Ijumaa, 18 Septemba 2015

MTUNZI WA 'NAENDEA MSALABA' ANA USHUHUDA WENYE MGUSO WILLIAM WALFORD McDONALD



William McDonald alizaliwa tarehe 1 Machi 1810 Belmont Maine. Alitwaliwa kutoka maisha haya yapata Septemba 11, 1901, huko Somerville, Massachusetts. William ambaye alikuwa kipofu kama anavyoelezea kwenye wimbo wake huu maarufu wa Naendea Msalaba alimiliki duka dogo [kiosk] huko Coleshire, England huku siku kwa siku akikaa kwenye kivuli cha dohani akichonga na kung’arisha vipande vya mifupa ya kutengenezea viatu na vitu vingine vya urembo na kuviuza kwa ajili ya kujipatia kipato. Mahali pake pa kazi alitengeneza ushirika wa maombi na Mungu, wakati fulani akiibua masomo kwa ajili ya ibada ya siku ya Bwana ya Jumapili.

William Walford MacDonald hakupata elimu rasmi ila Mungu alimpa kipawa cha ajabu cha kimiujiza ya kuweka kumbukumbu akilini mwake ya sehemu kubwa sana ya Biblia takatifu na alipata mialiko wakati fulani ya kwenda kuhubiri, kuongea kwenye mihadhara na mijadala mbalimbali ya Injili. Alipopanda mimbarini, mhubiri huyu kipofu aliweza kurejea kwa kusoma aya nyingi za Biblia neno kwa neno akitaja na namba za sura na mistari kama ilivyoandikwa pasina kukosea hata kidogo wala kukwama, jambo ambalo lilivuta wengi kwenye mahubiri yake kwenda kumstaajabia kwa kipawa hicho. 

Siku moja mwaka 1842 Mtumishi mmoja wa Kimarekani aliyeitwa Tom Salmon alimtembelea William MacDonald kwenye kibanda chake cha duka. Kipofu William aliweza kuongea naye kwa ufasaha kwa ushahidi wa maandiko aliyokuwa akiyataja pasina kuwa na Biblia huku Pasta Tom akijaribu kumfuatilia kwenye Biblia yake kuona kama maandiko anayoyarejea yameandikwa kama anavyoyarejea au anakosea. Maongezi yao yalihusu mada ya maombi na furaha aliyopata katika ushirika wake na Mungu. Baadaye akamuomba Pasta Salmon amsaidie kuandika mistari ya beti alizoghani.

“Hii itakuwaje?” alijiuliza William pale Pasta Tom alipoanza kuandika, ilionekana hakuwa na uhakika wa thamani ya uumbwaji wake. Lakini hakuhitajika kuwa na wasiwasi. Shairi lake likaja kuzaa wimbo maarufu wa Sweet Hour of Prayer/Muda Mzuri wa Maombi. Sauti yake ikaja kuandikwa na William Bradbury.

Bila shaka tunaweza na tunapaswa kuomba mara kwa mara wenyewe. Lakini Biblia pia inafunua kuhusu thamani ya maombi ya ushirika, kuwa na ushirika wa kimaombi na wengine. Inasikitisha sana kuwa ni kwa nini mikusanyiko ya maombi ndiyo mikusanyiko yenye mahudhurio hafifu zaidi katika juma! Jambo hili lilimgusa sana kipofu William na kufunuliwa na Roho wa Mungu kuandika wimbo huo wa Sweet Hour of Prayer/Muda Mzuri wa Maombi. Waumini walikusanyika kwa ajili ya maombi kuelekea kuzaliwa kwa Kanisa siku ya Pentekoste kama ilivyo katika Mdo.1:14, na baadaye wakadumu katika maombi kama ilivyoandikwa katika Mdo.2:42 anasisitiza William MacDonald. Wengi wetu tunahitaji kujenga tabia, nidhamu na mazoea ya maombi kama William MacDonald anavyofunua katika wimbo wake huo ambao hauko kwenye vitabu vya nyimbo vya nyakati hizi.

William McDonald alikuja kuwa Pasta kipofu wa Kimarekani aliyechunga Kanisa la Methodist Episcopal. Pia alihudumu kama Mhariri kipofu, ambapo licha ya kuwa na elimu ndogo tu aliweza kuandika vitabu zaidi ya 84. Aligoma kupokea mrahaba wa maandiko yake ya nyimbo na vitabu lakini akaanzisha mfuko wake uliojulikana kama Believers Bible Commentary [BBC] wa kutafsiri kazi zake katika lugha mbalimbali za kigeni. 
Wimbo wenye ujumbe mzito wenye mguso mkali na upako kwa wote wenye dhambi na mahitaji mbalimbali na ambao pia ni maarufu sana katika madhabahu za Kanisa na mikusanyiko mbalimbali wa Naendea Msalaba ambao kama nyimbo zake zingine pia umeongelea uhalisia wa maisha yake aliughani mwaka 1870 jijini Brooklyn, New York, akihudumu kama Pasta katika jiji hilo. Anafunua kuwa alihisi uhitaji wa wimbo wa kuwasaidia wahitaji wa usafi wa moyo alipokuwa madhabahuni... jambo ambalo ni jepesi kwa maneno, lakini kweli kwa uzoefu alioupata na pia la ukamilifu wa upendo. Hayo ni maneno ya hekima kubwa na nzito sana yenye uvuvio wa Roho wa Mungu yaliyoijia Kanisa kwa kinywa cha Pasta kipofu William MacDonald aliyezaliwa karne ya 19 na kufa mwanzo wa karne ya 20, Pasta William MacDonald amelala katika makaburi ya msitu wa vilima vya Jamaica Plain, Massachusetts. Kanisa limepata ushindi, Utukufu kwa Mungu.
 

Tenzi za Rohoni – 57

NAENDEA MSALABA
1.Naendea Msalaba, Ni mnyonge na mpofu, Yapitayo naacha, Nipone Msalabani.
Nakutumaini tu, Ewe Mwana wa Mungu; Nainamia kwako; Niponye, mponya wangu.
2.Nakulilia sana: Nalemewa na dhambi; Pole Yesu asema; “Nitazifuta zote”.
3.Natoa vyote kwako, Nafasi nazo nguvu, Roho yangu na mwili, Viwe vyako milele.
4.Kwa damu yake sasa, Nimegeuka roho, Nikaziacha tama Nimfuate Yesu tu.
5.Yesu yuaja tena! Nimepevuka kwake, Kila chembe kamili; Msifuni yeye mponya!
Na, Douglas Majwala.




KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: