Jumatatu, 25 Februari 2013

PENGO LILILOACHWA NA PADRI MUSHI WA ZNZ


Kabla ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi, Februari 17 mwaka huu, nimekuwa nikimfahamu kiongozi huyo wa kiroho kwa ukaribu kutokana na mchango wake kwa jamii hasa katika sekta ya elimu.
Alikuwa kiongozi wa karibu pia kwa waumini wake, kwa mafundisho na kuwajenga kiimani, akiwa Paroko wa Parokia ya Minara Miwili visiwani Zanzibar.

Lakini kwa hili la utetezi wa shughuli za maendeleo hasa katika sekta ya elimu, ndilo lililonisogeza na kunifanya niwe karibu naye, tukizoeana, kujenga mlahaka na maelewano ambayo kila mmoja wetu alikuwa muhitaji kwa fani na uwezo wa mwenzake.
Hapa, ninakusudia kuandika mambo niliyoyajua katika kipindi cha maisha na uhai wake, tulipokutana na kujuana hapa Zanzibar.

Amemondoka kabla ya wakati wake, baada ya maadui wa maendeleo kumpiga risasi na kuyakatisha maisha yake, akiwa bado anahitajika na familia yake, kanisa lake na jamii iliyomzunguka.
Wakati wote alitumia muda wake kuiasa jamii ili kuitafuta elimu popote inapopatikana, akiwahimiza wazazi kuwapelekea watoto wao shule na wakati mwingine, kuyakosoa mazingira magumu yaliowakabili wanafunzi katika msingi na muktadha wa kupata elimu.

Ukereketwa wake wa maendeleo ya elimu ndiyo maana Kanisa Katoliki lilipiga hatua kubwa kwa kuanzisha miradi mingi ya elimu, kwa faida ya kizazi kilichopo na kile kijacho visiwani Zanzibar.
Pamoja na Kanisa Katoliki kuwekeza kwa miongo mingi katika sekta ya elimu na baadaye shule zake kutaifishwa na serikali, bado halikuvunjika moyo, ila liliendelea kuanzisha miradi mingine mipya, ikazidi kuenea na kuunufaisha umma.

Miongoni mwa shule hizo ni zile za maandalizi, msingi na sekondari. Hapa Zanzibar, kuna Shule ya Mtakatifu Francis Maria, ambayo imejenga mtandao na kuwaunganisha wanafunzi wa madhehebu mbalimbali, ikipata umaarufu mkubwa visiwani humu.

HISTORIA YAKE
Alizaliwa Juni 15, 1957 huko Uru Kimanganuni, mkoani Kilimanjaro, akiwa mtoto wa nne katika familia ya Gabriel Wariro Andrea na mama Febronia Selemani Joseph.
Nyota yake ya ki-elemu ilianza kung’ara mapema tangu akiwa anapata elimu ya sekondari mwaka 1976, kutokana na imani za kiroho zilizojengeka kwenye moyo wake, aliamua kuwa mtumishi wa Mungu.
Alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho na kupata elimu ya falsafa ya dini kati ya mwaka 1978 – 1979, kabla ya kujiunga Seminari ya Matakatifu Paul huko Kipalala mkoani Tabora.
Alihitimu mafunzo yake ya tauhidi (theology) ambapo mwaka 1983 alirudi jimboni kwake Zanzibar kuendelea na kazi za kiroho.

Alikuwa mchungaji katika Kanisa Katoliki la Zanzibar na mwaka 1984 alirudi masomoni Kipalala na Julai 15, 1984, ilikuwa ni siku muhimu kwake kutokana na kupata daraja na upadri, akifanya kazi zake katika kanisa la Mtakatifu Joseph hapa Zanzibar. Safari yake ya maisha ya utumishi akiwa Padri iliendelea ambapo mwaka 1985, aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rosari huko Kitope, kisha kuhamishiwa kisiwani Pemba 1988 na kufanya kazi katika parokia ya Moyo Safi wa Maria huko Wete.
Pia alifanya kazi katika parokia ya Mtakatifu Anthony wa Padua huko Machui, kabla ya mwaka 1995 kwenda katika Chuo cha Amecia Pastoral na kuhimimu masomo ya kiuchungaji nchini Kenya Tokea mwaka 1997 hadi 2003, alikwenda masomoni Marekani na kutunikiwa Shahada za Uzamili katika mitaala ya elimu na ushauri nasaha.

Baadaye alirejea nyumbani na kuendelea na kazi ya kiroho katika kituo cha Hekima huko Cheju, ambapo mwaka 2006 alihamishiwa katika parokia ya Bikira Maria na Rosari huko Kitope sehemu ambayo mwili wake umewekwa katika maisha ya milele katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Machi Mosi, 2008 alipelekwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph akiwa Paroko na kufanya kazi kubwa ya kusaidia maendeleo ya kanisa na 2009, aliadhimisha jubilee ya fedha ya miaka 25 ya upadri kwa kulitumikia Kanisa Katoliki.

Licha ya kufanya kazi hizo za kiroho katika maisha yake,Padri Mushi amekuwa Mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya jimbo chini ya kanisa hilo visiwani Zanzibar, mlezi wa magereza na jeshi la wananchi.
Pia alikuwa mratibu wa afya wa jimbo, sekta ambayo imepata matumaini makubwa na kuwa tegemeo tangu kuanzisha kwa hospitali ya Machui na kuwa kimbilio la wananchi wanyonge kupata huduma za tiba.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Dk. Augostino Shao, anasema kanisa limempoteza mtu makini, muadilifu, mchapakazi na mpenda maendeleo ya watu wote, akiwa si mbaguzi wa imani na itikadi. Anasema na kukiri kuwa Padri Mushi ameacha pengo lisilozibika haraka, kanisa lake limepoteza mhimili mkuu na kwamba kazi aliyoianzisha itaendelea kuonekana kama mtaalam wa mitaala ya maendeleo ya elimu mbali na kazi za kiroho.

Kabla ya kifo chake Padri Mushi alizungumza nami tukiwa huko Machui, na kunieleza kuwa yeye anaamini kuwa hakuna mtoto asiye na akili, bali anahitaji kuwekewa msingi bora ya kimazingira.
Akanieleza kuwa msingi bora wa maandalizi ni kikwazo kwa watoto wengi kupiga hatua, kuwa watoto wema, vile vile akihimiza mbinu na mapenzi ya malezi kwa watoto kama ni jambo linalohitajika kwa makuzi yao.
Licha ya Kanisa Katoliki kumpoteza Padri Mushi, jamii kwa upande wake imepata hasara na pigo la kuondokewa na mtu aliyekuwa chachu katika mchakato wa maandalizi ya ufunguo wa maendeleo ya elimu. Mungu ampokee na kumlaza mahali pema Padri Evarist Mushi, kwa wema na hisani alizowafanyia waja wake hapa duniani. Amsamehe dhambi zake, amtunze na kumpa hadhi kuu katika maisha mengine mapya huko aliko-Amiin.

HABARI KUTOKA NIPASHE


KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: