“UNIKUMBUKE Babaa unapowazuru
wengine naomba unikumbuke, usinipite Yesu unapowazuru wengine naomba
unikumbuke, unikumbuke babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke…”
Haya ni baadhi ya maneno yaliyomo katika moja ya nyimbo zinazomtambulisha
vyema Mwimbaji wa Nyimbo za Injili, Christina Shusho.
Unikumbuke wimbo uliomuinua sana Shusho
Shusho amefanikiwa kujijengea sifa kwa mashabiki wa nyimbo za Injili ndani na
nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe mzito kwa
jamii, lakini ukiwa katika msingi wa neno la Mungu ambalo analiamini.
Umahiri wake katika kuimba nyimbo za Injili umemuwezesha Shusho kutambulika
vyema na kujinyakulia Tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Shusho alikuwa
kati ya wasanii wa Tanzania waliopata Tuzo za Muziki za Afrika Mashariki na
Kati (EMAS) zilizofanyika Agosti 20, mwaka huu na kushirikisha wasanii
mbalimbali wa kutoka nchi nane za Afrika Mashariki na Kati.
Mwimbaji huyo aliibuka na Tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Nyimbo za Injili
akiingia na wimbo wake Unikumbe na kumshinda mwimbaji mwenzake kutoka
Tanzania Upendo Nkone aliyeingia na wimbo wake Haleluya Usifiwe, Alice
Kamande kutoka Kenya na wimbo wake Upendo na Gaby kutoka Rwanda na wimbo wake
Amahoro.
Akizungumzia Tuzo hiyo, Shusho ambaye ni mama wa watoto watatu anasema ni
heshima kubwa kwa Mungu na kwake hasa kwa kuwa alishindanishwa na wanamuziki
wenye vipaji vikubwa vya uimbaji wa nyimbo za Injili akiwemo mwimbaji
mwenyeji Alice.
“Kidogo nilipata hisia za woga iwapo nitashinda hasa kutokana na ushiriki wa
Alice ambaye ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za Injili, lakini pia shindano
lilifanyika nchini kwao hivyo mashabiki wake nilihisi kuwa ni wengi zaidi,
lakini Mungu ni mwema nikapata mimi hiyo Tuzo hivyo nina kila sababu ya
kumshukuru Mungu,” anasema.
Shusho anasema ushindi huo umemfanya ajisikie kumheshimu na kumnyenyekea
zaidi Mungu kwa kumpeleka kila hatua, lakini pia anaona fahari kuwa watu
ndani na nje ya mipaka ya Tanzania wanatambua kipaji chake na kazi aliyopewa.
“Naona ushindi huu mbali na kumheshimu Mungu zaidi, lakini pia naona nimepewa
jukumu zaidi kwa maana kukitumia kipaji changu nilichopewa kwa kuimba zaidi
ya hapa na kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia uimbaji wa Injili,” anasema.
Nini msingi au chanzo cha uimbaji wake? Shusho anasema msingi wake umeanzia
nyumbani kwa kile alichoeleza kuzaliwa katika familia ya Kikristo ambayo
ilipenda kuomba na kusali. “Mimi nimezaliwa katika familia ya kikristo, kwa
hiyo Jumapili nilikuwa nikihudhuria Shule ya Jumapili (Sunday School) ambapo
watoto tulikuwa tukifundishwa dini, na huko ndipo nilianza kuimba,” anasema.
Anasema alipokuwa akiendelea kukua alijiona kuwa na wito na akaona ajaribu
kuimba mwenyewe na kugundua ana kipaji na wito wa kuimba nyimbo za Injili,
hivyo alianza kutunga nyimbo zake. “Mwaka 2003/2004 niliamua kuingia Studio.
Baada y kupata msukumo hasa 2004 nilitengeneza muziki na kuingia
studio…unajua nilipoamua tu nikaanza kutunga nyimbo zangu, kwa hiyo niliingia
studio na nyimbo zangu mwenyewe,” anasema. Shusho anasema msingi mkubwa wa
nyimbo zake ni neno la Mungu.
”Hata kama nitatoa wimbo kwa ajili ya jamii, lakini lazima msingi wake uanze
na neno la Mungu.” Kwa mujibu wa mwimbaji huyo, mtindo wa nyimbo wake ni
kusifu na kuabudu na kwamba hatungi wimbo kwa msingi wa kumjibu ama
kumshambulia mtu zaidi ya kumsifu Mungu kwa ukuu wake.
“Unajua kuna wengine wanaimba nyimbo za Injili, lakini ukiusikiliza uko
katika hali ya ama kumjibu mtu au kumshambulia mtu baada ya kuapa jambo
fulani. Mimi ni tofauti naimba kumsifu na kumuabudu Mungu,” anasema.
Hadi sasa Shusho ameshatoa Albamu nne ambazo ni Kitu Gani yenye nyimbo nane
iliyotoka mwaka 2004/2005, Unikumbuke yenye nyimbo nane iliyotoka mwaka
2007/2008, Nipe Macho yenye nyimbo 10 na Kwa Kanisa la Kristo yenye nyimbo
nane ambazo amezitoa pamoja mwaka 2010/2011.
Kwa mujibu wa Shusho, albamu ya Unikumbuke ambayo alizindua rasmi Novemba 30,
2008 ndiyo iliyomtambulisha vyema kwa mashabiki wa muziki wa Injili na hadi
sasa ameendelea kufanya vizuri hadi sasa.
Akizungumzia kukua kwa muziki huo anasema muziki wa Injili umekuwa, kwa kile
alichoeleza kuwa zamani kwaya ndio zilikuwa zikijulikana lakini tofauti na
sasa nyimbo za Injili zimepenya na unakuta zikitambulika katika matamasha na
mashindano makubwa ya nyimbo za Injili.
Shusho anasema kuimba kwake nyimbo za Injili kumemuwezesha kupata faida mbalimbali,
lakini kwanza jamii kumtambua na kukifahamu kipaji alichonacho, pili kazi
zake kutambulika na kukubalika, tatu anajiona kutumika vizuri na kwamba
anaamini Mungu anaona anavyofanya vyema kazi yake na nne imemuwezesha
kufahamika ndani na nje. “Mungu amenipa maono na mambo ya mbeleni.
Kwa kweli Mungu amekuwa akinibariki kwa njia moja au nyingine,” anasema.
Kutokana na uimbaji wake wa nyimbo za Injili Shusho anasema ameweza kushiriki
matamasha ya ndani, lakini pia katika nchi za nje ikiwemo Kenya, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Uingereza.
Mbali na Tuzo ya EMAS ambayo ameipata lakini pia anasema ameshawahi kupata Tuzo
nyingine ikiwemo Tuzo ya Meya Cup iliyotolewa nchini Kenya, Tuzo za Muziki wa
Injili (Gospel Music Awards) iliyotolewa hapa nchini ambapo aliibuka mshindi
wa Msanii Bora wa Muziki wa Injili na Tuzo ya Kenya Groove Music Awards
ambapo aliibuka na Tuzo ya Msanii Bora wa Nje.
Akizungumzia mtindo wa muziki wa Injili hivi sasa anasema, “kila mtu amepewa
staili yake ya uimbaji…lakini tunapaswa kukumbuka kila watu wana utamaduni
wao kwa hiyo ni vyema tukaimba kuzingatia mazingira yetu. Mungu angefurahi
zaidi kama Watanzania tutaimba kwa kuzingatia utamaduni wetu…sidhani kama
Mungu asingependa tuimbe kama Wachina, au Wazungu na kadhalika, Mungu atajali
tukiimba kwa namna na kipawa alichotupa.”
Anawashukuru mashabiki wake kwa kile anachosema wamemsaidia kwa ushauri wa
aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpa mapendekezo na kwamba wamemshauri
abakie na staili yake ya kuimba kwa taratibu.
“Kama nilivyosema nyimbo zangu ziko kwa mtindo wa kusifu na kuabudu ndio
maana naimba taratibu na hivyo ni rahisi mtu kusikiliza nyimbo zangu hata
akiwa anasikiliza katika redio wakati anaendesha gari njiani au amerudi
nyumbani anataka kutulia lakini akisikiliza nyimbo za Injili…mimi najiamini
na naamini staili yangu ni njema zaidi na ndio nadhani naimudu,” anasema na
kuongeza lengo lake ni kuliimbia kanisa ambalo litaendelea kuwepo milele.
Mbali na kuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Shusho anasema anapenda kupendeza
na kuonekana maridadi na ndio maana pia anajishughulisha na masuala ya
ubunifu wa mavazi na pia ananunua bidhaa au vitu kutoka nje.
Lakini pia Shusho ni mtangazaji wa kituo cha televisheni SIBUKA na akiendesha
kipindi kinachojulikana kama Gospel Hits.
Hata hivyo anasema lengo lake ni kuanzisha kipindi chake cha televisheni
ambacho anasema atakiita Christina Talk Show na kwamba kitakuwa kikijadili
masuala mbalimbali ya kijamii bila kubagua kabila au dini kwani lengo ni kuisaidia
jamii ya Watanzania.
Mwimbaji huyo ambaye ni mke wa mtu, wamebahatika kupata watoto watatu anasema
amesoma hadi kidato cha nne kisha akasomea masuala ya Teknolojia ya
Mawasiliano (IT) katika Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC),
lakini matarajio yake ni kujiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kupata elimu
zaidi.
“Ndoto yangu Mungu akinisaidia nataka mwakani niingine chuo kikuu na nikitoka
huko niwe Daktari wa Taaluma. Lengo langu ni kusomea Uongozi wa Biashara,
nataka pia kuchukua kozi ya muziki ili kuongeza ujuzi zaidi,” anasema na
kuongeza kuwa anataka kuchukua masuala ya uongozi wa biashara kwa sababu hata
muziki, ubunifu vyote vinahitaji usimamizi.
nipe macho nione zouk la nguvu big up Christina Shusho
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FACEBOOK Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni