Jumatatu, 2 Julai 2012

PADRI AAMURU KABURI KUFUKIWA, AGOMA KUMZIKA MUFU KWA SABABU ALIACHA KUSALI

KATIKA hali isiyotarajiwa, Padri wa Kanisa Katholiki Jimbo la Sumbawanga , Evalin Kombe hivi karibuni aliamuru kufukiwa kwa kaburi lililokuwa tayari kuhifadhi mwili wa mmoja wa waumini wa kanisa hilo kwa dai kuwa muumini huyo alikuwa ameacha kusali.
Mbali ya kuacha kusali, Padri huyo pia alidai sababu nyingine ya kuzuia mwili wa marehemu usizikwe katika makaburi hayo, wakati wa uhai wake, alikuwa anaishi na mume bila kufunga ndoa kanisani.

Kitendo cha Padri huyo ambaye ni Paroko wa Kanisa la Pito lililopo kijijini kuzuia mwili wa marehemu Noelia Mwanisenga (29) asizikwe kwenye shamba hilo la wafu kulichelewesha maziko ya marehemu kwa zaidi ya saa tatu .
Akisimulia kisa hicho, mume wa marehemu Noelia, Boniface Sali (32), mkazi wa kijiji cha Tamasenga ambaye pia ni askari Mgambo alisema kuwa wakati wakijiandaa na maziko wachimba kaburi ghafla walirejea msibani Pito na kutoa taarifa kuwa Paroko ameamuru kaburi lifukiwe na kuwa marehemu wake hatazikwa katika shamba hilo la wafu.
Alisema baada ya majadiliano wafiwa walifikia uamuzi wa kuchimba kaburi jingine kijiji jirani cha Tamsenga na kumsitiri marehemu wao jioni tena bila ibada zinazohusu imani yake ya Kikatholiki aliyokufa nayo.

Sali alikiri kuwa yeye ni mlokole wa madhehebu ya Pentekoste na marehemu mkewe alikuwa muumini wa Kanisa Katholiki.
Ignas Mwanisenga ambaye alishiriki kuchimba kaburi la marehemu kijijini Pito anadai kuwa Padri Kombe alipofika makaburini alikuta wanamalizia kuchimba kaburi hilo na kuwataka kulifukia huku akiwatishia kuwa kama angekuwa na bunduki angeweza kuwaua.
“Alionekana kuwa na hasira kwani alitutishia kuwa kama angekuwa na bunduki angetuua, kwanza alifukia mwenyewe halafu alituachia sisi tutufukie kusimamia zoezi hilo mpaka tukalimaliza huku akisisitiza kuwa kama tungeshindwa angefukia yeye mwenyewe hata kama ingemchukua siku kadhaa kufanya hivyo” alisema Ignas .

Sali alisema yeye na mkewe ambaye alikuwa askari Mgambo waliishi pamoja kwa zaidi ya miaka minane na kujaliwa kupata watoto watatu na wiki mbili zilizopita aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Charles Kusula , Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Tamasenga alithibitisha kuwa marehemu Noelia alizikwa kijijini humo saa 12 jioni .
Tukio hilo ambalo limetokea wiki mbili zilizopita, si la kwanza, kwani Padri huyo alishawahi kukataa kumzika katika makaburi hayo ya Pito, Marehemu Steven Kipesha (34), hali iliyomlazimu baba mdogo wa marehemu, Oto Kipesha mkazi wa Kijiji hicho cha Pito kumzika marehemu upenuni mwa nyumba yake.
Kutokana na kitendo cha Padri Kombe kufukia kaburi, ndugu wa karibu wa marehemu huyo na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Pito na vijiji jirani wamelielezea tukio hilo kuwa ni mkosi kwa wafiwa.
Baadhi ya wazee wa jadi waliozungumza na mwandishi wa habari hii wanadai kitendo cha Padri huyo kinaashiria mkosi kijijini humo wakisema kufukia kaburi tupu kutasababisha balaa jingine la kifo katika familia hiyo iliyozuiwa kumzika marehemu wao kaburini humo na kwenda kumzika kwingineko.

“Sisi katika desturi yetu ya kimila iwapo kaburi tayari limeshachimbwa lakini baadaye maamuzi yakatolewa marehemu asizikwe humo, basi hukatwa mgomba na ‘kuzikwa‘ kaburini , ikiwa ni njia ya kuondoa mkosi kwa wafiwa, lakini si kufukia kaburi likiwa tupu,” alisema mmoja wa wazee hao wa jadi ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe gazetini.
“Kwa kawaida tunavyofahamu sisi ni kwamba kama uamuzi umeshatolewa kuwa marehemu hatazikwa katika kaburi lililokwishaandaliwa kwa ajili yake basi kamwe kaburi hilo huwa halifukiwi, huachwa hivyo hivyo likiwa wazi na tupu lakini kitendo hiki cha Padri kufukia kaburi sio tu kimetustaajabisha wengi bali pia ni machukizo kwetu,” alisema Afred Mwananzumi , baba mdogo wa marehemu.

Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho cha Pito Oto Kipesha alimweleza mwandishi wa habari hizi kijijini humo jana kuwa alifikia maamuzi ya kumzika Steven Kipesha (34) ambaye ni mtoto wa kaka yake upenuni mwa nyumba yao kijijini humo baada ya Padri Kombe kuwazuia wasimzike marehemu huyo katika shamba la wafu kijijini humo kwa madai kuwa aliacha kusali muda mrefu.
“Marehemu alihamia Tunduma miezi mitatu iliyopita na baadaye aliugua na kufariki dunia katika Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya tulipopata taarifa za msiba tulijiandaa na kuusafirisha mwili hadi kijijini hapa lakini Paroko Kombe alituzuia tusimzike katika shamba la wafu kijijini hapa kwa kuwa eti alikuwa hasali …… mie nikachukua uamuzi wa kumzika upenuni mwa nyumba yangu.
Alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na visa hivyo viwili akiwa ofisini kwake jana katika Parokia ya Kanisa Katholiki kijijini Pito , Padri Kombe alikiri kuwa aliwaamuru vijana aliowakuta wakichimba kaburi katika shamba la wafu kijijini humo walifukie hata hivyo alikanusha kuwatolea maneno ya vitisho kuwa kama angekuwa na bunduki basi angewaua.
Akieleza sababu za kuchukua uamuzi wake huo , Padri Kombe alisema kuwa visa vya aina hiyo vimekuwa vikitokea sio kijijini humo pekee bali na kwingineko kwamba kidesturi zipo aina tatu za maziko katika Kanisa Katholiki ambapo marehemu wote wawili Kipesha na Noelia waliangukia katika aina ya tatu .
Alisema aina hiyo ya tatu inatokea pale muumini pamoja na kwamba amebatizwa, lakini hasali hivyo anajirudisha katika upagani basi azikwe mahali popote pale lakini sio katika shamba la wafu la Kanisa.

“Mara nyingi nimekuwa nikiwaeleza haya tena huwa nawafafanulia kuwa kwa kuwa hawataki kuja kanisani kusali basi wakifa wazikwe huko huko majumbani mwao kwa kuwa ni mahali wanapopapenda zaidi kwanini wasumbuliwe kupelekwa mahala pengine kwa maziko? “ Alihoji.
Pia aliendelea kufafanua akisema aina ya kwanza ya maziko inayofuatwa na Kanisa hilo Katholiki inahusu waumini waliobatizwa ambao katika uhai wao waliweza kutimiza na kuishi katika Ukatholiki wakisali na kushiriki mambo yote ya kanisa.
Padri Kombe alisema maamuzi hayo ya kutowazika katika shamba la wafu ni fundisho kwa wengine ili wafuate ibada kama watapenda kushughulikiwa kiimani baada ya kifo.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni