Jumatano, 5 Septemba 2012

WACHUNGAJI WAMKATAA ASKOFU WAO MWANZA

WACHUNGAJI wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza mkoani hapa, wametoa tamko la kumkataa Askofu wa kanisa hilo mkoani Mwanza, Boniface Kwangu.
Askofu mkuu Mokiwa wa kanisa la Anglican Tanzania

Katika tamko hilo, wachungaji hao 24 wameorodhesha tuhuma dhidi ya askofu huyo ikiwemo ya kushindwa kuiongoza Dayosisi, kujihusisha na ushirikina pamoja na kuliendesha kanisa hilo kwa chuki na ubabe.

Katika tamko hilo lililosomwa kwa niaba yao na Mchungaji Marco Iseke ndani ya Kanisa la Anglikana jijini Mwanza wakati wa ibada juzi Jumapili, wachungaji hao wamemtaka Askofu Kwangu kujiuzulu wadhifa wake mara moja na kuikabidhi Dayosisi hiyo mikononi mwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Valentino Mokiwa.

Wachungaji hao katika tamko hilo, wamedai kuwa Askofu Kwangu ameonesha kila dalili kwamba ni mshirikina baada ya kuwataka wahudumu wa Kanisa kuondoa zulia la madhabahuni kwa madai kwamba lilikuwa na hirizi.

Inadaiwa Askofu huyo amebadili utaratibu wa Ibada za Kanisa hilo na kuingiza Ibada za Kipentekoste na kuwaweka wakfu wachungaji ambao tayari wamewekwa wakfu na kutoa cheo cha u-canon kwa wachungaji bila kufuata utaratibu.

Mbali na madai ya ushirikina na kubadilisha utaratibu wa Kanisa, wachungaji hao wamedai Askofu huyo amefanya ubadhirifu kati ya 2008 hadi 2010.

Askofu Kwangu anadaiwa ameuza magari matatu ili kugharimia safari zake za kwenda kutalii Israel na katika mahubiri ya Muhubiri mashuhuri, Christopher Mwakasege huko Morogoro. Anadaiwa pia kumwezesha mkewe kwenda kutalii Korea Kusini.

Waliendelea kudai kuwa Askofu Kwangu amekarabati nyumba anayoishi kwa Sh milioni 60 wakati gharama halisi iliyoidhinishwa ilikuwa Sh milioni 20.

Wachungaji hao katika madai yao, waliendelea kudai kuwa Askofu Kwangu amekuwa akienda benki kuchukua fedha bila idhini ya wazee wa Kanisa Kuu na amekuwa akisubiri wazee wamalize kuhesabu fedha mara tu baada ya Ibada na kuchukua fedha hizo na kuondoka nazo.

Pia walidai ameshindwa kuonesha vyeti vyake vya elimu ya Shahada ya Uzamili aliyodai kuwa amesoma. Kwa mujibu wa madai hayo, Askofu Kwangu ameharibu uhusiano wake na wachungaji kwa kuwaita wajinga, wasio na akili na kwamba hawajui kutafuta fedha.

“Askofu Kwangu ameshindwa kuiongoza Dayosisi ya Victoria Nyanza kwa kuwa amekosa sifa zinazoelezwa katika Timotheo wa kwanza, mlango wa tatu, mstari wa kwanza mpaka wa saba na kitabu cha Tito, mlango wa kwanza, mstari wa saba mpaka wa tisa,” walidai katika tamko lao.
Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia tuhuma hizo, Askofu Kwangu alidai hajaliona wala kukabidhiwa kiofisi kwa sababu yuko vijijini anakoendelea na shughuli za huduma ya dini 
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Chapisha Maoni