Kama wewe ni msomaji wa biblia, utagundua kwamba katika hadithi maarufu
za biblia, na ambazo mahubiri mengi sana yametaja, tangu zama za manabii na
mitume wa zamani hata sasa, ni safari ya wana wa Israel Jangwani.
Pamoja na mambo MAGUMU mengi ya jangwani, hapo ndipo Mungu
ALISEMA uso kwa uso na Musa, na hata wana wa Israel walisikia sauti ya Mungu
kwa masikio ya damu na nyama.
Ni katika kipindi hiki cha kupita Jangwani, ambapo Mungu amesema
na Musa kule mlimani, na kumpa amri 10. Ni kule jangwani ambapo vitabu vya
Torati, ambavyo ni mwongozo wa taifa la Israel hadi leo viliandikiwa kutokana
na mambo ambayo Mungu alizungumza. Kwenye safari za maisha kuna sehemu nyingi
za kujifunza, lakini usikose darasa lako upitapo jangwani.
Je! Umegundua kwamba katika maisha yetu kuna vipindi vya kupita
jangwani? Nyakati ambazo unaona kabisa mambo hayaendi (kifamilia, kazini,
kwenye ndoa, shuleni, nk). Jangwani ni mahali pa kupungukiwa na kiu; Ni mahali
pa kero na misukosuko mingi, lakini, hapo ndipo kuna DARASA zuri la maisha
yako. Hapo jangwani ndipo Mungu atasema na wewe kwa habari ya hatma yako. KOSA
la kuondoka JANGWANI isivyosahihi litakugharimu HATMA ya maisha yako.
Sasa angalia jambo hili. Bwana Yesu alipopelekwa kujaribiwa,
Roho alichagua kumpekeka NYIKANI pia. BWANA Alikaa siku 40 usiku na mchana bila
kula wala kunywa, hapo ni jangwani. Zingatia jambo hili, ukiwa jangwani, ni
mahali ambapo pia utaisikia sauti ya Ibilisi kwa DHAHIRI sana. Kila mara sauti
hii itakuwa ikikutaka KUONDOKA jangwani (to find a comfort zone) kwa namna ya
KUMKOSEA Mungu. Ndio maana Ibilisi alikuja na vitu vingi vya kuvutia, ili
kuondoa USIKIVU wa Yesu kwa Mungu wake (Neno). Kila adui alipotaka kumhamisha
katika KUSUDI la Mungu, Yesu alisema, "imeandikwa"
kisha Alikataa vishawishi vya Adui.
Kukaa katika Neno la Mungu, ndio siri ya ushindi wako upitapo
jangwani. Kumbuka siku zote, jangwa halitadumu siku zote, ni njiani tu, lakini
hapo ndipo utasikia suati ya Mungu pia, Akikwambia mambo mengi ya hatma ya
maisha yako. Hapo ndipo utajifunza mambo na kumsikia Mungu akijibu yale maombi
yako ya siku nyingi. Kaa hapo jangwani usiondoke. Zidi kumkaribia Mungu kwa
KUFUNGA na KUOMBA, kaa jangwani kwa saburi na utulivu kabisa, naam, bila
KUNUNG'UNIKA. Ushindi wako ni mkubwa ukivuka hapo.
Usishangae wakati ukiuwa PEKEYAKO jangwani, ndipo ADUI hukujia
na kukuonesha UZURI wa TUNDA, kama alivyofanya kwa mama yetu Hawa pale kwenye
bustani ya Eden (alipokuwa peke yake). Zingatia jambo hili, kweli tunda lafaa
kwa chakula, kweli tunda linapendeza macho, kweli tunda linavutia sana; lakini
kumbuka hapo unashughulika na HATMA yako. Kweli unaweza KUEPUKA jangwa lako kwa
kufanya mambo mengi ya kukupa AHUENI (kivuli kidogo), lakini jiulize, Je!
Ndivyo Neno la Mungu limekuagiza hivyo? Kama jibu ni HAPANA, jua Adui anataka
KUKATILIA MBALI hatma yako kama alivyofanya kwa mama yetu Hawa.
Utulivu wako JANGWANi utakusaidia kusikia SAUTI ya Mungu kwa
namna ambavyo hujawahi kusikia ukiwa katika madarasa mengine. Darasa la jangwani
ni la muhimu; tulia hapo usiondoke hadi utakapopita, maana, hapo sio mahali pa
kudumu sana japo kuna maumivu mengi. Vumilia tena kidogo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.