Jumamosi, 30 Juni 2012

SERIKALI YAKUBALIANA NA WAISLAMU KUANZISHWA KWA MAHAKAMA YA KADHI

SERIKALI imekubaliana na Waislamu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi itakayokuwa nje ya Mfumo wa Serikali na itagharimiwa na kuendeshwa na waumini wa dini hiyo wenyewe.

Kwa kuanzia mahakama hizo zitakuwepo katika maeneo machache kwa lengo la kuufanya umma kuielewa vizuri tofauti na hisia potofu zilizokuwepo kuwa zitahusisha makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa msimamo huo wa Serikali uliokubaliana na Waislamu jana wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa kuipitisha bajeti ya ofisi yake.
“Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Kamati Kuu inayojumuisha Viongozi wa Waumini wa Dini ya Kiislamu na Serikali chini ya Uenyekiti wangu, kimsingi imekubaliana kwa kauli moja Uanzishwaji wa Mahakama hiyo Nchini itakayokuwa nje ya Mfumo wa Serikali. “Mahakama hiyo itagharamiwa na kuendeshwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wenyewe.
Serikali kwa upande wake hususan katika hatua hizi za awali za kuanzishwa kwa Mahakama hii itaendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa azma hii inafanikiwa,” alisema Pinda.
Pinda alikuwa akijibu hoja za wabunge waliotaka kufahamu maendeleo ya Mahakama hiyo huku wakitaka Serikali itimize ahadi yake hiyo ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Hamad Rashid Mohammed (Wawi); Rashid Ali Abdallah (Tumbe); Ahmed Juma Ngwali (Ziwani) na Hussein Nassor Amar ( Nyang’hwale).
Pinda alisema; “Katika kikao cha mwisho cha pamoja kati ya Serikali na ujumbe wa Wawakilishi wa Waumini wa Kiislamu kilichofanyika Machi mwaka huu, tumekubaliana katika kuwezesha suala hilo liende kwa haraka, kwa kuanzia, ni vyema zikaanzishwa Mahakama za Kadhi katika baadhi ya maeneo machache nchini.
Lengo ni kuwezesha umma kulielewa vizuri suala hili kinyume na hisia potofu zilizopo sasa zikihusisha Mahakama ya Kadhi na Sharia (inayohusisha masuala ya jinai) chini ya Dini ya Kiislamu”.

Pinda alitaja masuala yatakayoshughulikiwa katika Mahakama hiyo kuwa ni pamoja na Ndoa na Talaka, Mirathi, Wosia, Hiba/Zawadi/ Tunu, Wakfu; Malezi ya Watoto na Usuluhishi wa Migogoro ya Kiislamu.
Mahakama hiyo haitahusika na Mashauri ya Jinai. Alisema katika kikao cha mwisho cha Kamati Kuu inayosimamia suala hilo iliamuliwa na pande zote kuwa baadhi ya wajumbe kutoka upande Waislamu na Serikali wakafanye ziara ya mafunzo katika nchi za India, Uingereza, Kenya na baadaye Zanzibar ili wakajifunze namna ya kuratibu na kuendesha Mahakama za Kadhi katika nchi hizo ambazo zina Mahakama za Kadhi kwa muda mrefu.

“Lengo ni kupata uzoefu na kujua njia bora ya kutuwezesha kuanzisha Mahakama hiyo nchini. Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni na kugharimiwa na Serikali,” alisema.
Akizungumzia chenji ya Rada, alisisitiza kuwa itatumika kama ilivyokusudiwa kwani Tanzania na Uingereza zilikubaliana asilimia 75 ya fedha hizo kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada, viongozi vya walimu, mihtasari na miongozo ya mihtasari na asilimia 25 ya fedha hizo kununulia madawati.
Kwa sasa kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi 10, lakini baada ya kununuliwa kwa vitabu hivyo wanafunzi kati ya wawili na watatu wa shule za msingi watatumia kitabu kimoja. Alisema fedha hizo za madawati Sh bilioni 18.1 zitaweza kununua madawati 400,000 kwa ajili ya wanafunzi milioni 1.2.
Kwa sasa wanafunzi wenye uhaba wa madawati ni 8,000,000. Alisema ununuzi wa rada ulifanywa na Wizara ya Miundombinu ambayo sio Muungano hivyo Zanzibar haitapata mgawo huo.
Akizungumzia juu ya uvunjwaji wa Jiji la Dar es Salaam lililoanzishwa mwaka 1999, Pinda alisema mapendekezo ya kulivunja jiji hilo na kubakishwa manispaa zake tatu ili ziratibiwe na sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam yalitolewa Novemba mwaka 2010, lakini baada ya kuonekana lina kasoro tangazo hilo lilibatilishwa Februari mwaka huu.

Kuhusu zaidi ya Sh bilioni 300 zilizowekwa na Watanzania sita katika benki ya Uswisi zilizotokana na gesi ya nchini, alisema; “Serikali kupitia vyombo vyake vya Takukuru, Financial Intelligency Unit (FIU) wameanza kufanya uchunguzi wa taarifa hizo kwa kuzingatia taratibu za kisheria. Uchunguzi huo utakapokamilika matokeo yake yatatangazwa,” alisema.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni