Jumatatu, 17 Septemba 2012

ASKOFU AWAOMBEA WASIMAMIZI NA WATAKAOFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA

 ASKOFU wa Kanisa la Anglikana, Jimbo la Ziwa Rukwa, Mathayo Kasagara ameongoza waumini wa kanisa hilo kuwaombea wasimamizi wa mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi kuepuka kufedhehesha taifa kwa kupokea rushwa na kuvujisha mtihani.

Alisema hayo wakati wa Ibada ya Jumapili ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana mjini Mpanda katika Mkoa wa Katavi zikiwa zimebakia siku mbili kabla ya kuanza kwa Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi unaotarajiwa kuanza rasmi keshokutwa.

Ibada hiyo ilikuwa sehemu ya kuhitimisha semina ya wiki nzima ya wachungaji wa kanisa hilo na wake zao iliyolenga kuwafunda kimaadili na kiroho.

Askofu Kasagara alisema ni aibu kwa taifa kwa shule kufutiwa mtihani au shule kufaulisha watoto wasiokuwa na uwezo kwa kuwa siku za usoni ipo hatari ya kuwa na viongozi wabovu wasio na uwezo.

Alisema kuvujisha mtihani ni kosa la jinai kwa sababu shule zinazofutiwa matokeo ya mtihani husababisha watoto wasio na hatia nao kujikuta na aibu hiyo.

Katika mtihani wa mwaka huu, wasimamizi watatoka katika shule za sekondari kwa lengo la kudhibiti udanganyifu kama uliotokea mwaka jana ambapo baadhi ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo, waligundulika kutojua kuandika na kusoma.

Kuhusu uchangiaji wa maoni ya uandikaji wa Katiba mpya, Askofu Kasagara aliwaomba wananchi wajitokeze kutoa maoni yao na kuwahadharisha wasisimamie itikadi ya chama chochote cha siasa au imani ya dini yoyote nchini, bali watoe yale yatakayosaidia kujenga nchi.

Alisema chama chochote cha siasa kinaweza kuingia au kutoka madarakani, lakini Katiba itabakia kuwa ile ile kwa hiyo ni lazima iwe kwa ajili ya Watanzania wote bila kujali imani za kidini, itikadi ya chama chochote cha siasa, rangi wala kabila lolote nchini.

Katika Ibada hiyo, Askofu Mkuu mstaafu wa kanisa hilo, Donald Mtetemela alitumia fursa hiyo kutoa baraka kwa watoto wote nchini wanaotarajia kufanya mtihani huo wa kuhitimu elimu ya msingi.
Aliwawekea watoto kadhaa mikono na kuwaombea wafanye mtihani wao wa kuhitimu elimu ya msingi vizuri na kuwaombea wasimamizi wawe waadilifu katika kusimamia mtihani huo.

Awali, Askofu Mtetemela alisitiza kuwa ukosefu wa viongozi wa kweli, waadilifu na wanaomcha Mungu ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa maovu mengi duniani kwa sababu wengi wapo kujinufaisha wenyewe na kuwapa kisogo wale wanaowaongoza.

Alisema wapo viongozi wachache wanaosimama kutetea haki kwa niaba ya wale wanaowaongoza lakini wengi wao wapo kwa ajili ya kujinufaisha na kusababisha maumivu na mateso katika jamii wanayoiongoza.

Misa hiyo ilihudhuriwa na Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani ambaye alisema ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuhudhuria misa tangu kusimikwa kwa Askofu Kasagara kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo la Ziwa Rukwa.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni