Alhamisi, 6 Septemba 2012

KARDINALI RUGAMBWA KUZIKWA MARA YA PILI

MASALIA ya mwili wa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa ambaye alikuwa Kardinali wa Kwanza Mwafrika, yatazikwa rasmi katika Kanisa la Jimbo Katoliki la Bukoba Oktoba 6, mwaka huu, Bukoba mkoani Kagera, ikiwa ni miaka 15 tangu alipozikwa kwa muda katika Kanisa la Kashozi.

Aidha, Oktoba 7, mwaka huu, kutafanyika sherehe za kulitabaruku Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba mjini Bukoba, baada ya ukarabati mkubwa uliochukua miaka 17 sasa.
 
Hayo yalitangazwa jana mjini Dar es Salaam na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shughuli hizo mbili muhimu.
Askofu Kilaini alisema shughuli ya kuzikwa upya kwa masalia ya Kardinali Rugambwa itakwenda sambamba na sherehe za kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa kiongozi huyo mashuhuri.
“Masalia ya mwanamtukuka wa Afrika, Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa yataondolewa kutoka Kanisa Katoliki la Kashozi na kuzikwa katika Kanisa la mjini Bukoba, Oktoba 6, mwaka huu katika maziko rasmi,” alisema Askofu Kilaini na kuongeza:
 
“Tarehe saba (Oktoba) itakuwa siku ya kulitabaruku lile kanisa (Kanisa Katoliki la Bukoba Mjini), pamoja na kuadhimisha miaka mia moja tangu kuzaliwa kwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa.”
 
Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliyekuwa Kardinali wa kwanza Mtanzania na Mwafrika, alifariki duniani Desemba 8, 1997 na kuzikwa Desemba 17, 1997 katika Kanisa Katoliki lililoko Kashozi wilayani Bukoba Vijijini kwa muda, kutokana na ukarabati uliokuwapo katika Kanisa la Jimbo Katoliki Bukoba.
 
Askofu Kilaini alisema shughuli hizo za Bukoba, zinatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 10,000 kutoka nje ya Bukoba, viongozi mbalimbali pamoja na maaskofu kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Ulaya na mabalozi mbalimbali. Viongozi wakuu nchini ni miongoni mwa waalikwa.
 
Alisema tayari kuna kamati zimeundwa kwa ajili ya kuratibu michango inayohitajika katika shughuli hiyo ambayo inakadiriwa kutumika Sh milioni 200, zikiwamo fedha za kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Laurean Rugambwa ambao uanzishwaji wake unaratibiwa na Mwenyekiti Profesa Josephat Kanywanyi.
 
Alisema mbali ya huyo, Kamati ya sherehe hiyo inaongozwa na Profesa Mark Mjahuzi na kwamba wananchi wanaombwa kuchangia kwa hali na mali kufanikisha sherehe hizo muhimu, kwa kununua vitenge, fulana na kutoa chochote kitakachoweza kufanikisha sherehe hizo.
 
Kuhusu ukarabati wa kanisa hilo, Askofu Kilaini ambaye amekuwa Askofu Msaidizi kwa miaka miwili sasa katika Jimbo la Bukoba akitokea Dar es Salaam, alisema ukarabati huo umegharimu fedha nyingi na kwamba umehusisha ubadilishaji wa sakafu na kubadilisha minara.
 
Akimzungumzia Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Askofu Kilaini alisema baadhi ya tunu zake ni kuhimiza elimu na katika hilo, amesimamia na kujenga shule mbalimbali zikiwamo za Shule ya Wasichana ya Rugambwa, Ihungo na Itunga zote za mkoani Kagera na seminari za Segerea, Visiga na nyinginezo.
 
Alisema tunu nyingine ni suala la afya na maendeleo ya watu, kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha jamii inapata maendeleo makubwa kwa wananchi.
 
Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa alizaliwa Julai 22, 1912 katika eneo la Rutabo, Kamachumu wilayani Muleba, na alikuwa Padri Desemba 12, 1947, kabla ya kuteuliwa kuwa Kardinali Machi 23, 1960.
 
Alihamishiwa Dar es Salaam mwaka 1969, alipohudumu hadi kifo chake Desemba 8, 1997. Kwa upande wake, mmoja wa waratibu wa maziko hayo ya Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, James Rugemalira aliwataka Watanzania kujitokeza kuchangia shughuli hiyo muhimu ili kumuenzi kiongozi huyo aliyelingania amani, elimu, usawa na maendeleo kwa Tanzania, Afrika na dunia.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: