Ijumaa, 7 Septemba 2012

ASKOFU KAMETA AWAASA WENYE STUDIO

HAKUNA ubishi kuwa studio nyingi hapa nchini zimekuwa zikirekodi nyimbo za wasanii kwa kuwatajia kiasi kikubwa cha fedha ambacho wengi hasa wachanga hushindwa kumudu.
Wakati mwingine hii imewafanya wasanii wachanga kushindwa kupiga hatua hivyo baadhi yao kujikatia tamaa, wakiachana na fani hiyo.

Kwa kuliona hilo, hivi karibuni Askofu wa Jimbo la Mashariki Kusini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Lawrence Kametta alizindua studio iliyopewa jina la Niko Ambaye Niko.

Kupitia uzinduzi huo, akawataka wafanyakazi wa studio hiyo kufanya kazi bila kuwa na ubaguzi wa dini.

Kametta amesihi uongozi wa studio hiyo kutoza bei za kawaida ili wengi wakiwamo wasanii wachanga waweze kuzimudu.

“Mnatakiwa kufanya kazi kwa kutoza kiwango kidogo cha fedha isije ikawa mnatoza kikubwa ili kupata faida maradufu ilihali mnamtumikia Mungu kwa kazi hizo,” anasema Kametta.
Anawataka kufanya kazi kwa viwango na kuweka gharama ndogo ili wasanii waweze kumudu gharama za kurekodi nyimbo zao.

Askofu Kametta anasema kuna wasanii wengi wanashindwa kutoa nyimbo zao kutokana na kushindwa kumudu gharama za kurekodi, hivyo ni vema wakapunguza kodi ili kila mwenye kipaji apate fursa ya kurekodi kazi yake.

Hata hivyo, anawataka wafanyakazi wa studio hiyo kuwa na maadili mazuri bila kuwawekea vizuizi na kujitolea kwa hali na mali katika kuchangia huduma za jamii.

“Mbali ya kutoa huduma za kurekodi na kuwa na nidhamu, lakini pia mnatakiwa kutomsahau Mungu. Mnatakiwa kuwa mnasali na pia muwe mabalozi wazuri wa kutoa huduma kwa jamii inayowazunguka ambayo haina uwezo,” anasema Askofu Kametta.

Katika harambee iliyofanyika akati wa uzinduzi wa studio hiyo, jumla ya sh milioni 4.1 ziliahidiwa, huku Askofu Kametta akiahidi kutoa sh milioni 1.2.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa studio hiyo, Steven Wambura, anasema ni miongoni mwa studio za kisasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa na vifaa vyote vya kisasa kutoka Marekani.
Anasema studio hiyo imefungwa kwa mfumo wa udhibiti sauti na umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa na ubora unaohitajika katika uandaaji wa muziki, vipindi maalumu na mahubiri pia.
Wambura anasema studio hiyo inajenga ufalme wa Mungu kwa kuwasaidia wengine kutimiza wito wao.

“Mimi ni mwimbaji wa nyimbo za Injili na nimehangaika katika maeneo mengi kurekodi.
“Wakati mwingine sikupata kazi kwa ubora uliokusudiwa, nilikwamishwa na kasoro mbalimbali,” anasema Wambura.

Anasema kwa sababu hiyo, baadhi ya kwaya zimekuwa zikisafiri hadi nje kurekodi kwa gharama kubwa, hivyo watajitahidi kutengeneza studio bora kama hizo za nje.

“Pamoja na kurekodi na kuandaa vipindi, studio hiyo imeandaa utaratibu maalumu wa kutoa mafunzo kwa waimbaji makini wenye wito na vipaji ili wahudumu katika mikutano ya nje na ndani,” anasema.
Katika utaratibu huo, studio itakuwa ikiratibu mialiko yao hivyo kuwa rahisi kwao kupata fursa ya kumtumikia Mungu na kukuza vipaji vyao.

Aidha, makanisa taasisi zinazoandaa mikutano, tamasha, ibada maalumu, pia wataweza kuwapata kiurahisi tena kwa uhakika.

Anasema hiyo ni kutokana na kuwepo kwa malalamiko dhidi ya waimbaji kwamba wamekuwa wakidai makubaliano ya malipo kabla ya huduma kwenye mikutano, semina na hata ibada maalumu.
Wambura anasema ipo mifano mingi ya baadhi ya watumishi ambao wamealikwa kuimba iwe waimbaji au kwaya bila kupewa hata nauli ya kurejea makwao au chakula ilhali wametoka mbali.
Anasema ndiyo maana waimbaji wamekuwa wakitaka uhakika wa maslahi yao kabla ya kujifunga na makubaliano ya kutoa huduma.

Wambura anasema kuna waimbaji wasio waaminifu, ambao wanaweza kuchukua nauli na wasihudhurie mikutano, lakini ni kutokana na ukweli kuwa shetani bado yupo na anaendelea kuwajaribu baadhi ya watu.

Akielezea matarajio yake, Wambura anasema ni kuanzisha kituo cha redio ili kurahisisha kazi ya kupeleka habari njema za Injili kwa kila kiumbe, huku akieleza kuwa mchakato wa kupata masafa tayari unaendelea.
 
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: