“Ikawa
usiku uo huo malaika wa BWANA alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga
watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema,
kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka,
akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani
mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga;
wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake”
(2 Wafalme 19:35-37).
Katika somo lililotangulia tumeona
viwango viwili vya kujipima (kiwango cha Daudi mwana wa Yese na kiwango cha
Rehoboamu mwana wa Nebati) na kiwango cha tatu ambacho ni mchanganjiko wa cha
kwanza na cha pili (kiwango cha Uzia mwana wa Amazia). Rehoboamu, japo alikuwa
mtumishi wa Mungu na mpakwa mafuta, hakusimama katika njia za BWANA na uzao
wake ulipata mapatilizo kwa sababu alimchukiza BWANA kwa sanamu zake. Uzia,
mtumishi wa BWANA, alijitahidi kufuata njia nzuri za Daudi ILA hakuondoa ibada
za sanamu, akawa vuguvugu, huku akitenda kwa mfano wa Daudi na pia akiacha
ibada za sanamu ziendelee katikati yake kwa mfano wa Rehoboamu. Watu
wakaendelea kutoa sadaka kwa sanamu na BWANA akampiga Uzia kwa ukoma na
akatengwa na watu wake hata siku ya kufa kwake.
Katika kufuatilia habari za wafalme wa
Israel na Yuda, watumishi wa Mungu, nimemwona mmoja aliyempendeza BWANA kama
Daudi (2 Fal. 18:3), naam Mungu AKAMFANIKISHA katika KILA jambo alilotenda (2
Fal. 18:7). Huyu ni Hezekia mwana wa Ahazi mfalme wa Yuda (2 Fal. 18:1).
Katika kutawala kwake Hezekia, pamoja na
kumpenda Mungu na kusimama katika njia za BWANA kwa ukamilifu, na kuharibu
ibada za sanamu na kuondoa madhabahu za sanamu, bado adui zake waliinuka
kinyume naye (2 Fal. 18:13) na ilimpasa KUSIMAMA katika BWANA ili kuwashinda. Sasa
nilipotazama jambo hili, nikaona kumbe! Hata kama unamcha Mungu sana,
haimaanishi kwamba hutapata vita, ila Bwana atakupigania na kukupa mlango wa
kutokea. Jifunze kujua kupigana vita vyako vyema kwa maana yamkini katika hivyo
nani ajuaye yuko mtu mmoja zaidi ATAMJUA Mungu wako kwa kuona tu jinsi
ulivyovuka? Na watu wakijua ushindi wa vita vyako watatiwa moyo, watamtukuza
Mungu na wengine watamrudia Mungu.
Nimejifunza MBINU za vita ambazo Hezekia
mtumishi wa BWANA alitumia na zimenishangaza. Alipoinuka Senakeribu, mfalme wa
Ashuru, na kutuma majemadari wake ili kumtishia Hezekia, na kumtukana na kumpa
habari ya nguvu zake na kumtangazia kumpiga kama alivyofanya wafalme wengine,
watumishi wa Hezekia walikaa KIMYA (2 Fal. 18:36)! Majemadari wa Senakeribu
walipozidi kumtukana Hezekia pamoja na Mungu aliye hai, wajumbe wa Hezekea hawakujibu
neno hata moja ila kurarua mavazi yao. Ndipo Hezekia alipotafuta msaada kwa
BWANA, wala hakuweka majeshi yake kupigana wala hakuandaa farasi wa vita,
aliutafuta uso wa BWANA yeye na watumishi wake, huku wakivaa nguo za magunia (2
Fal. 19:1-7).
Ona jambo hili, “Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma;
kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA” (2 Fal. 19:14). Senakeribu alipotuma
waraka wa vitisho kwa Hezekia, Hezekia hakuujibu, alipiga magoti na kumwonesha
BWANA kitu kilichoandikwa. Ni kweli Senakeribu alikuwa na uwezo mkubwa, ni
kweli aliwaangamiza wafalme wengine na miungu yao, sawa, ila Hezekia aliona sio
jambo la kujibu bado kwa maana ALIJUA Mungu wake sio sanamu isiyoona wala
kusikia, akamsomesha BWANA waraka aone na kusikia mwenyewe; hakupoteza muda wa
KUBISHANA na adui yake.
Ukitizama katika bustani ya Eden, Mungu aliweka
mifumo ya maisha pale. Adamu na Hawa walipaswa kutunza bustani ili kupata
chakula chao, hawakuahidiwa kuishi kwa miujiza wala kufanyiwa kazi na malaika,
lakini nakwambia kuna wakati ambapo BWANA huingia kazini mwenyewe kupigania
watu wake kwa namna ambayo KILA mtu atajua huyu ni BWANA amepiga na si
mwandamu. Kinachosumbua, mara nyingi TUMEWAJIBU adui zetu na hatukumwacha BWANA
“atete na wanaoteta nasi”,
tumetumaini “magari ya vita na farasi
zetu” nasi tumeshindwa mbele ya adui zetu, japo vita ni vya BWANA! Kila
siku tunajua na kukiri kwamba “vita vyetu
si juu ya damu na nyama”, lakini mbona kila tukigeuka huku na kule tunaona
watu wa Mungu wanapigana kwa damu na nyama huku wakirushiana maneno na kujivuna
bure? Je! Yupo mtu alieenda kwa BWANA na kukunjua waraka, au mashutumu mbele zake
na kumwonesha ili aone mwenyewe? Je! Hatukujibu wenyewe na kuwatafutia adui
zetu maneno ya kuwasambaratisha badala ya kukaa kimya?
Mungu alimsikia Hezekia katika kuomba kwake,
Akasoma waraka wa Senakeribu uliokunjuliwa mbele Zake, akachukua hiyo tenda
mwenyewe. Safari hii hakusema “shuka
kapigane kwa maana nimemtia adui yako mikononi mwako”, BWANA aliteremka
mwenyewe na kupigana, tazama! Usiku mmoja malaika wa BWANA walipiga Waashuri, watu laki moja na themanini na
watano (185,000) wakafa! (2 Fal. 19:35-37) na kisha Senakaribu akaanguka kwa upanga
mbele za mungu wake Nisroki, wakati wakimwabudu, ili kila mtu ajue kwamba mungu wa Senekeribu haokoi.
Angalia hapa, “Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa
kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu
yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu
ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema
BWANA” (Isaya 54:16, 17). Sio kila URITHI ni mali na pesa, kuna ahadi
ambazo ni URITHI WA WATUMISHI wa Mungu, kati ya mambo mengi jua haya: 1. SILAHA za adui zako hazitafanikiwa juu
yako na; 2. Kila maneno/ULIMI utakaoinuka juu yako BWANA
atashughulika nao. Angalia hapa, “haki yao (yaani haki ya watumishi wa BWANA)
inayotoka kwangu mimi, asema BWANA”.
Kama umejifunza kwa Hezekia, ndipo utajua ni kwanini alikaa KIMYA mbele za adui
zake bila kupigana, akawa salama na haki yake akapata. Usisahau, Hezekia
alienda KWANZA katika njia ZOTE za Daudi, ndipo aliporithi na HAKI za urithi wa
watumishi wa Mungu kwa maana alimtumikia Mungu kwa moyo wake wote na hakuacha
njia za BWANA.
Angalia wewe unayevukiza uvumba kwa miungu
mingine, huku ukilitaja jina la BWANA. Ukaenda katika sanamu zako na kisha
kudai haki za watumishi wa Mungu. Je! Mungu ni mwanadamu hata umdanganye? Je!
BWANA ni sanamu ya miti na mawe hata asione njia zako za sirini?
Frank Philip.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775
AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni