Jumamosi, 21 Julai 2012

WACHUNGAJI WALIOKUWA WANAMILIKI DECI WATAJITETEA KWA KIAPO

WACHUNGAJI wanne wa madhehebu ya Kanisa la Pentekoste ambao pia ni Wakurugenzi wa Taasisi ya Kuendesha na Kusimamia Mchezo wa Upatu (Deci) wamesema watajitetea kwa njia ya kiapo.
Wiki iliyopita, washtakiwa hao walipatikana na kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma zinazowakabili za kuendesha na kusimamia mchezo wa upatu kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ilitajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washtakiwa hao walisema watajitetea wenyewe kwa njia ya kiapo na kwamba hawatakuwa na mashahidi wala vielelezo vyovyote.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Mkazi Stewart Sanga aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20 mwaka huu itakapotajwa tena na kuamuru washtakiwa wapewe mwenendo wa kesi hiyo.

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Dominic Kigendi, Jackson Mtaresi, Timotheo ole Loiting’inye, na Samwel Mtares.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuendesha na kusimamia mchezo wa kuchangisha fedha kwa ahadi ya malipo maradufu maarufu kama ‘Panda Mbegu’.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2007 na Machi mwaka 2009 kwenye makao makuu ya Deci yaliyo eneo la Mabibo Mwisho wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Washtakiwa hao wanadaiwa kusimamia mradi wa upatu kwa kuchukua fedha kwa wananchi kwa ahadi ya kuwapa matumaini ya fedha zaidi kuliko mapato ya mradi waliokuwa wakiuendesha.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni