Ijumaa, 11 Mei 2012

KANISA LA EFATHA LATISHIWA KULIPULIWA NA AL-SHABAAB

Kikundi kinachojiita ‘Al-Shabaab Tanzania’, kimetishia kuteketeza kwa mabomu eneo lote pamoja na majengo ya Kanisa la Efatha, lililopo Mwenge, jijini Dar es Salaam, wakati wowote kuanzia sasa, kuhakikisha linabaki kama uwanja wa kuchezea mpira, taarifa ambazo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), Robert Manumba, amesema hajazipata na kuahidi kuzifanyia kazi.Mpango huo umeelezwa na kikundi hicho kuwa utatekelezwa kupinga uongozi wa kanisa hilo kujichukulia sheria mikononi kila mara na kunyanyasa watu wasio na hatia bila sababu za msingi.Kanisa hilo linamilikiwa na kuongozwa na Nabii na Mtume wake, Josephat Mwingira.

Mpango huo wa kikundi hicho kinachojiita cha chenye msimamo mkali kinachopigania haki zilizoshindwa kutekelezwa na serikali kwa wakati kupitia mamlaka zake zinazohusika hususan mahakama, umebainishwa katika taarifa yake ya Aprili 20, mwaka huu.

 Nakala ya taarifa ya kikundi hicho yenye anuani ya sanduku la posta Tanga, Tanzania, imetumwa pia, ikivitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinatangaza taarifa hiyo.
“Vyombo vya habari tunavitaka kutoa taarifa hii kwa umma kwamba tunao mpango wa kuteketeza kwa mabomu eneo lote na majengo ya Efatha Ministry iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam wakati wowote kuanzia sasa na kuhakikisha eneo hilo linabakia kama uwanja wa kuchezea mpira,” inadai sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na mtu anayedai kuwa ni mwakilishi mkazi wa kikundi hicho lakini hakujitaja jina.Katika taarifa hiyo, kikundi hicho kimewataka waumini wote kutohudhuria ibada ya aina yoyote katika kanisani hilo.

 Pia kimewataka kutofanya kazi yoyote ya kiuchumi ili kuepuka milipuko inayoweza kutokea eneo hilo wakati wowote.“Kwa hiyo, hatutaki kuwauwa watu wasio na hatia, lakini kwa wale watakaopuuzia taarifa hii waendelee tu kuhudhuria kanisani hapo au katika kitegauchumi chao cha benki halafu familia zao zitashuhudia kitakachowatokea,” inadai taarifa hiyo.Kikundi hicho kinadai kuwa kitendo cha uongozi wa kanisa hilo kujisafisha kupitia gazeti moja linalotolewa kwa lugha ya Kiswahili kila wiki, hakina msingi, badala yake ni uongo mtupu.

Kimesema kujisafisha kwa uongozi huo kwamba wanaongoza roho za watu na kujikinga kwa mwamvuli wa kanisa na kuwaua wengine ni dhambi kubwa siyosamehewa. “Hata hivyo, kama kanisa hilo linaweza kuwa na haki kwa namna yoyote ile, Biblia yao kama mhimili mkuu wa imani yao ni wapi pameandikwa kwamba ni haki kumvunjia jirani yako nyumba yake?” kilihoji na kuongeza:
“Mbona Yesu alisema jirani yako akikupiga kofi shavu la kulia mgeuzie na la kushoto? Iwapi kwa Efatha subira hii hadi kukiuka agizo la mahakama na kuvunja sheria ya nchi.”

KAULI YA EFATHA
Mwingira jana hakupatikana. wasaidizi wake walisema  kwamba alikuwa katika kikao ambacho haikufahamika kilikuwa kinafanyika wapi.Hata hivyo, walipoulizwa kuhusiana na kuwapo kwa tishio hilo, walisema hawajapata taarifa hiyo ya kutaka kufanyika kwa uhalifu huo kwenye kanisa lao..


DCI MANUMBA
Kwa upande wake, DCI Manumba aliahidi kuzifanyia uchunguzi taarifa hizo ili kujua ukweli wa suala hilo. “Tutachunguza jambo hilo kufahamu kama ni kweli au kuna kikundi cha watu wachache kinataka kutishia watu. Taarifa hizo zilikuwa hazijanifikia, wewe ndio unaniambia,” alisema Kamishna Manumba.

KAIMU RPC KINONDONI
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, John Mtalimbo, alisema taarifa za tishio za kikundi hicho dhidi ya kanisa hilo bado hajazipata.Alisema anachokifahamu katika kanisa hilo ni kuwa awali palikuwapo na mgogoro na kuahidi kulifanyia kazi jambo hilo ili kufahamu ukweli juu ya taarifa zilizoenezwa na kikundi hicho.
Kikundi hicho kinadai kuwa jambo lingine linalothibitisha kwamba Efatha chini ya Mwingira ina huduma ya kutia shaka kiroho ni pale wanapojichukulia sheria mkononi kuvunja na kuharibu mali za jirani zao ilihali kesi ya msingi kuhusiana na eneo hilo ipo mahakamani na hukumu bado haijatoka.
Kinadai dini nchini zipo kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi, lakini dini ya aina yoyote haipaswi kuwa juu ya sheria, katiba, mahakama wala watu wenyewe. Kinadai kuwa mtu anayo haki, utashi na uhuru wa kuabudu na si kujificha chini ya kivuli cha dini au kanisa na kufanya uharibifu juu ya wengine.

 Kutokana na hilo, kinadai kuwa hata kama Efatha ingekuwa mmiliki halali wa eneo hilo, haikupaswa kujichukulia sheria mkononi kwa kuwavunjia wengine ilhali mahakama haijatoa hukumu kwa kuwa mahakama ilitoa taarifa ya eneo hilo kuendelea na shughuli zake kama kawaida.“Hivyo, basi umma wa Watanzania na wapenda amani duniani kote wanaona kwamba kanisa la Efatha ni lazima liwajibike kulipa mali zote za kiwanda kilichoharibiwa ili iwe fundisho hata kwa madhehebu mengine yasiyofuata nyayo za Yesu au Mtume,” kilidai kikundi hicho.

 Kikundi hicho kimetahadharisha kuwa taarifa yake hiyo haihusiani kwa namna yoyote ile na upande ulioathiriwa iwe kiwanda au wakazi wa Bagamoyo au Sumbawanga na kusisitiza kuwa taarifa hiyo ni ya kikundi maalum kilichodhamiria kuona haki inatendeka kwa namna yoyote ile.

“Na katika hili tunaamini kwamba tunakwendea peponi. Na hata hivyo huu ni mwanzo. Mengine yatafuata,” kilidai.
Mwenyekiti wa ulinzi wa Kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Kanali mstaafu Mama Kambo, alipoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo alijibu kwa kifupi kuwa hajaipata.

 Akizungumza jana mchana lilifika kanisani hapo, Mama Kambo alisema hawajapata taarifa za tishio hilo na wala hajui hatua za kuchukua ili kukabiliana na tishio hilo.Hata hivyo, baada ya kuonyeshwa  nakala ya barua iliyoandikwa na kikundi hicho, Mama Kambo alijibu kwa kifupi kuwa hawajui hatua zozote za kuchukua na kutaka mwandishi ampe ushauri.Juhudi za mwandishi kuwaomba kumpata Mwingira kuelezea tishio hilo ziligonga mwamba baada ya wachungaji waliokuwapo kusema kuwa ni vigumu kumuona moja kwa moja.

“Yaani huwezi kumuona Mwingira na wala hatuwezi kukupa namba yake ya simu labda subiri tuendelee kuwasiliana na wasaidizi wake,” alisema Kambo.
Hivi karibuni, kanisa hilo liliingia katika mgogoro baada ya kubomoa kiwanda cha Afro Plus ambacho kipo ndani ya uzio wa Efatha.Katika uharibifu huo waumini zaidi ya 50 walikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni na baadaye walifikishwa mahakamani.

Jana kulikuwa na ulinzi mkali katika kanisa hilo, na walinzi walijaribu kumzuia mwandishi asifike katika baadhi ya maeneo aliyotaka kupita na kumueleza kuwa utaratibu wa kanisa hauruhusu.
“Hiyo taarifa ni mpya na nimeisikia kutoka kwako. Ila tutaifuatilia ili tuweze kubaini ukweli wa jambo hilo na hatua kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Mtalimbo

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FACEBOOK martmalecela
Chapisha Maoni