Jumamosi, 4 Agosti 2012

GRACE MWENDA. ATOKA AFRIKA KUSINI NA MAPENZI YA INJILI

NILITAKA kujua kwanini anaimba Injili. Majibu yake hayakuwa ya moja kwa moja kama walio wengi wanaomuamini Yesu Kristo, alikuwa na jibu lililoonesha dhahiri kwamba moto wake wa kuimba akiwa mdogo uliwashwa tena wakati akifanya kazi katika nyumba za kulea wazee Afrika Kusini.

Ni karama ya namna gani kupata nafasi ya kulea wazee, ambao wengine husahau muda mfupi tu baada ya wewe kuwapa huduma zinazostahili katika muda ule kwa mujibu wa ratiba na mahitaji yao. Kukubali kutumika katika mazingira magumu ya kusaidia wenye uhitaji kuliamsha moyo wa kuimba wa Grace Kadiva Mwenda uliokuwa umefifia baada ya kwenda ughaibuni.

Ni huku ughaibuni Afrika Kusini ambako mwanadada huyu aliyezaliwa hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam mwaka 1970 alianza kuimba nyimbo za Injili na hatimaye kuamua kurekodi. Kwa mujibu wake, amefanikiwa kurekodi nyimbo nane katika mfumo wa sauti.

Nyimbo hizo ni Damu ya Yesu, Niokoe Niokoe, Mungu Isikie Sauti yangu, Tujikumbushe, Altareni kwa bwana Yesu, Naja Bwana, Tangaza Injili ya Yesu na Mchunga wangu. Baadhi ya nyimbo zimeshasikika katika Radio Wapo na watu wamezipenda.

Zikiwa katika mahadhi ya nota na pia katika miondoko ya nyimbo za Injili, Grace anasema ni matumaini yake kwamba hisia alizopata ni nguvu kubwa ya kuendelea kumhubiri Yesu kwa kupitia nyimbo ambazo mengi ya mashairi yake yametoka katika Biblia.

“Watu wamempokea Kristo na kumkiri Yesu kwa kusikiliza nyimbo zake...kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa Nyimbo,” anasema Grace katika mahojiano yaliyofanyika ofisi za gazeti hili zilizopo barabara ya Mandela mkabala na Tazara. Kumpokea Kristo kuna maana kubwa kwa binti huyu ambaye anaona kwamba achangie kwa kutumia sauti yake mororo ambayo ilikuwa inatamba katika kwaya A ya kanisa Katoliki Msimbazi, kanisa la Bikira Maria wa Fatma kwaya ya Mtakatifu Cecilia.
Akiwa amerejea nyumbani kwa sasa, Grace anatafuta watu wa kusaidiana naye kukamilisha video tano zilizobaki kati ya nane zinazofanya albamu ili aweze kuiingiza mtaani. “Niliporejea nyumbani baada ya muda mfupi, mume wangu tuliyekuwa tukishirikiana naye katika kukamilisha albamu alifariki dunia na sasa natafuta mtu ambaye anaweza kukamilisha kazi hii ya Mungu,” anasema Grace.

Akiwa mama watoto wawili walioachwa na mume wake kipenzi, Lulu na William, Grace ana historia ndefu ya maisha kuanzia shule ya msingi aliyosomea Msimbazi Mseto, kisha akajifunza masuala ya nyumba kupitia Kituo cha Msimbazi na kujifunza ukatibu mahsusi Magogoni kati ya mwaka 1985-1996.

Baada ya kumaliza masomo yake alijiunga na Shirika la Kilimo la Tanzania linalomilikiwa na CCM , SUKITA. Alikaa katika shirika hili kwa miaka minane kabla ya kuachia nafasi yake na kujiingiza katika biashara binafsi.

“Nilikuwa na saluni, duka la nguo na viatu nilivyokuwa nikivitoa Zanzibar wakati huo,” anasema Grace na kuongeza hayo yalipobadilika aliachana nayo na kuamua kwenda Afrika Kusini.Amekaa Afrika Kusini kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2010 aliporejea nchini huku akiwa amekuja na zawadi ya nyimbo nane katika mfumo wa sauti akianza pilikapilika za kutumbukiza katika DVD.
“Kama kukiwa na mtu tayari kukamilisha hizi video, kazi nitakayofuata itakuwa kuizindua na kuwapa rasmi watu neno la bwana,” anasema Grace na kuongeza kwamba albamu yake hiyo inakwenda kwa jina la ‘Mungu Uisikie Sauti Yangu’. Katika albamu hiyo nyimbo tatu zina mahadhi ya kilokole na nyingine sita zina mahadhi ya Kikatoliki kwa kufuata mfumo wa nota.

Nyimbo hizo zinawakumbusha binadamu kuhusu dhambi kwa kuangalia shina lake duniani, haja ya kuomba msamaha na dhiki ya maisha inavyowagombanisha hata wenye ndoa na wakasambaratika. Anasema ana hamu kubwa ya kufanya kazi na watu kama Martha Mwaipaja, Bahati Bukuku, Rose Mhando na Serafina, kwani hao wamemkosha sana katika safari ya kuwahimiza wanadamu kumhimidi bwana.

KUTOKA GAZETI LA HABARI LEO

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: