Jumapili, 17 Januari 2016

UMEPIGA MISHALE MINGAPI?


4 Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake! 15Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale. 16Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme. 17Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza. 18Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha. 19Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu” (2 Wafalme 13:14-19).

Katika tafakuri la mistari hii ya 2 Wafalme 13:18, 19, nimejiuliza maswali mawili makubwa: kwanini nabii Elisha alikasirika mfalme Yehoashi alipopiga mishale mitatu tu? Na, mfalme Yehoashi angejuaje kama anapaswa kupiga mishale mara tano au sita kama hakuambiwa?

Hii ni vita ya kiroho ambayo mfalme Yehoashi ameanza dhidi ya adui zake Waashuri. Ukienda kwa watumishi wa Mungu juu ya shida yako, au ukianza maombi kwa ajili ya shida fulani, hapo tunasema umeanza vita kwa namna ya rohoni. Kumbuka, Yehoashi anajua uadui kati yake na Washami, anajua kwamba baada ya muda kutakuwa na vita halisi kwa jinsi ya mwilini au vita ipo, sasa ameamua kwenda kutafuta msaada wa kiroho kwa mtumishi wa Mungu nabii Elisha.

Sasa angalia, kiwango na jinsi anavyofanya mambo katika ulimwengu wa roho (maombi) kinaonesha kiwango cha hasira au nia ya kushinda aliyonayo mtu dhidi ya jambo linalomsumbua. Kwa mfano, “Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. 17Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake” (Yakobo 5:16b-18).

Ninachoona hapa, wakati Elisha amemwambia Yehoashi, “piga mishale”, Elisha alitarajia kuona kiwango fulani cha kupambana katika ulimwengu wa roho ambacho kinaonesha “hasira au nia” ya ushindi dhidi ya adui. Yehoiashi akapiga mishale mitatu tu, Elisha akakasirika! Fikiri Mungu anataka uombe, ila kwa bidii! Sawa, unahaki wewe, bidii ipo? Je! Unabidii?

Ukitaka kuona jambo hili angalia tena hapa mfano wa BWANA Yesu, “1 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. 2Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. 3Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 4Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, 5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. 6Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. 7Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 8Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” (Luka 18:1-8). Kilichomfanya mjane huyu apate anachotaka sio HAKI yake ila BIDII yake! Kwa sababu huyu Kadhi ni dhalimu, huwa hajali haki za watu, ila bidii ya huyu mama ikamtoa jasho. Huyu mjane angeenda mata tatu tu, asingeweza kuvuka katika shida yake, ila alienda mara nyingi.

Sasa utajuaje kwamba mara ngapi (kiasi cha maombi) inatosha?  Kuna namna tatu tu: kwanza, kama jambo unaloomba limetokea (umepata majibu ya maombi yako); pili, Mungu amekwambia “acha kuomba juu ya hilo jambo”; na tatu,  unasikia wepesi fulani hivi na hali ya kuvuka (upenyo) ndani ya nafsi yako wakati ukiomba juu ya hilo jambo [hii ni ngumu kueleza maana inatambulikana kwa uzoefu].

Kumbuka siku zote, endelea kupiga mishalie (maombi) hadi upenyo utakapopatikana katika ulimwengu wa roho; omba bila kukoma. Hiyo ni ishara kwamba kuna ushindi wakati utakapofika wa kufanya vita vyako kwa jinsi ya mwili. Jambo jingine, nguvu na bidii unayoweka na kung’ang’ania (kutokukata tama) ni muhimu sana ili kuweza kupokea ushindi wa vita unavyopigana. Usiwe mlegevu katika ulimwengu wa roho, hakikisha unafurukuta kwa nguvu zako zote na kwa bidii, tena kwa MUDA mrefu. Acha kuomba kama unaombe chakula, jifunze kutofautisha uzito wa mambo na bidii zake katika maombi, hivyo ndivyo utavuka siku zote kwa ushindi.
 
Frank P. Seth

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: