Ijumaa, 22 Juni 2012

CHRISTINA SHUSHO: MUIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI NA MBUNIFU WA MAVAZI





























































































































































“UNIKUMBUKE babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke, usinipite Yesu unapowazuru wengine naomba usinipite.”

Haya ni baadhi ya maneno yaliyomo katika moja ya nyimbo zilizomtambulisha vema mwimbaji galacha wa nyimbo za Injili nchini, Christina Shusho.
Mwimbaji huyo ambaye anaaza kwa kusema kuwa amefanikiwa kujijengea sifa kwa mashabiki wa nyimbo za Injili ndani na nje ya mipaka ya nchi kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe mzito kwa jamii, lakini ukiwa katika msingi wa neno la Mungu.

Umahiri wake katika kuimba nyimbo hizo za Injili umemuwezesha kutambulika vema na kujinyakulia tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambapo yeye ni kati ya wasanii waliopata tuzo za muziki za Afrika Mashariki na Kati (EMAS).

Mwimbaji huyo alishaibuka na tuzo ya msanii bora wa kike wa nyimbo hizo akiingia na wimbo wake wa Unikumbe. Shusho, mama wa watoto watatu, anasema ni heshima kubwa kwa Mungu na kwake hasa kwa kuwa alishindanishwa na wanamuziki wenye vipaji vikubwa vya uimbaji wa nyimbo za Injili.

“Kidogo nilipata hisia za woga iwapo ningeshinda hasa kutokana na ushiriki wa Alice ambaye ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za Injili, lakini pia shindano lilifanyika nchini kwao hivyo nilihisi kuwa alikuwa na mashabiki wengi zaidi, lakini Mungu ni mwema nikapata mimi hiyo tuzo, hivyo nina kila sababu ya kumshukuru Mungu,” anasema.

Shusho anasema ushindi huo umemfanya ajisikie kumheshimu na kumnyenyekea zaidi Mungu kwa kumpeleka kila hatua, lakini pia anaona fahari kuwa watu wa ndani na nje ya Tanzania wanatambua kipaji chake na kazi aliyopewa.

“Naona ushindi huu mbali na kumheshimu Mungu zaidi, lakini pia naona nimepewa jukumu zaidi kwa maana ya kukitumia kipaji changu nilichopewa kwa kuimba zaidi ya hapa na kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia uimbaji wa Injili,” anasema.

Shusho anasema msingi wa uimbaji wake umeanzia nyumbani kwao baada ya kuzaliwa katika familia ya Kikristo ambayo ilipenda kuomba na kusali na alikuwa akihudhuria Shule ya Jumapili ambapo watoto walikuwa wakifundishwa dini, na huko ndiko alikoanzia kuimba.
Anasema alipokuwa akiendelea kukua alijiona kuwa na wito na akaona ajaribu kuimba mwenyewe na kugundua ana kipaji na wito wa kuimba nyimbo za Injili, hivyo alianza kutunga nyimbo zake. Anaeleza kuwa mwaka 2003 aliamua kuingia studio baada ya kupata msukumo na alitengeneza muziki wake mwenyewe.

“Unajua kuna wengine wanaimba nyimbo za Injili, lakini ukiusikiliza uko katika hali ya ama kumjibu mtu au kumshambulia mtu baada ya kuapa jambo fulani mimi ni tofauti naimba kumsifu na kumuabudu Mungu,” anasema.
Hadi sasa Shusho ameshatoa albamu nne ambazo ni Kitu Gani, Unikumbuke, Nipe Macho, na Kwa Kanisa la Kristo ambapo anasema kuwa albamu ya Unikumbuke aliyoizindua mwaka 2008 ndiyo iliyomtambulisha vyema kwa mashabiki wa muziki wa Injili.

Mwanadada huyo mwenye mvuto wa sura na tabasamu la bashasha anaelezea kuwa muziki wa Injili unakua na kukua huko kunatokana na kuwa zamani kwaya ndizo zilizokuwa zikijulikana lakini tofauti na sasa nyimbo za Injili zimepenya na unakuta zikitambulika katika matamasha na mashindano makubwa ya nyimbo za Injili.
Shusho anasema kuimba kwake
 nyimbo za Injili kumemuwezesha kupata faida mbalimbali ikiwemo jamii kumtambua na kukifahamu kipaji alichonacho, pili kazi zake kutambulika na kukubalika, tatu anajiona kutumika vizuri na kwamba anaamini Mungu anaona anavyofanya vyema kazi yake na nne imemuwezesha kufahamika ndani na nje huku akisema kuwa Mungu amempa maono ya mambo ya mbeleni.

Shusho amepata tuzo ya EMAS, Meya Cup iliyotolewa nchini Kenya, Tuzo za Muziki wa Injili (Gospel Music Awards) iliyotolewa hapa nchini ambapo aliibuka mshindi wa Msanii Bora wa Muziki wa Injili na tuzo ya Kenya Groove Music Awards akiibuka msanii bora wa nje.
Akizungumzia mtindo wa muziki wa Injili hivi sasa anasema kila mtu amepewa staili yake ya uimbaji lakini waimbaji wanapaswa kukumbuka kila watu wana utamaduni wao kwa hiyo ni vema wakaimba kwa kuzingatia mazingira ya nchi.

“Kama nilivyosema nyimbo zangu ziko kwa mtindo wa kusifu na kuabudu ndio maana naimba taratibu na hivyo ni rahisi mtu kusikiliza nyimbo zangu hata akiwa anasikiliza katika redio wakati anaendesha gari njiani au amerudi nyumbani anataka kutulia lakini akisikiliza nyimbo za Injili, mimi najiamini na naamini staili yangu ni njema zaidi,” anasema.

Mbali na kuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Shusho anasema anapenda kupendeza na kuonekana maridadi na ndio maana pia anajishughulisha na masuala ya ubunifu wa mavazi na pia ananunua bidhaa au vitu kutoka nje.
Lakini pia Shusho ni mtangazaji wa runinga ya Sibuka akiendesha kipindi kinachojulikana kama Gospel Hits huku akieleza kuwa lengo lake ni kuanzisha kipindi chake cha runinga ambacho atakiita ‘Christina Talk Show’ na kwamba kitakuwa kikijadili masuala mbalimbali ya kijamii bila kubagua kabila au dini kwani lengo ni kuisaidia jamii ya Watanzania.

Mwimbaji huyo ameolewa na amebahatika kupata watoto watatu anasema amesoma hadi kidato cha nne kisha akasomea masuala ya teknolojia ya mawasiliano (IT) katika Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC), lakini matarajio yake ni kujiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kupata elimu zaidi.

Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono mwanamuziki huyu ambaye amepata bahati ya kipekee kuchaguliwa kuchuana na waimbaji wengine kutoka barani Afrika. Shusho ameingia katika kategori mbili ya mwanamuziki bora wa Afrika Mashariki na mwanamuziki bora wa kike barani Afrika, tuzo hizo zitatolewa Julai 7, mwaka huu, jijini London nchini Uingereza.

namna ya kupiga kula soma maelakezo hapa chini

bonyeza hapa http://africagospelawards.com/nominate.html na fuata maelekezo hapa chini.


KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: