Jumatano, 30 Mei 2012

Mwema, Aboud wahaha kurejesha Amani Zanzibar

 
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema
















Elias Msuya na Salma Said, Zanzibar
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mohamed Aboud pamoja na viongozi wa dini jana walitembelea maeneo yaliyoshambuliwa katika vurugu zilizotokea visiwani hapa.Ziara hiyo imekuja wakati hali ya amani ikielezwa kurejea visiwani hapa baada ya ghasia zilizoanza Jumamosi usiku na kuendelea hadi juzi.

Wakizungumza baada ya ziara hiyo, viongozi wa makanisa visiwani hapa walitoa malalamiko yao kuhusu vitendo vya uchomaji na uharibifu wa makanisa huku wakiitaka Serikali kutumia nguvu ya ziada kuingilia kati suala hilo wakisema tangu mwaka 2001 hadi sasa jumla ya makanisa 23 yameshachomwa moto Zanzibar.

Katibu wa Umoja wa Wachungaji wa Zanzibar, Jeremiah Kobero alisema licha ya makanisa matatu kuchomwa na kubomolewa katika vurugu hizo za juzi, kuna matukio 23 ya uchomaji moto makanisa yaliyotokea tangu mwaka 2001 na Serikali hajachukua hatua madhubuti kudhibiti.

Alitaja baadhi ya matukio hayo kuwa uchomwaji moto wa makanisa ya The Church of God na Siloam na makanisa mawili yaliyoko Masunguni mwaka 2001, Kanisa la EAGT la Fuoni mwaka huohuo, Kanisa la Pefa mwaka 2009, Kanisa la Mwera mwaka 2012, Kanisa la Redeemed, Dilikane mwaka 2001, yote ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Makanisa yaliyochomwa moto katika Mkoa wa Kaskazini kuwa ni Kanisa la Tunguu, Unguja Ukuu, Kanisa la CMF, Chukwani na Manyanya. Alisema hali hiyo pia imejitokeza Pemba.

Askofu wa Kanisa la TAG, Kariakoo - Zanzibar, Dickson Kaganga aliwataka viongozi wa Serikali kuchukua tahadhari mapema kabla vurugu hazijatokea.

“Wakristo tumewafundisha kuvumilia… juzi walipovamia hapa walichoma moto Biblia 50, ingekuwaje sisi tumechoma japo kitabu kimoja tu cha Kurani? Hayo makanisa yote yaliyochomwa taarifa ziko polisi, lakini ukienda kutoa taarifa unaulizwa, una kibali? Yaani wanakutafutia tena kosa,” alisema askofu Kaganga.

Makamu Mkuu wa Askofu wa TAG Taifa, Askofu Magnus Mhiche alihoji kitendo cha wahuni kuvamia makanisa ilihali Serikali ipo: “Mimi siamini kama ni Waislamu wamefanya haya.... Hivi kweli wahuni wanatawala Zanzibar?” alihoji.

Askofu wa Kanisa Kuu la Anglikana, Michael Hafidhi aliiomba Serikali kudhibiti mahubiri yanayotukana dini ya Kikristo kwa njia ya kaseti akidai kuwa yanachochea vurugu.

“Zipo Kaseti zinazotukana Ukristo na kuchochea vurugu. Tunaomba Serikali idhibiti. Hata ile kamati yetu ya ushirikiano wa dini nayo imekufa inabidi ifufuliwe,” alisema.

Mwakilishi wa Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Thabit Jongo aliwataka Waislamu kuvumiliana na Wakristo akisema kuwa hata Mtume (SAW) alifanya hivyo wakati akiitetea dini yake.

“Hata Mtume wetu (SAW) alipopata tabu alipokuwa Madina alikimbilia kwa Wakristo. Mpaka Uislamu ulipoenea Makka yote. Hata alipotoka Madina na kwenda Makka aliyempeleka hakuwa Mwislamu. Nashangaa leo ninaposikia eti Waislamu wanachoma makanisa,” alisema Jongo na kuongeza:

“Hawa ni Waislamu gani? Mbona wamechoma hata bendera ya CCM, wamechoma baa na kunywa bia. Nini hasa malengo yao?”

Akijibu hoja za viongozi hao, Aboud alipiga marufuku mihadhara na maandamano yanayofanywa na vikundi vinavyopinga Muungano... “Baadhi ya viongozi wa dini wanatoa maneno ya uchochezi, yanachochea vurugu zote hizi…. Maneno ni sumu, ndiyo tumeiingiza nchi katika machafuko yote haya. Kuanzia sasa ni marufuku kufanya maandamano na mikusanyiko yoyote ya aina hiyo.”

IGP Said Mwema alisema jeshi lake limeongeza ulinzi katika maeneo maalumu yenye usalama mdogo hasa makanisa... “Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa tunadhibiti maeneo maalumu ili yasiendelee kuvamiwa. Tunafanya uchunguzi ili kuhakikisha nani hao wanaofanya vurugu, kwa nini na wako wapi.”

Alisema jeshi hilo kwa sasa lina kikosi maalumu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kudhibiti machafuko kisiwani humo na kwamba hadi jana, watu 46 walikuwa wamekamatwa na kati hao, 43 wamefikishwa mahakamani huku wengine watatu wakifanyiwa uchunguzi.

Alikiri jeshi lake kuchelewa kuzuia uhalifu huo na kusema hatua iliyopo sasa ni kudhibiti usiendelee... “Kuna mifumo mitatu ya ulinzi, kwanza ni kuzuia kabla mambo hayajatokea, kwa hapo sisi tumeshachelewa. Tuko hatua ya kudhibiti yasiendelee na baada ya hapo tutajenga amani iwe endelevu.”Vyama vyalaani

Vyama vikubwa vya siasa nchini, CCM, CUF na Chadema vimelaani vurugu hizo vikisema hazijengi badala yake zinabomoa umoja na mshikamano uliopo baina ya Wazanzibari.

“Chama Cha Mapinduzi kinalaani vitendo hivyo na kuzitaka Serikali zote kudhibiti hali ya amani na utulivu tuliozoea na kuwachukulia hatua kali wote waliosababisha vurugu hizo” ilisema taarifa ya CCM kwa vyombo vya habari jana.

Taarifa ya CUF iliyosainiwa na Salim Bimani imesema: “Vitendo vya watu wachache kuharibu mali za watu ni uvunjifu wa sheria na kinyume na utamaduni wa Kizanzibari. Uchunguzi wa kina ufanyike na waliohusika wachukuliwe hatua bila ya uonevu wala upendeleo.”

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Yussuf Naibu alivitaka vyama vya siasa kutoandaa makundi ya vijana ambayo mwisho wake vinashindwa kuwapatia kazi na hatima yake kugeuka kuwa vikundi vya kihalifu.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FACEBOOK Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: