Ijumaa, 20 Aprili 2012

UKATILI HUU JAMANI HOUSE GIRL AUA MTOTO KINYAMA! KWA KUMKABA MPAKA KUFA

Mtoto aliyeuliwa Anjela David

Mtoto mwenye umri wa miezi saba, Anjela David, anadaiwa kuuawa na mfanyakazi wa ndani jijini Dar es Salaam na kisha kutoroka na mizigo yake.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, baba mzazi wa mtoto huyo, David Salakana, mkazi wa Sinza Afrika Sana alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi, ingawa hana uhakika na muda kamili kitendo hicho kilipofanyika.

Alisema kuwa juzi majira ya asubuhi aliondoka na mkewe kwenda katika shughuli zao na kumuacha mtoto wao akiwa na mfanyakazi huyo aliyemtaja kwa jina moja la Marietha (19).
Salakana alisema mkewe, Anna Haule, ilipofika majira ya mchana alimpigia simu mfanyakazi huyo ili kufahamu hali ya mtoto wao kama tayari ameshampatia chakula au la.
Alieleza kuwa mfanyakazi huyo baada ya kupigiwa simu hiyo alijibu kuwa haelewi kama mtoto huyo amekula au la na kwamba yeye (Marietha) hayupo ameondoka zake.

Alisema baada ya kumjibu hivyo, mkewe aliamua kumpigia simu kijana mmoja ambaye alimtaja kwa jina moja la Ally ambaye ni jirani yake na kumuomba aende nyumbani kwake na aingie ndani na kumuangalia mtoto huyo.
Salakana alisema kijana huyo baada ya kufika alimkuta mtoto huyo akiwa amelala na alipojaribu kumuamsha hakuamka ndipo alipomueleza mkewe kuhusiana na hali hiyo.

Hata hivyo, Salakana alisema baada ya mkewe kupatiwa taarifa hizo alirudi nyumbani ghafla na ndipo alipoamua kumchukua mtoto wao na kumpeleka katika Hospitali ya Marie Stopes iliyoko Sinza ili kumuangalia kama ni mzima au la na ndipo alipojulishwa kuwa alishafariki dunia.
“Kutokana na mazingira hayo, nashindwa kukueleza kuwa mwanangu amefariki muda gani kwani muda ya mchana ndipo niliporudi na kumchukua na kumpeleka hospitali, sijaelewa vizuri kifo cha mwanangu kwani tulimuacha akiwa ni mzima halafu namkuta ni marehemu cha ajabu mfanyakazi katoroka na mizigo yake,” alisema Salakana.

Salakana alisema wakati anaingia chumbani alikuta chakula aina ya mtori kipo chini. "Sasa sijaelewa kama alimlisha mtoto chakula au la,” alisema.
Alisema tayari amekwisha kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Kijitonyama, lakini mfanyakazi huyo ambaye anatokea Mkoa wa Shinyanga hajapatikana.

Alisema mfanyakazi huyo baada ya tukio hilo, alifunga mizigo yake yote na kuamua kuondoka nyumbani hapo na kuelekea kusikojulikana huku simu yake ya kiganjani ikiendelea kuita bila kupokelewa.
Salakana alisema mfanyakazi huyo amekaa naye kwa muda mrefu na kwamba alimpata kupitia kwa dalali.

Alisema wamekuwa wakiishi na msichana huyo kama ndugu yao na kwamba hawajawahi kumgombeza kwa chochote, ingawa walimsisitiza suala la usafi kwa mtoto huyo na kuhakikisha anampatia chakula kwa wakati.

Aidha, Salakana alisema kuwa majibu waliyopatiwa kutoka kwa daktari yameonyesha kuwa mtoto huyo katika sehemu za mgongo wake amepigwa na pua zake zimeminywa.
Alisema jana jioni walitarajia kufanya kikao cha ndugu na baada ya hapo watatoa maamuzi kuhusiana na tukio hilo na kwamba mwili wa mtoto huyo unatarajia kusafirishwa leo kwenda Rombo mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza kwa masikitiko, Salakana alisema kuwa kuna jirani yake ambaye alikuwa akimtafuta ili amweleze kuhusiana na mfanyakazi huyo alivyokuwa akimfanyia vitendo vibaya mwanaye.

Alisema jirani yake alimueleza kuwa wakati Marietha akiwa anamlisha mtoto huyo chakula, alikuwa anamtukana matusi makubwa ambayo hayaendani na umri wa mtoto na wakati mwingine alikuwa anampiga.

“Huyu mfanyakazi sijui ni kwanini sikumuamini sana kwani hata nikiwa kazini nilikuwa narudi mapema na kuamua kushinda na mwanangu hapa dukani,” alisema. Mwanangu amefariki katika mazingira magumu, sielewi amemuua kwa kitu gani na kama sio yeye ni kwa nini aliamua kukimbia na mizigo yake yote?” Alihoji Salakana.
Mama wa mtoto huyo, alishindwa kuzungumzia tukio hilo kutokana na uchungu aliokuwa nao.

Naye bibi wa mtoto huyo, Beatrice Ndemasi, alisema kuwa kifo cha mtoto huyo kimewasikitisha kwa kuwa kimetokea ghafla kwani hakuwa mgonjwa.
Ndemasi alisema mjukuu wake alionekana kwenye mgongo wake kuwepo na alama ambazo zilivimbia damu alipofikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Alisema mwili wa mjukuu wake kwa sasa umehifadhiwa MNH kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi leo asubuhi.
Alisema wanategemea uchunguzi huo utawapatia majibu ili wabaini kilichomuua.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Kenyela alisema kuwa polisi bado wanaendelea kumtafuta mfanyanyakazi huyo wa ndani kwa tuhuma za mauaji.
Alisema mfanyakazi huyo aliachiwa mtoto na wazazi walipokwenda katika shughuli zao za kila siku na kumkuta ameshafariki naye akaondoka.
Kamanda Kenyela alisema ni lazima msichana huyo akamatwe kuhusiana tuhuma za tukio hilo.
CHANZO: NIPASHEKumekuwa na matukio mengi maovu yanayotendwa na jamii dhidi ya watoto. Watoto wanabakwa na vijana wenzao mashuleni hasa watoto wa kiume.Magazeti ya Tanzania yanaripoti matukio haya na baadhi ya vijana hao wako polisi na kesi zao ziko mahakamani.
Sambamba na tukuio la mtoto huyu, inasikitisha. NINASHAURI WAZAZI NA WALEZI
 WAJULISHWE KANISANI JUU YA HATARI HII, MAANA SI WOTE WANAOSOMA MAGAZETI NA
 KUSIKIA TOKA VYOMBO VINGINE VYA HABARI. MF: RADIO NA TV. 
Kutokana na majukumu mengi ya kujitafutia riziki ya kila siku. Wazazi na walezi wamesahau jukumu lao muhimu, nalo ni malezi ya kimungu na usimamizi wa watoto wao. Ajabu ya jambo hili ni kwamba miongoni mwa watoto wa kiume waliobakwa ni mtoto wa
mwalimu wa shule hiyo hiyo ambako vitendo hivyo viovu vinatendeka ni huzuni kiasi gani, na mwl (mama) hakujua, hadi mtoto alipoamua kuiba pesa ili akawapatie vijana wanaomtendea ukatili huo wasimtendee maana hapendi na anahumizwa.
Ndipo mama alipojua baada ya kuibiwa pesa na mwanae na mtoto kusema, kwanini ameamua kufanya hivyo. 

KWA KANISA TUSISAHAU KANUNI YA MUNGU KATIKA MAISHA;
1. MUNGU (USHIRIKA WAKO NA YEYE NAMBA MOJA)
2. FAMILIA YAKO (WEWE NDIO MZAZI, MLEZI NA MSIMAMIZI WA KWANZA WA WATOTO WAKO) 3. KANISA (YAANI HUDUMA).
Mungu awabariki.
Mch Kanemba D.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FACEBOOK martmalecela
Chapisha Maoni