Ijumaa, 22 Juni 2012

WAZIRI MEMBE AONYESHA MSIMAMO KUHUSU NDOA ZA JINSIA MOJA

 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewataka marafiki na mashabiki wa nchi zinazoshabikia ndoa za jinsia moja waache kuitania Tanzania.
Membe alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, (CUF) Khatib Said Haji, aliyeitaka serikali kuzieleza nchi hizo kuwa ni kheri kuondoa misaada yao kuliko ndoa za jinsia moja.

Akijibu swali hilo, Membe alisema suala hilo ni la kisiasa pia na ni vyema marafiki na mashabiki wanaozungumza na mataifa hayo kuwaaambia kuwa waache kuwatania Watanzania.
Katika swali la msingi mbunge huyo, alisema kumekuwa na msimamo mkali wa kimkakati wa nchi za Magharibi wa kuzitaka nchi rafiki ya zile zinazopokea misaada kutoka kwao kuhalalisha ndoa hizo.

Alihoji Tanzania ikiwa ni moja kati ya nchi hizo zinazopata misaada mbalimbali kutoka kwa mataifa hayo imejianda vipi kukabiliana na janga hilo hasa pale nchi hizo wahisaani zitakapokatisha misaada kwa Tanzania.
Akijibu swali hilo, Membe, alisema itakapotokea wahisani wakasitisha misaada kwa sababu ya msimamo wa Watanzania, nchi iko tayari kujifunga mikanda na kujibeba wenyewe badala ya kukubali kudhalilisha utu na utamaduni.

Alisema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kipengele cha 9(a) tafsiri ya ndoa imeelezwa kuwa ni “Muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke wenye lengo la kudumu katika maisha ya wawili hawa”.
Alisema kulingana na sheria hiyo, suala la msingi ni kulingana na matakwa ya sheria ya Tanzania ili kuwepo na ndoa inayotambulika kisheria na ni lazima kuwepo pande mbili za jinsia tofauti yaani mwanamume na mwanamke.

“Nchi marafiki duniani zikiwemo za magharibi, zimeendelea kutuheshimu kutokana na msimamo wetu huo thabiti na usioteteleka kwa kuendelea kutoa misaada ya ushirikiano wa kiuchumi kwa serikali ya Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa Tanzania itaendelea kupokea misaada ambayo haina masharti ya kubadili sera, utamaduni wa sheria za nchi.

Hakuna maoni: