Swali “UNAFANYA nini UNAPOFANIKIWA?” sio la kupuuza hata
kidogo. Mara nyingi nimesikia watu wakisema, “ukitaka kujua tabia ya mtu, mpe
pesa nyingi au cheo kikubwa” Nimetathmini sana maisha yangu binafsi, na
nikatazama maisha ya wetu wengine na kuona jambo hili, “maisha baada ya
mafanikio yanaweza kuwa baraka itakayokuinua kwenye baraka zingine, au laana
itakayokuangamiza wewe mwenyewe”.
Kama hukujua, mafanikio yanaweza kuwa uangamivu, angalia
hapa, “32Maana kurudi nyuma kwao wajinga
kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza” (Mithali 1:32).
Ukiangalia wakati wana wa Isarael wanatoka UTUMWANI kwenye nchi
Misri kwenda nchi ya ahadi, iliyojaa MAZIWA na ASALI, utaona onyo ambalo Musa
aliwapa, akisema, “11 Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika
amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. 12Angalia,
utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13na
makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu
yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; 14basi
hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya
Misri, katika nyumba ya utumwa; 15aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa
lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji;
aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, 16aliyekulisha jangwani kwa mana,
wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema
mwisho wako. 17Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono
wangu ndio ulionipatia utajiri huo. 18Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako,
maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake
alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumbukumbu la Torati 8:11-18).
Unafanya nini unapuvuka
ngazi fulani ya maisha, na kuingia ya juu zaidi, unapofika mahali ambapo “umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri
na kukaa ndani yake; 13na makundi yako ya ng’ombe na kondoo
yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu
ulicho nacho kitakapoongezeka”, (Kumb. 8:12b-13), Unafanya nini? Angalia
tabia yako ya sasa na ya zamani, kisha jiulize, wewe ni yule yule au ni
mwingine? Je! Hofu yako kwa Mungu ni ile ile au imebadilika? Jitihada zako
katika mambo ya Mungu imeathiriwa vipi na mafanikio yako? Unapojiuliza maswali
haya na kujijibu mwenyewe angalia usijipandelee wala kujihesabia haki kupita
kiasi. Ni muhimu kijiuliza na kujijibu na kuchukua hatua, wewe mwenyewe.
Sasa angalia tena jambo hili, unajua kwamba mafanikio yako
hayakuja kwa nguvu zako mwenyewe tu; unajua ulipomlilia Mungu wakati wa mateso
na vita vyako na Akakuvusha, Yeye ndiye aliyekupa “nguvu za kupata utajiri” (Kumb. 8:18). Mbona leo umesahau?
Ukitaka kujua kwamba umemsahau Mungu, kumbuka wakati “ule”
Alipokuwa Ngao na Kigao kwako. Kila ulipokuta magumu ulimgeukia kwa KUFUNGA na
KUOMBA, sasa umepata pesa na mafanikio, hayo ndio sasa yamekuwa ngao na kigao
kwako. Unakinga KIFUA kwa sababu unajua
unakazi nzuri, biashara nzuri, watu wanakujua, unajina kubwa mjini, nk. Wala
hukumbuki kumshirikisha tena Mungu mipango yako! Je! Hukumsahau Bwana Mungu
wako wewe? Mbona humgeukii tena katika MAHITAJI yako ila unatafuta faraja na
msaada kwa miungu mingine?
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni