Jumatatu, 2 Julai 2012

ASKOFU NGALALEKUMTWA KUIONGOZA TEC

MKUTANO wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) umemchagua Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcisio Ngalalekumtwa kuwa Rais mpya wa baraza hilo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Rais mstaafu wa TEC, Askofu Mkuu, Yuda Thadeus Ruwa‘ichi, alisema kwamba pia aliyewahi kuwa Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi, amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
Askofu Ruwa‘ichi aliongeza kuwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Padri Anthony Makunde, amechaguliwa kuendelea tena na wadhifa wake huo huku Naibu Katibu Mkuu akichaguliwa Padri Raymond Saba kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma.
Alisema kuwa waliochaguliwa kuongoza idara ni Askofu wa Jimbo la Zanzibar Augustino Shao atakayekuwa Idara ya Fedha, Idara ya Afya itaongozwa na yeye mwenyewe wakati Idara ya Kichungaji itakuwa chini ya Askofu wa Jimbo Dodoma, Gervas Nyaisonga.
“Idara ya Karitas itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo la Mbulu, Beatus Kinyaiya, Idara ya Utume wa Walei itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo Singida, Deusderius Rwoma na Idara ya Elimu itakuwa chini ya Askofu wa Jimbo la Mbinga, John Ndimbo,” alisema Ruwa‘ichi.

Alizitaja Idara nyingine kuwa ni ya Katekesi itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo la Mpanda, Pastory Kikoti, Idara ya Liturjia itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Ifakara, Salutaris Libena, huku Askofu wa Jimbo la Kondoa, Bernadine Mfumbusa akiwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano.
Kuhusu wakuu wa tume mbalimbali za baraza hilo, Askofu Ruwa‘ichi alisema kuwa Rasilimali watu itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Kahama, Ludovick Minde, Ekumeni itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Lindi, Bruno Ngonyani.
Askofu wa Jimbo la Njombe, Castory Msemwa, ataongoza Tume ya mazungumzo ya dini, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paul Ruzoka ataongoza Tume ya haki, amani, majeshi na magereza na Askofu wa Jimbo la Moshi, Isaac Amani akiongoza Tume ya wahamajihamaji.

Tume ya Sheria za Kanisa itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Same, Rogath Kimaryo, Askofu wa Jimbo la Kayanga, Almachius Rweyongeza ataongoza Tume ya Teolojia wakati Askofu wa Jimbo la Geita, Damian Dalu, ataongoza Tume ya Uinjilishaji.
Askofu Ruwa‘ichi aliongeza kuwa Tume ya watawa itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Bunda, Renatus Nkwande, Tume ya familia itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude na Tume ya utamaduni itaongozwa na Askofu wa Jimbo la Mahenge, Agapit Ndorobo

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni