Kuna
mambo kadhaa ya kukumbuka UPITAPO jangwani:
1.
Ni marufuku kuchoka/kukata tamaa/ kuzimia roho.
Kuchoka ni kikwazo cha mavuno yako.
“9 Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati
wake, tusipozimia roho” (Wagalatia 6:9).
Nikiangalia katika
Wagalatia 6:9, naona kwamba kuna uwezekano wa kupanda mbegu, yamkini na
kupalilia, hata kunyeshea, lakini KUSUBIRI kwa muda mrefu, katika hali ngumu
(jangwani), inaweza kuleta hali ya KUKATA TAMAA/KUCHOKA/KUZIMIA MOYO, ambayo
hali hii inazimisha UWEZO wako wa kuvuna (kupata majibu ya maombi yako au
kupata matarajio yako kule ng’ambo ya jagwa).
2.
Manun’guniko
ni kivutio cha adhabu badala ya msaada.
“5Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha
huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana
maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. 6BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu
wengi wakafa. 7Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu
tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa.
Basi Musa akawaombea watu” (Hesabu 21:5-7)
Angalia
maneno yako unapopita jangwani. Mara nyingi ni rahisi kunung’unika kwa sababu
ya adha mbaliambalia unazopitia. Utakuta mtu anaanza tu kusema, “kwa hali hii,
mi naona maisha ya wokovu ni magumu sana”, “aheri hata ndoa za wamataifa, naona
yangu ni mateso tu”, “yaani pamoja na kumtumikia Mungu bado nateseka kuliko
watenda dhambi”, “sasa unafikiri mtu ataishije namna hii?”, “hata Mungu anaona
kwamba nimevumilia muda mrefu”, n.k. Haya ni maneno ya mtu aliyechoka na
yamkini sasa anajifariji wakati anatafuta namna ya “kuchepuka” apitapo
jangwani.
3.
Kanuni
za kula manna; kila chakula (Neno) huja kwa wakati na kusudi maalumu
kukufundisha. Elimu ya jangwani ni muhimu kwa maisha ya Kaanani.
“35 Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa
miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata
walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani” (Kutoka 16:35).
Ukiwa
jangwani, bado Mungu atakuletea “chakula cha siku”, hadi uvuke hapo. Kumbuka,
manna ilikuwa “chakula cha kuokota”, wana wa Israel hawakutafuta, kazi yao
ilikuwa ni kuokota tu, tena kwa KANUNI maalumu. Kila siku ilimpasa mtu
kukusanya chakula cha siku moja, na siku ya 6 walikusanya chakula cha siku
mbili, kwa sababu siku ya Sabato hawakutakiwa kufanya chochote ila kupumzika.
Kumbuka,
siku 6 walikusanya chakula cha siku moja (hapakuwa na kiporo), na aliyekusanya
zaidi, ile manna iliharibika! Angalia jambo hili, siku ya Sabato manna hiyo
hiyo iliweza kudumu siku 2 bila kuharibika! Na, kwenye Sanduku la Agano ipo manna
nyingine hata leo haijaharibika, imefichwa hadi kwenye ufalme ujao; watakaoshinda
watapewa huko Mbinguni (Ufunuo 2:17).
Uwe
makini na chakula (NENO) Mungu analosema nawe ukiwa jangwani. Huja kwa wakati
maalumu na kwa kusudi maalumu, hilo Neno ndilo litakuvusha kwenye jangwa lako
salama. Hilo Neno haliji holela, linakuja kwa namna maalumu kwa ajili yako.
Omba sikio la “kusikilia” ili usikie litamkwapo.
4.
Ukimwangalia
nyoka wa shaba utapona; Msaada wako unatoka katika Bwana. Yeye aliyakupitisha
hapo jangwani anaDAWA ya kila shida yako.
“8Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya
shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo
ataishi. 9Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa
nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi” (Hesabu
21:8,9).
Pamoja
na majanga yote ya jagwani, Mungu hufanya “njia ya kutokea”, na msaada ambao
imekupasa KUUJUA na KUTII ili weze KUPONA. Watu wengi waliofia jangwani ni kwa
sababu ya kukosa UTII. Kumbuka siku zote, kama yuko NYOKA WA SHABA, kuumwa na
NYOKA sio tatizo, dawa ipo. Watu wengi wamekatishwa tamaa kwa sababu katika
kupita kwao jagwani wamemkosea Mungu (wakaumwa na nyoka za moto), na wemehukumiwa
na wanadamu kwamba kwasababu wamemkosea Mungu wataangabia bila shaka! Hivyo,
hawakuona sababu tena ya kuinua macho yao na kumwangalia ‘nyoka wa shaba’ ili
wapone. Sikiliza, Inua macho yako sasa, angalia juu, Kristo anakuona ulipo,
liitie jina lake UTAOKOKA na KUPONYWA kwa maana “kila aliitiaye jina la BWANA
ataokoka”.
Yesu
hatishwi na dhambi zako, wala hakuchukii wewe kwa sababu ya hayo makosa yako
unayohukumiwa nayo; Amekuja kwa ajili ya mtu kama wewe, yaani “amekuja kwa
walioDHAIFU wanaohitaji TABIBU”.
5.
Urefu
wa jangwa unakutegemea wewe na sio Mungu. Kadri UNAVYOJIFUNZA mapema na KUTII
ndivyo utafupisha urefu wa njia yako jangwani.
Wakati
wana wa Israel walipotoka Misri, kulikuwa na njia fupi ya kufika Kaanani, ila
kulikuwa na maadui, hivyo Mungu akawaepusha na vita kwa kuwapitisha MBALI. Sasa
ona mambo mawili: Kwanza, Iliwapasa wazunguke umbali mrefu kwa sababu ya HALI
yao wenyewe, kwa maana wangepitia VITA mapema, wengi wangekatishwa tamaa kwa
sababu aidha HAWAJUI kupigana vita (maana kule Misri hawakujifunza vita ila
kazi za ujenzi, na utumishi) au HAWAKUWA tayari kupigana; Njia yao ikawa ndefu.
Pili, Baada ya kumkasirisha Mungu, wakiwa karibu kabisa na kuvuka Yordan,
waliambiwa “wageuke” kurudi tena nyuma kuelekea jangwani. Hawakuwa tayari
kuvukia ile AHADI kwa sababu ya uhaba wa IMANI yao, baada ya Mungu kusema nao
kwa namna nyingi [Soma Hesabu mlango wa 13 na 14]. Hapa tena ni wao wenyewe!
Angalia
hapa, “24 lakini mtumishi wangu
Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo
wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo
aliyoingia; na uzao wake wataimiliki. 25Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende
jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu” (Hesabu 14:24). Hawa watu
walifika karibu kabisa na nchi ya ahadi, pale ambapo Musa alimtuma Kaleb na
wale wengine 11 ili kuipeleleza nchi, na walitumia siku 40 tu kwenda Kaanani na
kurudi. Inamaana baada ya miaka 40 jangwani, walibakiza siku hata hazifiki 40
ili kumaliza safari yao, na kuirithi ile AHADI, wakamkorofisha tena Mungu.
Wakageukia jangwa kwa upya! Kwa sababu IMANI yao ilitindika, na kuna MAADUI
bado! Ila walibakiza kidogo tu wamalize jangwa. Wakashindwa mahali pa kumalizia!
Angalia vita uliyonayo sasa,
umepigana vingi, usichoke sasa, hata hii nayo utashinda tu. Simama, utamwona
Mungu, jangwa sio la milele, ni njia tu, utavuka.
6.
Nguvu
za kuvuka Yordan zinatoka kwa Mungu pia; Usikorofishane na Mungu, hutafika
Kaanani, kwa maana bila yeye huna nguvu za kuvuka Yordan.
Kumbuka,
Kutoka Misri palihitajika MUUJIZA wa kuvuka bahari ya SHAMU, na baada ya
jangwa, palihitajika muujiza mwingine wa kuvuka YORDAN ili kuingia Kaanan.
Ukikorofishana na Mungu, hata ukikimbilia kwa njia zako hadi ukingoni (ufukweni)
mwa Yordan, utavukaje mto? Bado utagundua kwamba unamhitaji tena Mungu. Kuwa
mtulivu jangwani. Mwombe Mungu akupe neema ya kutulia kabisa na kuchukua shule
zake zote na KUKUA kiIMANI ili ukivuka hapo uingie hatua zingine za Baraka na
kufanikiwa.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.