Ijumaa, 20 Julai 2012

FOMU ZA VITAMBULISHO VYA TAIFA ZINAENDELEA KUTOLEWA DAR HAKIKISHA UNAJIANDAIKISHA KABLA MUDA HAUJAISHA

MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema imeanza kutoa fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya NIDA  ya wiki hii, zoezi hilo lilianza rasmi  Jumatatu na litachukua siku 15.

“Baada ya hatua hii taarifa za mwombaji zitaingizwa katika mfumo wa kompyuta yaani kuanza kutengeneza daftari la kumbukumbu sambamba na uhakiki wa taarifa kabla ya NIDA kurudi kwa mwombaji kuchukua alama za vidole, picha na saini,” inasema taarifa hiyo ya NIDA.
Ikimkariri Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maimu taarifa hiyo ilisema  zoezi hilo limeanza na Mkoa wa Dar es Salaam na taratibu litasambaa nchi nzima ili wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na zaidi, waweze kusajiliwa na hatimaye kupewa Vitambulisho vya Taifa.

Kwa mujibu wa Maimu, Vitambulisho hivyo vitakuwa na faida nyingi kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kwani kitakuwa na wigo mpana wa matumizi katika nyanja zote; kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, na kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na vielelezo vya msingi vitakavyo mtambulisha, kama vile cheti cha kuzaliwa, kadi ya kupigia kura, vyeti vya elimu ya msingi, sekondari au chuo, au pasi ya kusafiria.

Kwa sasa zoezi la usajili linafanyika katika kila mtaa, ambapo vituo vitakuwa wazi kuanzia asubuhi mpaka jioni, na kuratibiwa kwa pamoja na NIDA na uongozi wa serikali ya mtaa mpaka ngazi ya kata.Usajili na utambuzi wa watu kwa Dar es Salaam unahusisha wakazi wote wakiwemo raia, wageni na wakimbizi.

Mpaka sasa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kufuatia zoezi la usajili wa makazi lililoanza Juni 22, mwaka huu, ambapo wasajili wasaidizi walipita nyumba kwa nyumba kuandikisha taarifa za watu wanaoishi katika kila kaya na kuweka taarifa katika daftari la wakazi.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: