Jumatatu, 25 Juni 2012

KADINALI PENGO: WAHUNI WASIACHWE KUCHOMA MAKANISA ZANZIBAR


Mwadhama Polykarp Kardinal Pengo
 
      

ASHANGAA SMZ KUZIDIWA NGUVU, UAMSHO YAKUBALI KUSHIRIKI MCHAKATO WA KATIBA MPYA
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ‘kudhibiti wahuni wanaotaka kuvuruga amani visiwani humo’.

Kauli hiyo ya Pengo ni ya kwanza tangu kuibuka kwa vurugu visiwani Zanzibar mapema mwezi huu, na kusababisha uharibifu wa mali, huku makanisa yakilengwa zaidi na kikundi kinachojiita cha Jumuiya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI).

Pengo alitoa kauli hiyo wakati wa ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Msalabani Bagamoyo, mkoani Pwani, ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, utakaofanyika kwa siku 30 kuanzia jana.

Kardinali Pengo alisema, ‘wahuni hawawezi kuizidi Serikali makini’.“Makanisa yetu yamecomwa moto na watu wahuni. Kama Serikali ipo na haiwezi kuchukua hatua dhidi ya wahuni, usalama uko wapi?” alihoji Kardinali Pengo.

“Wahuni wanaweza kutuunguzia makanisa saba kwa mpigo, lakini mbele ya hapo kuna makanisa kadhaa ambayo yalikwishaunguzwa na kubomolewa na hao wahuni,” alisema.Pengo aliendelea kuhoji, “Kama sasa wahuni wameishinda nguvu Serikali ya watu kwa hiyo tutawaliwe na wahuni na wafanye lile wanalolitaka, tunajiuliza tunakwenda wapi?

Mara baada ya vurugu za Zanzibar, jopo la maaskofu kutoka madhehebu mbalimbali, walifanya mazungumzo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), huku wakiituhumu kushindwa kudhibiti vitendo vya uchomaji moto makanisa na kuihadharisha kuchukua hatua za haraka.

Jana, Pengo alilitaka shirika hilo kumsaidia Askofu Augustine Shayo wa Jimbo Katoliki Zanzibar, kuunganisha nguvu zao katika harakati za kuimarisha amani.
Pengo alisema mbali ya vurugu hizo, hivi sasa utumwa bado unandelea kukithiri nchini, hususan kwa viongozi wa Serikali kuwakandamiza wananchi wa hali ya chini.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wanaotaka utumwa uendelee kuwapo kutokana na matendo yao dhidi ya wananchi.

“Tanzania ni huru sawa, lakini mimi sitaki kusadiki kuwa ni huru kwa kila mmoja na kila Mtanzania, wapo watu ambao wangependa wao waneemeke hata kwa madhara ya wengi bila huruma hadi siku ya leo,” alisema na kuongeza:

“Tangu Shule ya St. Marian inaanzishwa, kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitaka watoto wao wakasome pale na watoto wa maskini wasipate nafasi.”

Alitoboa siri kuwa ‘kuna barua za maombi zisizo za msingi ambazo amekuwa akipelekewa Askofu Shayo na kuzikataa, na wakati mwingine amekuwa akitishiwa maisha, kwani wapo wanaotaka kuwasomesha watoto katika shule nzuri ili waendele kujineemesha. Sasa huu sio utumwa?’
Kardinali Pengo alililitaka Shirika la Roho Mtakatifu kutumia mkutano huo kuendelea kuhimiza amani hapa nchini na kutupia jicho Zanzibar, ambako amani inavurugika kwa matendo ya watu aliowaita wahuni.

Mkutano wa Shirika

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, Padre John Kuff kutoka Ghana, mkutano huo unafanyika Afrika kwa mara ya kwanza, tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 1868.

Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo wa 20 ambao umekuwa ukifanyika kila baada ya miaka sita, na mkutano wa mwisho ulifanyika Ureno mwaka 2004.
Baadhi ya nchi zitakazoshiriki mkutano huo ni Canada, Nageria, Ureno, Ufaransa, Ghana, Uingereza, Irand na mwenyeji Tanzania.”

Akizungumzia shirika hilo, Pengo alisema wakati linaanza kazi nchini walikuta amani imevurugika, lakini walifanya kazi kubwa amani ikarejea, hivyo alilitaka kusimamia ukweli hata kama watu wengine watawabeza.

Kipozi aahidi amani
Akitoa salamu za Serikali kanisani hapo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema washiriki wa mkutano huo wawe na amani kwani ulinzi utaimarishwa wakati wote.

“Kwa siku zote 30 za mkutano huu ulinzi na usalama utaimarishwa ili kuhakikisha mnafikia malengo yenu,” alisema Kipozi.


KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni