Peterson Hermas
ni mzaliwa wa kijiji cha Bungoi Kata ya Mlalo Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga
yapata miaka 45 iliyopita. Ameoa mke aliyefunga naye ndoa ya madhabahuni mwaka
1995 na Mungu amewajalia watoto watatu Hans, Paschal na Laura. Kwa sasa anaishi
jijini Dar es Salaam, Kata ya Kibamba, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Mtumishi
Peterson anatoka katika familia ya Kichungaji pia ya kimuziki, kwani mwaka 1952
marehemu babu yake Mch. Joshua Hermas ni kati ya Wachungaji walioteuliwa kwenda
Ujerumani kupata kozi ya Uchungaji. Babu yake huyu alipokuwa Ujerumani katika
kozi yake hiyo ya Uchungaji, alibahatika pia kujifunza somo la muziki kwa ajili
ya kufundisha katika Usharika pindi arudipo kutoka masomoni Ujerumani. Baada ya kurudi toka Ujerumani akiwa amebobea
katika fani ya muziki akiwa na uwezo wa kutumia kinanda, tarumbeta, violin,
aliona umuhimu wa kurithisha kizazi chake kipawa hicho cha muziki na akaamua kuifundisha
familia yake (wazazi wa Peterson) muziki ambapo nao wakaja kuwa na upako na
weledi katika tasnia ya muziki.
Mwaka 1982 baba
yake Peterson mzee William Hermas (marehemu) naye akabahatika kupelekwa Ujerumani
kufuatia kutunga wimbo na kuutuma Ujerumani na Wajerumani walipoupokea
walistaajabu, hawakuweza kuamini jinsi muziki ulivyoandikwa kwa ustadi tena kwa
mkono tu bila mashine ya chapa na ulivyopangiliwa kwa kila chombo cha muziki
kama tarumbeta, kinanda, violin, gitaa, ngoma n.k. ndipo walipomtumia baba yake
Peterson mzee William Hermas tiketi ya ndege ili aende Ujerumani wakamuone uso
kwa uso. Mzee William Hermas akaenda na kupokelewa vizuri. Katika ibada ya siku
ya Bwana, mzee William Hermas alipoitwa kuuimba wimbo wake huo, aliomba wapiga
vyombo wote na kwaya zote ambapo jumla yao ilipata watu 80; ziimbe pamoja wimbo
huo wakiufuatisha kwenye maandishi yake [noten] na kusisimua Washarika
waliohudhuria ibada hiyo na kuleta maadhi ya tofauti kabisa kuwahi kutokea
katika uimbaji Kanisani pale, ikawa furaha kuu katika Usharika ule aliofikia
baba yake Peterson uitwao Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Minden,
habari hii ikawa gumzo kiasi cha Meya wa jiji kuomba mzee William Hermas apelekwe
kuonana naye, mzee William Hermas akapelekwa kuwa mgeni maalum wa Meya na
habari zake zikaandikwa katika gazeti likiwa na kichwa “Mtanzania aliyetunga wimbo uliopigwa na watu themanini pia
aliyetufundisha kula ugali.”
Pindi mzee
William Hermas alipofika Ujerumani alikuta wamelima na kuvuna mahindi ambayo
yalikuwa wanapewa mifugo kama ng’ombe, punda na farasi. Mtumishi William Hermas
akawaambia “sisi kwetu Tanzania hiki ni chakula cha binadamu walakini ninyi hapa
mnawapa mifugo?” Akawaambia waandae mahindi yakasagwe, akawafundisha jinsi ya
kupika chakula cha ugali, ukapikwa ugali ulioliwa na wale watu wote pale Usharikani
siku ya Jumapili. Wajerumani wakapenda sana chakula cha ugali na hiyo ikawa
habari gazetini na akawafumbua macho Wajerumani wale kujua kuwa kumbe wao
walijua ni chakula cha mifugo lakini kwa wengine ni chakula cha binadamu!, wakajifunza
jambo jipya na Mtumishi wa Mungu William Hermas akafanyika baraka kwao kwa
namna mbalimbali na sio tu ule wimbo aliotunga ulioitwa “Mungu Aliupenda Ulimwengu”
aliourejea katika kitabu cha Yn.3:16 “kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee ili
kila amwaminie asipotee bali awe na uzima wa milele”
Mkurugenzi wa
muziki katika chuo cha muziki cha jiji hilo la Ujerumani aitwaye Reinhard
Neuhaus ambaye naye ni Msharika wa Minden akabarikiwa sana na Mtumishi William
Hermas kiasi cha kumjumuisha William Hermas katika chuo chake cha muziki na akaamuru
William Hermas pekee kati ya wanachuo wote akae nyumbani kwake. Wakaja kuwa
marafiki wakubwa kiasi cha kutembeleana Tanzania na Ujerumani kwa vipindi
tofauti.
Baada ya William
Hermas kufuzu mafunzo yake alirejea nyumbani Tanzania kuendelea na huduma, naye
kama baba yake Mch. Joshua Hermas akaja kuwafundisha watoto wake muziki
wakiwemo Dickson, Witness, Regina, Janeth, Rehema, Grayson, Upendo na Peterson
aliyepata mafanikio katika tasnia ya muziki kwa kuwa maarufu kwa wimbo wake wa
pambio wa “Namshangaa Bwana Yesu Kila Niendako Namkuta.” Mwaka 1977 Mtumishi
William Hermas aliwakusanya watoto wake na majirani wachache akaunda kikundi
cha kwaya alichokipa jina “Kwaya ya Mahubiri(C.Y.M)” kwaya ambayo ilikuwa maarufu
pale Usharikani Mlalo-Hoheni ambapo Mtumishi William alikuwa na upako na uwezo
wa kughani wimbo mpya kila Jumapili akirejelea somo la mahubiri la siku hiyo na
kwaya hii ikawa inaimba somo hilo la mahubiri pale Usharikani na ukawekwa
utaratibu kwamba kabla ya mahubiri kwaya ile lazima iimbe kwanza wimbo wenye
somo la mahubiri.
Kwaya ya C.Y.M ikaja
kuwa gumzo pale Usharikani kwani ilikuwa kwaya iliyojumuisha familia nzima ya
baba, mama na watoto. Mtumishi William Hermas hakuwa na mzaha katika suala la
kuhudhuria mazoezi kwa watoto wake kitu kilichowajengea nidhamu njema katika
suala la kumtukuza na kumwimbia Mungu. Mtumishi
Peterson Hermas anasema kipekee anamtukuza Mungu kwa ajili ya baba yao William
Hermas kwa msingi mzuri aliowawekea na kuwarithisha watoto wake kipawa hiki cha
muziki ambao mbegu aliyopanda baba yao kwao sasa imeota kwa mafanikio makubwa
sana kama tunavyoona hivi sasa watoto wa William Hermas wakihudumu kwa kufyatua
nyimbo zenye upako na mvuto sana. Kwaya ya C.Y.M ilikuja kutia nanga ya huduma
kufuatia waimbaji wake kuwa watu wazima waliolazimika kuanza maisha yao sehemu
mbalimbali japokuwa hawajaacha kutumika hata huko walikotapakaa katika Sharika
mbalimbali.
Peterson Hermas aliyetoa
ushuhuda huu sasa yuko jijini Dar es Salaam akihudumu katika Usharika wa
Kurasini Lutheran. Pale ana huduma ya kinanda cha Usharika na kufundisha kwaya
ya Nuru ya wamama. Kaka yake Dickson Hermas yeye yuko pale Hai Moshi Sanya Juu,
akihudumu kama Mwalimu wa kwaya, tarumbeta na kinada cha Usharika. Mdogo wake
Grayson Hermas yeye yuko Usharika wa Kisosora Tanga naye akiwa katika huduma
hiyo hiyo ya uimbaji katika nafasi ya Mwalimu wa kwaya na pia tarumbeta na
kinada. Familia hii inamtukuza Mungu kuwaweka shambani kwake kulisha kondoo
zake.
Ushuhuda ufuatao
unahusu namna Mtumishi wa Mungu Peterson Hermas alivyoibua wimbo wa “Namshangaa
Bwana Yesu Kila Niendako Namkuta.”
Ilikuwa
Jumapili moja nilikuwa napiga kinanda Usharikani kwetu kule Mlalo Lushoto Tanga,
alialikwa baba yangu mdogo kuja kuhubiri pale Usharikani. Kama nilivyokwisha
kuelezea juu ya familia yetu kuwa ni ya Kichungaji na kimuziki, tukajikuta
katika ibada ile baba ni mhubiri, mimi mtoto wake ni mpiga kinanda. Hali ile
ilimfurahisha sana baba yangu mdogo Mch. Richard Hermas. Mara baada ya Ibada,
akanitaka nijiandae niondoke naye nikahudumu Usharikani kwake Irente nje kidogo
ya mji wa Lushoto. Nikatii wito ule nikatoka pale Usharikani nikamwacha baba
yangu mzazi mzee William Hermas akichukuwa
nafasi yangu ya mpiga kinanda pale Usharikani akisaidiana na mzee aitwaye Nkanileka Shekolowa (marehemu).
Pale
Usharika wa Irente nikapewa jukumu la kufundisha kwaya kuu na tarumbeta. Usharika
ule wa Irente ulikuwa na vituo vitatu vya huduma; kituo cha watoto yatima,
kituo cha watoto wasioona na kituo cha wagonjwa wa akili. Baba yangu mdogo Mch.
Richard Hermas alikuwa pia mkuu wa Kituo cha wagonjwa wa akili akaniomba
nijiunge na wenzangu 9 niliowakuta pale katika huduma ya wagonjwa kwani
wagonjwa walikuwa wengi zaidi ya 90, nikajiunga katika huduma hiyo ngumu,
nikajiuliza nitamudu vipi kazi ile ngumu ya kusimamia na kuwaongoza watu wale? Wenzangu
niliowakuta pale namshukuru Mungu kwa ajili yao kwani walinitia moyo sana
ukichukulia nilikuwa kijana mdogo. Kipekee ninamshukuru baba yangu mzee Tahona
Shemkole aliyekuwa bega kwa bega nami katika huduma ile ya wagonjwa wa akili.
Nikiwa pale,
mkuu wa kituo cha watoto yatima mama Betty Hozza alikuja kuniomba
nikawafundishe wanafunzi (Wadada) waliokuwa wanajifunza mafunzo ya uuguzi pale
kituoni huku wakiwahudumia/wakiwalea watoto yatima, nikaombwa nikawafundishe
nyimbo kwa ajili ya mashindano ya Ukwata yaliyotakiwa kufanyika Tanga mjini.
Kilikuwa kikundi kidogo cha wasichana 16 tu. Ikafika siku ya mashindano,
tukasafiri kuelekea Tanga mjini tayari kwa mashindano. Tulipofika kule tukakuta
wenzetu nao wamewasili kwaya mbalimbali na idadi ya kwaya ilikuwa 14. Wenzetu
walikuwa wamekamilika kila idara, walikuwa na majoho mazuri, walikuwa
wamekamilika wavulana na wasichana.
Wale wasichana
wachache (wanafunzi) nilioenda nao wakaingiwa hofu wakajiona si kitu kwa jinsi
walivyoona wenzao walivyo wengi na walivyojipanga, nikawaambia “msihofu Yesu
wetu haangalii wingi wala mbwembwe” ninyi imbeni kama nilivyowafundisha na Bwana
Yesu akawe mwamuzi. Nikajihudhurisha pembeni nikajitenga nao kwa kitambo nikamwomba
Bwana Yesu atupiganie, kweli mwisho wa uimbaji kikundi hiki kidogo cha wadada (wanafunzi)
wakawa wa kwanza, wakajawa na furaha kubwa. Tukiwa njiani ndani ya gari wakati tunarudi,
wakaniambia Mwalimu sasa tunga wimbo twende tukiwa tunaimba. Nikawaambia “Mimi
namshangaa Yesu kila ninapoenda namkuta na ananijibu.” Na huo ukawa mwanzo wa wimbo huu
Namshangaa Bwana Yesu kila niendako namkuta.” Wimbo huu niliutunga
mwaka 1995. Zipo nyimbo nyingi nilizotunga na kufundisha kwaya mbalimbali. Nimeisha
hudumu kwa kufundisha kwaya Sharika zifuatazo:-
Kwaya
kuu Usharika wa Huduma Irente Lushoto 1989 – 1995, Kwaya kuu Usharika wa
Kariakoo 1996 – 1998, Kwaya kuu Usharika wa Kimara 1998 – 2001, Kwaya kuu
Usharika wa Kawe 2001 – 2003, Kwaya kuu Usharika wa Kiluvya 2003 – 2006, Kwaya
ya wamama ya Nuru Usharika wa Kurasini na huduma ya kinanda cha Usharika
ninapohudumu hadi sasa.
Mji
wangu ninamoishi, niliupata baada ya kupanda mbegu kwenye semina ya kupanda
mbegu iliyoratibiwa na New Life In Christ Ministry na kuhudumiwa na huduma ya
MANA ya Watumishi wa Mungu Mwl. Christopher na Diana Mwakasege Diamond Jubilee
jijini Dar es Salaam baada ya jasho jingi, kusubiri kwingi na muda mrefu sana
wa kutamani kumiliki makazi yangu binafsi. Ndani ya mwaka mmoja wa kupanda
mbegu, namshukuru Mungu aliziotesha na kuzikuza ambapo nilipata kiwanja na
kukamilisha ujenzi na kuhamia ndani ya mwaka huo huo mmoja. Mwisho.
Babu
yake Peterson Hermas Mch. Joshua Hermas alikuwa mwanamuziki aliyerithisha
watoto wake kipawa cha muziki na karama ya Kichungaji na watoto wake Richard
Hermas akaja kuwa Mchungaji na William Hermas akaja kuwa Mwanamuziki wa Injili
ambaye naye baada ya kwenda Ujerumani kama baba yake Mchungaji Joshua Hermas;
akaja akawarithisha watoto wake wote wanane na mke wake kipawa cha muziki na
akaunda kwaya ya familia yake aliyoiita C.Y.M na sasa watoto wake hawa wote
wanane wakike na wakiume wanahudumu kwenye uimbaji wengine wakiwa kwenye nafasi
za ualimu wa kwaya na vyombo ambapo wameunganisha vipawa vyote viwili vya
nyimbo na vyombo. Huu ni ushuhuda wenye uvuvio zaidi ambapo kizazi chote tangu
babu hata wajukuu wote wako kwenye huduma ya Mungu ya Uimbaji na
Kichungaji.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni