Alhamisi, 26 Julai 2012

VIONGOZI WA DINI WAONYWA SIKU YA MASHUJAA

VIONGOZI wa dini wameonya kuwa tofauti za kiitikadi zisiwe chanzo cha Watanzania kubomoa misingi ya umoja na mshikamano iliyojengeka kwa miaka mingi.


Katika kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa ambayo jana Rais Jakaya Kikwete aliongoza mamia ya Watanzania kuiadhimisha jijini Dar es Salaam, Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro lilitaka viongozi wawajibike kwa ajili ya Taifa na si kwa ajili yao.

Akitoa salamu za Kanisa katika maadhimisho yaliyofanyika Morogoro, Katibu Mkuu wa Jimbo hilo, Padri Luitfrid Makseyo alisema kumbukumbu za mashujaa zisikomee kwa watu wachache walioonesha uzalendo wao na kujitoa mhanga kupigania na kutetea Taifa, bali uzidi kukua kwa jamii zote. Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera aliyeweka ngao na mkuki kwenye mnara huo, Padri Makseyo alisema hivi sasa Taifa linashuhudia ulegevu wa aina mbalimbali katika nyanja nyingi wakati viongozi hawawajibiki kwa Taifa lao, bali kwa ajili yao wenyewe.

“Wenzetu mashujaa hawa walikuwa wazalendo wa kweli hata kuutoa uhai wao kwa ajili ya maslahi ya Taifa,” alisema na kusisitiza kwamba ni wajibu kwa viongozi na wananchi kujitoa kwa hali na mali kuwa Wazalendo ili kuifanya nchi kuwa mahali pema kuishi.

Kutokana na ukweli huo, aliwataka Watanzania watambue thamani ya mashujaa ili nao waweze kupambana na kila uovu, kuuchukia umasikini, kupiga vita rushwa na kutafuta elimu ili wananchi wote waweze kuwa mashujaa wa amani na kuishi kwa amani. Viongozi wengine waliotoa salamu zao kuwaombea mashujaa hao ni Shehe wa Mkoa wa Morogogo, mwakilishi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Ahmadiya.

Arusha Mkoani Arusha, viongozi wa madhehebu ya dini walisisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kudumu katika umoja wa kitaifa kwa maslahi ya nchi na Watanzania licha ya tofauti za kiitikadi. Walisisitiza kuwa tofauti za kiitikadi zisiwe chanzo cha Watanzania kubomoa misingi iliyojengwa kwa miaka mingi ya umoja, mshikamano na amani.

Mpiganaji wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Akundaeli Nasimay na Luteni Kanali mstaafu Ernest Maingu ambaye alipigana vita vya Kagera na Msumbiji, kwa nyakati tofauti waliishauri Serikali kuangalia maslahi ya askari hao ambao wametoa mchango mkubwa kwa Taifa.

Waliiomba Serikali ifanye uhakiki ili ijue askari wote waliostaafu Jeshi na kuangalia maslahi yao. Walitoa mfano kwamba wanalipwa Sh 50,000 kwa mwezi wakati askari wanaostaafu sasa wanalipwa zaidi ya Sh milioni moja. Dar es Salaam Amiri Jeshi Mkuu, Rais Kikwete aliwasili katika viwanja vya Mnazi Mmoja saa 3.10 asubuhi na kupokea salamu ya Rais na kupigiwa Wimbo wa Taifa na kupigiwa mizinga.

Rais Kikwete aliweka silaha za asili ambazo ni mkuki na ngao kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashujaa na kufuatiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange aliyeweka sime. Kiongozi wa mabalozi nchini, Balozi Juma Mpango wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliweka shada la maua. Meya wa Jiji la Dar es Salaam Didas Masaburi aliweka upinde na mshale na Mwenyekiti wa Wanajeshi Wastaafu -Tanzania Legion, Rashid Mgonja aliweka shoka. Viongozi wa dini walisoma sala za kuiombea amani nchi, mchakato wa Katiba na sensa. Aidha waliomba viongozi waongoze nchi kwa hekima, busara na uvumilivu.

Wakaombea pia vyombo vya usalama na vya uamuzi kutenda haki wakitaka usiwepo ubaguzi wa rangi, kabila na dini. Walioongoza sala ni Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na kufuatiwa na Mchungaji John Kamayo kwa niaba ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Padri Monsinyori Deogratius Mbiku wa Kanisa Katoliki.

Baada ya sala hizo, gwaride lililoundwa na vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza lilitoa heshima mbele ya Rais. Katibu wa Tanzania Legion Steven Lubala alisema ipo haja kwa Serikali kutunza wazee waliopigana Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kutokana na ushiriki wao kwa moyo wote.

Naye Maulid Said aliitaka Serikali kuwasaidia kuzungumza na Serikali ya Uingereza ili walipwe mafao yao yaliyotokana na kushiriki vita hivyo.

Viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Amer Kificho, Jaji Kiongozi Fakihi Jundu, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, viongozi wa Serikali na baadhi ya mabalozi wa nchi mbalimbali.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni