Jumatatu, 2 Julai 2012

KKKT SINGIDA WAPATA ASKOFU MPYA

MKUTANO Mkuu wa Sinodi ya 12 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati Mkoa wa Singida, umemchagua Mchungaji Dk. Alex Mkumbo kuwa askofu mpya wa Dayosisi hiyo.
Dk. Mkumbo anakuwa ni askofu wa nne kuiongoza dayosisi hiyo tangu kuanzishwa kwake katikati ya miaka ya themanini.
Katika mkutano huo wa uchaguzi ambao ulifanyika mjini hapa, mchuano wake ulikuwa ni mkali hali iliyolazimisha upigaji kura kurudiwa mara tatu ili kumpata mshindi kati ya Dk. Mkumbo na aliyekuwa akitetea kiti hicho, Mchungaji Eliufoo Sima.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Askofu wa Dayosisi ya Meru, Paul Akyoo na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki mwa Ziwa Victoria, Andrew Gulle ambapo wajumbe wa mkutano huo walikuwa 241.
Askofu mteule, Dk. Mkumbo mara kwanza alipata kuwa 135 kisha mara ya pili 137 na mara ya tatu alipata kura 136 dhidi ya kura 105 za mshindani wake, Sima, ambaye naye alipata kura 106 na 105 kwa mara ya pili.
Hata hivyo katika uchaguzi wa nafasi ya askofu msaidizi iligombewa na watu wawili, akiwamo Mchungaji Cyprian Hilinti na aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Mchungaji Yohana Mjungu.

Kwa mujibu wa matokea, Mchungaji Hilinti alinyakua nafasi hiyo baada ya kupata kura 164 dhidi ya kura 77 za mpinzani wake.
Aidha, aliyekuwa mwandishi wa kumbukumbu za vikao katika awamu iliyopita, Victor Bilahama, alishinda kwa kupata kura 165 dhidi ya kura 76 za Joramu Njiku.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Katibu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Brigton Kilewa, aliwataka wajumbe wote wa mkutano huo, kuhakikisha wanaungana na kuwa kitu kimoja. KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni