Jumatatu, 6 Agosti 2012

KANISA LA WOTCH TOWER RUKWA KUTIMIZA MIAKA 100

KATIKA tukio linalotajwa kuwa ni la kihistoria, lakini ambalo halifahamiki kwa watu wengi nchini, kitongoji cha Kitika tarafa ya Kasanga, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kina hadhi ya kuwa makao makuu ya Kanisa la Watch Tower duniani.
Baba Mtakatifu’ (Papa) wa Kanisa la Watch Tower, Wilson Sikazwe (katikati) akiwa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo lililopo kitongoji cha Kitika maarufu kama ‘Vatican City’ wilayani Kalambo mkoa wa Rukwa hivi karibuni.

Kanisa hilo lililoanzishwa miaka 98 iliyopita, ndipo yalipo makazi ya kudumu ya Baba Mtakatifu au Papa wa Kanisa hilo lenye waumini zaidi ya 70,000 duniani, wengi wakitoka Tanzania, Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Uchunguzi wa gazeti hili katika makao makuu ya Kanisa hilo lililoanzishwa na Baba Mtakatifu wa Kwanza, Enock Sindani akitoka Marekani alikokuwa anaishi na kufanya kazi, umebaini kuwa kwa sasa limegawanyika, na kusababisha kuwapo Baba Watakatifu watatu, kila mmoja akiwa na waumini wake, lakini wote wakibakiza makao makuu kijijini hapo.

Baba Mtakatifu Wilson Sikazwe (73), alisema ndiye mrithi halali wa upapa, akisema tangu kuanzishwa kwa Kanisa hilo, limeshakuwa na Baba Watakatifu watano.

Aliwataja kuwa ni muasisi Sindani, Samwel Mwimanzi, John Chamboko, Edwin Simugala na sasa Sikazwe; na wote mbali ya kuwa viongozi wa juu wa kiroho wa Kanisa hilo pia wanajishughulisha na kilimo ili kujikimu kimaisha na hadi sasa hakuna Baba Mtakatifu wa Kanisa hilo anayetoka nje ya nchi hii.

Baada ya mpasuko, Baba Watakatifu waliopo na wanaotambuliwa, kila mmoja akiwa na waumini wake, lakini wote wakiwa na makao makuu ‘Vatican City’ ni Sikazwe, Jonas Simulunga (65) wanaoishi makao makuu, wakati Joseph Simgomba (50), akiwa wa Turiani, Morogoro.
Akizungumzia mgawanyiko huo Sikazwe alisema ulisababishwa na Baba Mtakatifu wa wakati huo, Chamboko, baada ya kuhukumiwa na Mahakama kifungo cha miezi sita au kulipa faini kwa kukutwa na hatia ya kuiba kuku wanne.

Alilipa faini na kumrejeshea kuku wanne mtu aliyedai kuibiwa. Alitamba kuwa kwa sasa ana waumini zaidi ya 50,000 ndani na nje ya nchi zikiwamo nchi jirani ya Zambia, Malawi na DRC.
Lakini mapapa wengine Sikazwe na Simgomba wanasisitiza kuwa ni kweli Chomboko ambaye ni marehemu, `alikwapua’ kuku hao na alistahili adhabu ya kifungo. Kutokana na tuhuma hizo, Kanisa lilimtawaza Edwin Simgala kuwa Papa mpya.

Lakini muda mfupi tangu alipoteuliwa kuwa Baba Mtakatifu, Simgala alikumbwa na tuhuma za uzinifu akitajwa kuwa na uhusiano wa siri kimapenzi na shemeji yake ambaye alikuwa mjane wa nduguye. Simgala naye kwa sasa ni marehemu.

Mapapa hao wote watatu wanadai kuwa makanisa yao hayo hayana mfadhili yeyote na kwamba yamejengwa kwa nguvu za waumini wao pia wao hawalipwi mshahara wowote.

Kwa mujibu wa Baba Watakatifu hao, Kanisa hilo ambalo lina misimamo mikali linaongozwa na Amri 10 za Mungu ambapo waumini na viongozi wake wanalazimika kuzishika kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, kinyume cha hivyo wanatengwa au kuvuliwa madaraka.

Sikukuu

Kanisa hilo lina sherehe moja kubwa kwa mwaka, nayo ni ya Mwaka Mpya. Kwa sasa, kutokana na mpasuko, kila Papa husherehekea na waumini wake katika maeneo tofauti, lakini ndani ya Kitika.
Walidai kuwa Baba Mtakatifu ni chaguo la Mungu hata akiwa hajui kusoma na kuandika, kwa kuwa Mwenyezi Mungu huwajaza hekima, busara na uwezo wa kutawala kupitia Roho Mtakatifu.
Kauli hiyo imejidhihirisha kwani uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa kati yao, mwenye kiwango cha juu ana elimu ya darasa la saba.

Siasa mwiko Hata hivyo kwa mujibu wao waumini na viongozi wao wanazuiwa kujiunga na chama chochote cha siasa au kushika nyadhifa za juu serikalini na hawajawahi kupiga kura katika uchaguzi wowote ukiwamo Uchaguzi Mkuu tangu nchi hii ijipatie Uhuru miaka 50 iliyopita.
Wakifafanua, walidai kuwa wanawafananisha wanasiasa na watu waongo kwamba kusema uongo ni dhambi kwa mujibu wa Amri za Mungu.

Aidha, waumini wa Kanisa hilo ambalo licha ya kuwapo kwa miaka 98 sasa halijasajiliwa kokote kutokana na agizo la muasisi wake, hawaruhusiwi kushiriki michezo ya aina yoyote ikiwamo soka, ngumi na mingine kwa kuwa wakati wa kucheza watu wanaumizana, wanazozana.

Hata hivyo, wote wamekiri kuwa hawako tayari waumini na viongozi wao kujitokeza kujiandikisha katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 26, kwa kuwa wao wanachodai wanataka wahesabiwe tu bila kuulizwa maswali tena yasiwe ya siri kwa kuwa hawako mahakamani.

Pia hawaruhusiwi kuoa zaidi ya mke mmoja, kunywa pombe na kuvuta sigara au aina yoyote ya dawa za kulevya, ingawa gazeti hili lilibaini kuwa viongozi hao wa Kanisa wanawagwaya wafanyabiashara wakubwa, kwa kuwa baadhi yao wameoa zaidi ya mke mmoja, lakini hawajachukuliwa hatua zozote za kinidhamu.

Walidai kuwa wanajihusisha na kujitolea katika shughuli za maendeleo zikiwamo kujenga shule, zahanati na pia wanaruhusu watoto wao kwenda shule na hata wao wenyewe wanatibiwa hospitalini, lakini ni marufuku kumsaidia mtu damu au kuongezwa damu kwa madai kuwa ni mali ya mtu. Hawana miiko katika suala la chakula.

Kwao, chakula cha aina yoyote, wanakula. Hata hivyo, wanaruhusiwa kufanya au kuhudhuria sherehe za harusi, ubatizo ambao unafanyika mtoni; pia mapapa wote waliopita wamezikwa katika kaburi moja.

Waumini wametengewa eneo la makaburi katika eneo hilo ambapo pia wasio waumini wa Kanisa hilo nao wanaruhusiwa kuzikwa.

habari kutoka gazeti la habari leo
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni