Jumatatu, 25 Juni 2012

PINDA 'AWAPIGIA MAGOTI' VIONGOZI WA DINI

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini na viongozi wa vyama vyote vya siasa wakiwamo madiwani, kuhamasisha na kuelimisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa kitaifa ambalo litafanyika kuanzia Agosti 26 mwaka huu nchini kote.

Pinda alitoa wito huo jana, wakati akifungua mafunzo ya wakufunzi 150 wa sensa ya watu na makazi ngazi ya Taifa , katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini mjini hapa.

Waziri Mkuu alisema viongozi hao wakiwamo masheha, watendaji wa kata, wenyeviti wa mitaa na vijiji, wanapaswa kuwaeleza wananchi umuhimu wa kushirikiana na makarani, wasimamizi na watumishi wengine watakaofanyakazi ya sensa katika kipindi cha kuhesabu watu, ili kufanikisha zoezi hilo.

“Naomba pia kutumia fursa hii, kuwakumbusha wananchi wote, kuwa kazi ya kuhesabu watu itaanza Agosti 26 na kuendelea kwa siku saba, ninaomba wananchi mtunze kumbukumbu za taarifa za maswali yatakayoulizwa kwa watu wote watakaolala kwenye kaya zenu usiku wa kuamkia siku ya sensa Agosti 26, mwaka huu’’, alisema Pinda.

Alisema kazi ya sensa haikusudii kusimamisha shughuli za kiuchumi au kijamii kwani makarani wa sensa watapita kwenye kaya muda wowote katika kipindi cha simu saba.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa kila mtu atakayelala nchini usiku wa kuamkia Agosti 26 lazima ahesabiwe mara moja”, alisema Pinda.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, aliwatoa hofu watu kuhusiana na zoezi hilo kwa kuwaeleza kuwa taarifa zote zitakazotolewa na mtu, zitakuwa ni za siri.

Pinda alisema katika zoezi hilo la sensa mwaka huu, Serikali imeamua kwamba uingizaji wa takwimu za sensa kwenye kompyuta utafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya “Scanning” ijulikanayo kama Optical Mark Reader(OMR) technolojia ambayo ilitumika pia katika sensa ya mwaka 2002 na kuwa na ufanisi mkubwa.

Katika ufunguzi huo, Waziri mkuu pia aliwataka wakufunzi hao, kwenda kutoa elimu nzuri katika ngazi mbalimbali ili kufanikisha zoezi hilo la sensa mwaka huu.

Awali waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, alisema Serikali imetenga fedha za kutosha kufanikisha zoezi hilo ambalo lengo lake kuu ni kujua idadi ya watu na kukusanya taarifa za kina za kidemografia, Kiuchumi, kijamii na maelezo ya makazi ili kupata takwimu muhimu za kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya wananchi hasa katika utekelezaji mipango kadhaa ya maendeleo ya Taifa, ikiwapo ya malengo ya millenia

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni