel-na.html
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775
AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni