Ijumaa, 22 Juni 2012

PINDA, IPO HAJA YA KUUDWA TUME HURU KUCHUNGUZA VURUGU ZA ZANZIBAR

Nakumbuka Rais Jakaya Kikwete alipata kueleza hadharani kwamba, kuna wakati aliwahi kumfukuza kazi mtu mmoja, lakini baadaye akaja kujutia uamuzi wake huo.
Alijuta baada ya kubaini baadaye kuwa alipelekewa taarifa zisizo sahihi na kushauriwa vibaya kuhusiana na mtu huyo.

Ninalojifunza hapo kwa Rais Kikwete ni kuwa kupeleleza au kuchunguza kwanza habari au taarifa unayoletewa kabla ya kuchukua hatua au kuadhibu, ni jambo la wajibu.
Wajibu huo unakuwapo kutokana na ukweli kwamba, kupeleleza au kuchunguza, kunaweza kumsaidia mtu kuepuka kujuta baada ya kuwa amehukumu na kuadhibu kwa kutekeleza habari au taarifa, ambayo baadaye inaweza kuja kubainika kuwa ilikuwa ni uongo au uzushi.
Kauli za kusigana zilizojitokeza baada ya matukio yaliyotokea katika vurugu zilizotokea kisiwani Unguja, Zanzibar hivi karibuni, zinaibua utata mkubwa juu ya ukweli wa nani hasa aliyehusika na matukio hayo.

Matukio hayo ni yale ya kuchoma moto makanisa, nyumba ya Mufti wa Zanzibar, gari la polisi na kuteketeza baa kisiwani humo.
Tuhuma hizo zilitolewa kwa upande mmoja na baadhi ya viongozi wa dini; akiwamo Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), mkoani Arusha, Thomas Laizer.
Wengine ni Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi na baadhi ya vyombo vya habari.

Kwamba, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), maarufu kama "Uamsho" ndiyo inayohusika moja kwa moja na matukio hayo.
Uamsho wanahusishwa kwa kuwa matukio hayo yalitokea saa chache baada ya maelfu ya Wazanzibari kufanya mkutano wa hadhara na maandamano makubwa kushinikiza kuachiwa kwa kiongozi wao, Sheikh Mussa Abdallah Juma, aliyekamatwa na polisi.
Maandamano hayo pia yalilenga kuishinikiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuitisha kura ya maoni juu ya Muungano na kupeleka ujumbe kwa Umoja wa Mataifa (UN) kutaka Zanzibar ijitenge kama muundo wa Muungano hautarekebishwa.

Hata hivyo, siku moja baada ya matukio hayo, ambayo yalifanyika kwa siku mbili mfululizo, Uamsho nao walijitokeza hadharani na kukanusha vikali kuhusika nayo.
Katika taarifa yao iliyotolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari, Uamsho walisema hawahusiki kabisa na vitendo vyote vya uvunjaji wa amani vilivyotokea Mei 26, mwaka huu, kisiwani humo na wanaheshimu nyumba zote za ibada, yakiwamo makanisa na mahekalu.
Tukitafakari msigano huo, pengine nami hapa niungane na wote waliojitokeza hadharani kulaani matukio hayo.

Kwamba, kila mpenda amani na anayeshimu uhuru na haki ya mtu kuamini dini anayoitaka na kumuabudu Mungu anayemuamini, kamwe hawezi kuyakubali wala kuyavumilia.
Pamoja na hivyo, swali bado linabaki palepale. Nani hasa anahusika na matukio hayo?
Mimi bado nimegubikwa na utata. Hasa baada ya Uamsho nao kujitokeza hadharani na kukanusha kuhusika na matukio hayo baada ya kunyooshewa kidole.
Utata huo unakolezwa zaidi na kauli iliyotolewa na Mbunge (BLW), Rajab Mbarouk Mohammed, aliyoitoa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, bungeni, mjini Dodoma, Alhamisi wiki hii.

Mohammed alivishutumu vyombo vya habari kwa madai ya kuandika upande mmoja wa vurugu zilizotokea kisiwani humo, akidai havikuripoti uchomaji wa misikiti na mali za watu, badala yake vilitangaza kuhusu uchomaji wa makanisa pekee
Kutokana na hali hiyo, aliishauri SMZ kuunda tume huru ya uchunguzi ili wahusika wa vurugu hizo wachukuliwe hatua na kudhibiti hali hiyo isitokee tena.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akijibu swali hilo, alisema rai ya kuunda tume huru ya uchunguzi ni nzuri na kuahidi kuwasiliana na SMZ kuona hatua walizofikia kumaliza tatizo hilo na kama kuna haja ya kuunda tume.

Pengine niungane na Pinda hapa kwamba, rai ya mbunge huyo ya kutaka iundwe tume huru kuchunguza vurugu hizo ni nzuri.
Uzuri wa rai hiyo unatokana na kanuni niliyoigusia hapo juu. Ya kupeleleza au kuchunguza kwanza ukweli wa habari au taarifa unayoletewa kabla ya kuhukumu au kuadhibu.
Ni kwa kufanya hivyo, tunaweza kuepuka majuto kama yale yaliyomsibu Rais wetu mpendwa, Kikwete. Haitoshi tu mtu kuibuka na kusema fulani ni mwizi au gaidi, kIsha wengine tukadaka na kuimba wimbo huo.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni