“4 Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye
Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema,
Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! 15Elisha
akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. 16Akamwambia
mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu
yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. 17Akasema,
Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema,
Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda
Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. 18Akasema, Itwae mishale; akaitwaa.
Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. 19Yule
mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara
sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara
tatu tu” (2 Wafalme 13:14-19).
Katika tafakuri la mistari hii ya
2 Wafalme 13:18, 19, nimejiuliza maswali mawili makubwa: kwanini nabii Elisha
alikasirika mfalme Yehoashi alipopiga mishale mitatu tu? Na, mfalme Yehoashi
angejuaje kama anapaswa kupiga mishale mara tano au sita kama hakuambiwa?
Hii ni vita ya kiroho ambayo
mfalme Yehoashi ameanza dhidi ya adui zake Waashuri. Ukienda kwa watumishi wa
Mungu juu ya shida yako, au ukianza maombi kwa ajili ya shida fulani, hapo
tunasema umeanza vita kwa namna ya rohoni. Kumbuka, Yehoashi anajua uadui kati
yake na Washami, anajua kwamba baada ya muda kutakuwa na vita halisi kwa jinsi
ya mwilini au vita ipo, sasa ameamua kwenda kutafuta msaada wa kiroho kwa mtumishi
wa Mungu nabii Elisha.
Sasa angalia, kiwango na jinsi
anavyofanya mambo katika ulimwengu wa roho (maombi) kinaonesha kiwango cha hasira
au nia ya kushinda aliyonayo mtu dhidi ya jambo linalomsumbua. Kwa mfano, “Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. 17Eliya alikuwa
mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua
haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Akaomba
tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake” (Yakobo 5:16b-18).
Ninachoona hapa, wakati Elisha
amemwambia Yehoashi, “piga mishale”, Elisha
alitarajia kuona kiwango fulani cha kupambana katika ulimwengu wa roho ambacho
kinaonesha “hasira au nia” ya ushindi dhidi ya adui. Yehoiashi akapiga mishale mitatu
tu, Elisha akakasirika! Fikiri Mungu anataka uombe, ila kwa bidii! Sawa,
unahaki wewe, bidii ipo? Je! Unabidii?
Ukitaka kuona jambo hili angalia
tena hapa mfano wa BWANA Yesu, “1 Akawaambia
mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. 2Akasema,
Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. 3Na
katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema,
Nipatie haki na adui wangu. 4Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni
mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, 5 lakini, kwa kuwa mjane
huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. 6Bwana
akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. 7Na Mungu, je! Hatawapatia
haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 8Nawaambia,
atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani
duniani?” (Luka 18:1-8). Kilichomfanya mjane huyu apate anachotaka sio HAKI
yake ila BIDII yake! Kwa sababu huyu Kadhi ni dhalimu, huwa hajali haki za
watu, ila bidii ya huyu mama ikamtoa jasho. Huyu mjane angeenda mata tatu tu,
asingeweza kuvuka katika shida yake, ila alienda mara nyingi.
Sasa utajuaje kwamba mara ngapi (kiasi
cha maombi) inatosha? Kuna namna tatu
tu: kwanza, kama jambo unaloomba limetokea (umepata majibu ya maombi yako);
pili, Mungu amekwambia “acha kuomba juu ya hilo jambo”; na tatu, unasikia wepesi fulani hivi na hali ya kuvuka
(upenyo) ndani ya nafsi yako wakati ukiomba juu ya hilo jambo [hii ni ngumu
kueleza maana inatambulikana kwa uzoefu].
Kumbuka siku zote, endelea kupiga
mishalie (maombi) hadi upenyo utakapopatikana katika ulimwengu wa roho; omba
bila kukoma. Hiyo ni ishara kwamba kuna ushindi wakati utakapofika wa kufanya
vita vyako kwa jinsi ya mwili. Jambo jingine, nguvu na bidii unayoweka na kung’ang’ania
(kutokukata tama) ni muhimu sana ili kuweza kupokea ushindi wa vita
unavyopigana. Usiwe mlegevu katika ulimwengu wa roho, hakikisha unafurukuta kwa
nguvu zako zote na kwa bidii, tena kwa MUDA
mrefu. Acha kuomba kama unaombe chakula, jifunze kutofautisha uzito wa mambo na
bidii zake katika maombi, hivyo ndivyo utavuka siku zote kwa ushindi.
Frank P. Seth
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni