“Kila
apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama
mnyama” (Methali 12:1).
“Mwenye
haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani;
Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao” (Zaburi
141:5).
Umewahi kujiuliza faida za kupigwa,
kukemewa, kulaumiwa, kulalamikiwa, kuulizwa, nk. mara ufanyapo jambo ambalo
mwingine hakupenda au jambo ambalo si haki kufanya?
Nimejifunza jambo hili juu ya NAFSI ya
mtu ampendezaye Mungu; huchukua maonyo, makemeo, mapigo, matukano, laumu,
malalamiko, nk., kama mambo MUHIMU ya kujiweka vizuri zaidi na si mambo ya
kuleta chuki, hasira, kisasi, kinyongo, mafarakano, matengano, nk. Suleiman
anasema, “achukiaye kulaumiwa ni kama
mnyama”! Yaani, kwa binadamu BORA, kulaumiwa ni sehemu ya maisha, ili aweze
kujiboresha na kubadilika, ni lazima KUPOKEA na KUFANYIA kazi malalamiko na
malaumu bila KUWACHUKIA au KUWAPINGA wakulaumuo kwa maana wao ni MSAADA kwako
na sio lazima kwamba ni adui zako.
Akusaidiaye SANA sio akusifiaye tu,
bali akuambiaye MAPUNGUFU yako kwa uwazi (bila kujali sana lugha anayotumia).
Mara nyingi KIBURI kimejiinua na kusema, “sawa, angeniambia ila angesema taratibu,
sasa yeye ananipigia kelele”, au “mimi ni mtu mzima, naelewa ninachofanya”, “sipendi
kupangiwa cha kufanya”, nk.
Ukiona unaambiwa MAPUNGUFU yako
(kulaumiwa, kufokewa, nk.) halafu unasikia kama kuna kitu kinakukaba koo, basi
ujue unamahali pa kujiweka vizuri kwa maana hiyo hali itakuangamiza. Daudi
anasema, “Mwenye haki na anipige, itakuwa
fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana
siachi kusali kati ya mabaya yao”. Kwa Daudi, sio kukemewa tu, hata
akipigwa ni sawa. Umeona jinsi ambavyo Daudi hakuchagua namna ya kukemewa? Wala
hakuwafundisha wamkemeao namna ya kumkemea! Vyovyote vile, kwake ni fadhili, na
kama mafuta kichwani mwake, tena anakiambia KICHWA chake (akili za nafsi yake)
kisikatae maonyo (bila kujali sana yamekujaje).
Anaheri mtu yule AFURAHIYE aambiwapo
mapungufu yake, naam, ASIYEMCHUKIA amkemeaye na kumwonya, maana huyo atakuwa
BORA zaidi na ataona kuongezeka na baraka zikimfuata na kumpata. Na ajuapo
KUOMBA juu ya mapungufu yake, huyo atakuwa kama meli iliyotia nanga,
hatayumbishwa kamwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni