Jumanne, 5 Aprili 2016

UNAFANYA NINI UNAPOFANIKIWA? (Sehemu ya 2)

 


Kwanini Mzabibu? Kwani Bwana alishindwa kuchagua miti mingine mizuri na ya gharama zaidi porini, akachagua kujiita Mzabibu? Haya ni mwaswali ambayo nilijiuliza. Maana Yesu ni Mzabibu na sisi ni matawi, na Baba yake ni Mkulima (Yohana 15:1, 5).
Nimeona mambo kadhaa:
1. Mungu amekuchagua sio kwa UBORA wako, ila kwa sababu amekupenda.
"1Neno la BWANA likanijia, kusema, 2Mwanadamu, mzabibu una sifa gani kuliko mti mwingine, au tawi la mzabibu lililokuwa kati ya miti ya msituni? 3Je! Mti wake waweza kutwaliwa, ili kufanya kazi yo yote? Watu waweza kufanya chango kwa huo, ili kutundika chombo cho chote? 4Tazama, watupwa motoni kwa kuni moto umeziteketeza ncha zake zote mbili, nao umeteketea katikati, je! Wafaa kwa kazi yo yote? 5Tazama, ulipo kuwa mzima, haukufaa kwa kazi yo yote; sembuse ukiisha kuliwa na moto, na kuteketea; je! Waweza kufaa kwa kazi yo yote?" (Ezekieli 15:1-5).
 
2. Kwa kuitwa MZABIBU au TAWI la mzabibu, maana yake, Mungu anajua MWANZO wako na udhaifu wako (kwamba huwezi neno lolote pasipo yeye), na ambavyo hukufaa kwa chochote; ila amekuchagua kwa KUSUDI lake na kwa AJILI yake, na anategemea MATUNDA kutoka kwako.
Ndo maana BWANA anasema, "Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni" (Yohana 15:16) Hatuna haki yetu wenyewe iliyotustahilisha kuitwa wana wa Mungu; sisi tumechaguliwa tu. Hii ni maana halisi ya Neema.
 
3. Kuna GHARAMA imelipwa kukufikisha hapo ulipo sasa.
Ukisoma Ezekieli 16: 1-63, Utaona jinsi ambavyo BWANA ameGHAMIKIA watu wake, na sasa WAMEFANIKIWA na WAMEMWACHA!
Angalia, mambo machache katika mlango huu:
[i]. Ulikotoka/Asili yako - umetoka kati ya mataifa
"Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti" (.
Eze. 16:3b)
[ii]. Kuzaliwa kwako - Hakuna aliyekijali, ulikuwa masikini tu aliyestahili kufa kwa sababu uliachwa. Hukupendwa, hakuna aliyekujali, huna jina.
"4Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa. 5Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa" (Eze. 16:4, 5).
 
[iii]. Mungu akakufuata katika hali yako mbaya na KUKUOKOA, ukapewa UZIMA bure.
" 6Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai" (Eze. 16:6).
[iv]. Mungu AKAKUBARIKI na KUKUONGEZA
"7Nalikufanya kuwa maelfu-elfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, huna nguo" (Eze. 16:7)
 
[v]. Mungu akakuFUNIKA aibu yako. Sasa unaHESHIMA na JINA mjini
"8Basi, nilipopita karibu nawe, nikakutazama; tazama, wakati wako ulikuwa wakati wa upendo; nikatandika upindo wa vazi langu juu yako, nikakufunika uchi wako; naam, nalikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu" (Eze. 16:8).
[vi]. Ukapewa kusafiwa kwa Neno na kujazwa Roho na VIPAWA, ambavyo vimekufanyia NAFASI ya KUKETI na wakuu wa nchi
 
"9Kisha nikakuosha kwa maji; naam, nalikuosha kabisa damu yako, nikakupaka mafuta" (Eze. 16:9)
[vii]. UTUKUFU wa Mungu ukadhihirika maishani mwako kwa ile NEEMA uliyopewa; Mkono wa Mungu ulidhihirika sana juu yako, naam, ukavikwa UTAYARI kwa ajili ya HUDUMA.
"10nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa hariri. 11Nikakupamba kwa mapambo pia, nikatia vikuku mikononi mwako, na mkufu shingoni mwako. 12Nikatia hazama puani mwako, na pete masikioni mwako, na taji nzuri juu ya kichwa chako. 13Hivyo ulipambwa kwa dhahabu na fedha; na mavazi yako yalikuwa ya kitani safi, na hariri, na kazi ya taraza; ulikula unga mzuri, na asali, na mafuta; nawe ulikuwa mzuri mno, ukafanikiwa hata kufikilia hali ya kifalme" (Eze. 16:10-13).
[viii]. JINA lako likawa MAARUFU kwa sababu ya ile NEEMA juu yako, na KUFANIKIWA sana juu ya nchi.
"14Sifa zako zikaenea kati ya mataifa kwa sababu ya uzuri wako; kwa maana ulikuwa mkamilifu, kwa sababu ya utukufu wangu niliokutia, asema Bwana MUNGU" (Eze:16:14).
4. Baada ya KUFANIKIWA umefanya nini? Je! Umemkumbuka BWANA na kuendelea KUMTAFUTA na KUMFUATA kwa BIDII?
[i]. Wapo walioABUDU mafanikio yao badala ya Mungu! Na kufanya MACHUKIZO yale ya MATAIFA walikotwaliwa.
 
"15 Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako, ukamwaga mambo yako ya kikahaba juu ya kila mtu aliyepita; ulikuwa wake" (Eze. 16:15).
[ii]. Je! Umekumbuka ULIKOTOLEWA na Mungu? Pale ulipokuwa sio kitu chochote, wala huna jina? Sasa, badala ya kuwapeleka wengine kwa BWANA unawapoteza na wale walio wadogo; Umewapotosha!
"21hata ukawaua watoto wangu, na kuwatoa kwa kuwapitisha motoni kwa hao? 22Na katika machukizo yako yote, na mambo yako ya kikahaba, hukuzikumbuka siku za ujana wako, ulipokuwa uchi, huna nguo, ukawa ukigaagaa katika damu yako" (Eze. 16:21, 22)
 
[iii]. Sasa unajijengea UFALME wako, na JINA lako na wala humwinui Mtakatifu wa Israel! Unajifanyia mambo yako kwa faida zako kwa kuzidisha machukizo yako.
"25Umejenga mahali pako palipoinuka penye kichwa cha kila njia, ukaufanya uzuri wako kuwa chukizo, ukatanua miguu yako kwa kila mtu aliyepita karibu, ukaongeza mambo yako ya kikahaba" (Eze. 25).
[iv]. Kwa ajili ya FAIDA yako unafanya KAMA wafanyavyo mataifa, na Jina la BWANA linatukanwa juu ya nchi. Wanasema, "hivi na huyu ni mtu wa Mungu, mbona anafanya hivi?"
"26Tena umezini na Wamisri, jirani zako, wakuu wa mwili; ukaongeza mambo yako ya kikahaba, ili kunikasirisha....28Pia umefanya mambo ya kikahaba pamoja na Waashuri, kwa sababu ulikuwa huwezi kushibishwa; naam, umefanya mambo ya kikahaba pamoja nao, wala hujashiba bado. 29Pamoja na hayo umeongeza mambo yako ya kikahaba katika nchi ya Kanaani, mpaka Ukaldayo, wala hujashibishwa kwa hayo" (Eze. 26, 28-29).
 
[v]. Je! Hukukaza mkono wako KUTAWALA na KUTUMIKISHA wengine kwa FAIDA yako tu?
"30Jinsi moyo wako ulivyokuwa dhaifu, asema Bwana MUNGU, ikiwa unafanya mambo hayo yote, kazi ya mwanamke mzinzi, 31apendaye kutawala watu; kwa kuwa wajijengea mahali pako pakuu penye kichwa cha kila njia, na kufanya mahali pako palipoinuka katika kila njia kuu; lakini hukuwa kama kahaba, kwa maana ulidharau kupokea ujira. 32Mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!" (Eze. 16:30-32)
 
[vi]. Umevifanyia nini VIPAWA vya Mungu? Fedha na utajiri, na Neema? Je! Hivyo havikuwa uharibifu kwa wengine na kubomoa Zaidi kuliko kujenga?
"17Pia ulivitwaa vyombo vyako vya uzuri, vya dhahabu yangu na vya fedha yangu, nilivyokupa, ukajifanyia sanamu za wanaume, ukafanya mambo ya kikahaba pamoja nazo" (Eze. 16:17)
5. Kuna jambo Mungu alitarajia kukona baada ya kukuinua kwa kiasi hicho. Je! Umerudi nyuma hata ukamsikitisha Mungu? Mafanikio yako yanamtukuza Mungu au yanamtukana?
Kumbuka hali yako ya mwanzo ulipokuwa si kitu, kama mti wa mzabibu usio faa kwa chochote, sasa uko juu sana kwa kuwa BWANA amekuinua.
Haya maneno yamesema na mimi kwa nguvu kubwa, na nimeona nilivyopungua. Nimeweka hapa, sio kukuhukumu ila kama mimi Frank nilivyopata changamoto na kujitathminina, nimeweka hapa ili uone kama kuna mahali pa kurekebisha, rekebisha; ILI kwa mara hii tena MAFANIKIO yako yawe Baraka si kwa watu tu ila na kwa Mungu pia.

Frank P. Seth
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: