Jumanne, 31 Julai 2012

HAYA MLIOKUNYWA KIKOMBE CHA BABU, SERIKALI YASEMA HAIKUWA NA NGUVU YA KUPONYA

MATOKEO ya awali ya utafiti wa dawa iliyotolewa na Mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwaisapile, yameonesha kuwa dawa hiyo haikuwa na nguvu za kuponya magonjwa iliyodaiwa kutibu.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi, alitangaza matokeo hayo jana bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Katika bajeti hiyo, Serikali imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 581.6 na kati ya hizo, Sh bilioni 298.2 za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 283.4 za maendeleo.

Dk Mwinyi alisema matokeo ya awali ya utafiti huo yanaonesha wagonjwa waliopata dawa hiyo hawakupata ahueni yoyote katika CD4, uzito na ubora wa afya yao. Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, utafiti huo ulioanza Machi 2012, unahusisha wagonjwa 200 wanaofuatiliwa kwa kupimwa vipimo mbalimbali.

Vipimo hivyo ni damu, CD4, uzito wa wagonjwa na ubora wa afya wa wagonjwa hao wa Ukimwi na kisukari wanaoendelea kuhudhuria kliniki katika hospitali mbalimbali za rufaa nchini ili kuona mabadiliko yoyote.

“Taarifa zao za awali zilizopo katika kliniki kuanzia walipokunywa dawa hadi utafiti ulipoanza zilifuatiliwa na kujumuishwa katika taarifa za utafiti,” alisema Dk Mwinyi.
Kuhusu uboreshaji wa sekta ya afya, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa vifaa na dawa katika vituo vya afya na ustawi wa jamii kwa kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo ya kutolea huduma.

Katika kuboresha utoaji huduma, Dk Mwinyi alisema katika mwaka unaoisha wa fedha, Wizara ilipata kibali cha kuajiri watumishi 260 wa kada ya afya kwa ajili vituo mbalimbali.
Pia katika kuboresha maslahi ya watumishi hao ambayo hivi karibuni yalikuwa hoja maalumu katika mgomo wa madaktari, Dk Mwinyi alisema watumishi 282 walirekebishiwa mishahara.

Ili kuongeza idadi ya watumishi katika sekta hiyo, Serikali iliongeza idadi ya wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo vya afya iliongezeka kutoka 4,296 mwaka 2008 mpaka 7,458 mwaka 2011.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, hilo ni ongezeko la wanafunzi 3,162 sawa na asilimia 57.6 na lengo ni kudahili wastani wa wanafunzi 10,000 kwa mwaka ifikapo 2017.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni