Jumatano, 20 Januari 2016

UZINDUZI WA BWENI JIPYA LA WANAUME KATIKA CHUO CHA TAG DODOMA.



Idara ya Elimu ya kanisa la Tanzania Assemblies of God linatekeleza mpango wa maboresho wa vyuo vyake vya Biblia nchi nzima. Mwezi Januari Mwaka 2016, jengo jipya lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wanaume zaidi ya 200 katika chuo cha Biblia cha Central Bible College (CBC) Dodoma lilizinduliwa katika hafla iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God Rev. Dr. Barnabas Mtokambali. Mradi huu umefadhiliwa kwa ubia baina ya "Priority One"kutoka Marekani na Idara ya Elimu ya TAG.



Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni Rasmi Dr. Sam Johnson kutoka Marekani ambaye pia ndiye mfadhili mkuu wa mradi huo alisema mradi huo ni utekelezaji wa Agizo Kuu la Bwana Yesu la kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Yesu. Dr. Johnson alisema chuo cha CBC kitawavutia watumishi wengi kuja kunolewa na kupata elimu ya theolojia ili waje kuwa watumishi wazuri zaidi, kwa kupata Stashahada, Shahada, na Shahada za Uzamili na Uzamivu. Aliongeza kwamba anaamini kwamba CBC itakuwa kitovu cha umahiri katika elimu ya theolojia hapa Tanzania na nje ya Tanzania.



Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God, Rev. DR. Mtokambali alisema anapolitazama jengo hili na aliposikia historia yake kutoka kwa Mkurugenzi wa Elimu, anaona mbali zaidi ya mamilioni ya shillingi yaliyotumika. Alisema anaona mamilioni ya roho za watanzania na wasio watanzania zikiokolewa kupitia elimu itakayotolewa katika chuo hiki. Alisema katika Mpango Mkakati tumefanya kazi nzuri miaka saba iliyopita na kwamba miaka mitatu iliyobaki ni ya kufanya kazi ya kufa na kupona ili tuivune Tanzania kwa ajili ya Yesu.



Askofu mkuu alimshukuru Dr. Sam Johnson na "Priority One" kwa ukarimu wao wa utoaji, Mkurugenzi wa Elimu Rev. Jonas Mkoba kwa kujitoa kwakwe kusimamia mradi huu, na kila mtu aliyeshiriki kwa njia moja au nyingine kuukamilisha mradi huu.






















KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: