Jumatano, 13 Machi 2013

MTOTO ANAYEWAKA MOTO WA AJABU APONA BAADA YA KUFANYIWA MAOMBI



                                                                Christina Mjema
 
Mtoto anayedaiwa nguo zake kuwaka moto wa maajabu na kuteketeza nyumba katika kijiji cha Kabuku, wilayani Handeni mkoani Tanga, Christina Mjema (12), hivi sasa yuko Dar es Salaam akiendelea vizuri baada ya kuombewa.

Mtoto huyo, ambaye aliamriwa ahifadhiwe kituo cha polisi baada ya wananchi kumuogopa,hata hivyo, kanisa lililoamua kumsaidia kwa maombezi limekuwa likishuhudia mambo ya ajabu yakitokea kanisani hapo yanayodaiwa kuambatana na nguvu za giza.

Mtoto huyo anapatiwa huduma ya maombezi katika kanisa la House of Prayer shield of Faith Christian Fellowship maarifa kwa jina la kanisa la `Mzee wa Yesu' eneo la Boko Magengeni jijini Dar es Salaam.

Christina, mwanafunzi wa darasa la sita shule ya Msingi Kabuku, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, alikuwa anakabiliwa na tatizo la kuwaka moto nguo zake bila ya yeye mwenyewe kuungua pamoja na kusababisha nyumba ya wazazi wake kuteketea kwa moto.

Akizungumza , Mchungaji kiongozi msaidizi Justine Materu, alisema mtoto huyo alifikishwa kanisani hapo Februari 20, mwaka huu, baada ya kupata taarifa ya matatizo yake kupitia vyombo vya habari.

Alisema mara alipofikishwa hapo wachungaji wa kanisa hilo walimfanyia maombezi mazito kiasi ambacho hali hiyo imetoweka na ameanza kuishi kama watu wengine.
Alisema kabla ya kumchukua, hali ya mtoto huyo ilikuwa mbaya kiasi ambacho hakuweza kuvaa nguo yoyote kwa kuhofia kuwaka moto.

"Tunamfanyia maombi mazito ili hizi nguvu za giza alizokuwa nazo zitoweke kabisa, tumeanza kupata mafanikio makubwa kwa sasa hawaki moto tena," alisema Mchungaji Materu.
Mchungaji Materu alisema kazi ya kuombea mtoto huyo imekuwa ngumu baada ya kila siku kanisa hilo kuvamiwa na kundi la watu kutoka kijijini kwao wakitaka wamchukue.

Alisema kutokana na tatizo hilo wamechukua uamuzi wa kumzuia kanisani hapo wakati wakiendelea kumfanyia maombezi hadi hapo watu waliohusika na kumfanyia kitendo hicho waangamizwe.

"Tumemzuia kurudi nyumbani kwao mpaka watu hawa wanaokuja hapa usiku watakaposhindwa, tunapambana sana lakini kwa nguvu ya Yesu watashindwa," aliongeza kusema.

Aidha, Mchungaji Materu alisema tatizo lililompata Christina limekuwa kitu cha kawaida kwao, kwani mara nyingi wanatoa huduma ya maombezi kwa watu wenye matatizo mbalimbali ya mateso yanayotokana na nguvu ya giza, uchawi, mapepo na kupona kabisa.

Pamoja na maombezi hayo, Christina bado anakabiliwa na tatizo la kukosa nguo baada ya nguo zote kuungua moto, huku wazazi nao wakikabiliwa na umasikini mkubwa kutokana na vitu vyao pamoja na duka lao kuunguzwa na moto huo wa ajabu.

Kutokana na tatizo hilo, mchungaji Materu amewaomba wasamaria wema kumsaidia mtoto huyo ili aweze kuishi kama watoto wengine wakati anaendelea na huduma ya maombezi.
Kwa upande wake Christina alisema hali yake kwa sasa imerudi kama zamani, kwani tangu afike eneo hilo hakupata tukio la kuwaka moto wala vitu vinavyomzunguka haviwaki kama ilivyokuwa nyuma.

"Tatizo lile naona limekwisha, naishi kwa furaha sana kuliko siku ya nyuma sikuweza kukaa na watu kwani kila mara moto ulikuwa unawaka tu," alisema mtoto huyo.

Matatizo ya mtoto huyo yalianza mwezi Agosti mwaka jana baada ya kusimamishwa shule kutokana na kuwa na matatizo ya kukimbia huku akidai anaitwa na bibi mmoja anayeishi kijijini hapo.
Ilipofika Februari 9, hali ilianza kubadilika baada ya nguo zake alizokuwa amezivaa kuanza kuwaka moto ghafla pamoja na vitu mbalimbali vilivyokuwemo nyumbani kwao kuteketea kwa moto.

Tukio hilo limethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Muhingo Rweyemamu kwa kueleza kabla ya kufikishwa kanisani hapo kwa maombezi, wazazi wa mtoto huyo waliomba kibali cha kuwaita waganga wa jadi maarufu kama rambaramba ili watoe kile kinachodaiwa kuwa ni moto wa uchawi unaomtesa mtoto huyo.

Kwa watu watakaojitokeza kumsaidia mtoto huyo watume msaada wao kwa kutumia simu namba 0763818244 na 0715346562 au wafike kanisani hapo moja kwa moja.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: