"Your life style affects you more than your prayers"
"21 Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia. 22
Uyapokee, tafadhali, mafunzo yatokayo kinywani mwake, Na maneno yake yaweke
moyoni mwako. 23Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa; Ukiuondoa udhalimu mbali na hema
yako. 24Nawe hazina zako ziweke mchangani, Na dhahabu ya Ofiri iweke kati ya
mawe ya vijito; 25Naye Mwenyezi atakuwa hazina yako, Atakuwa ni fedha ya
thamani kwako. 26Kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, Na kuinua uso
wako kumwelekea Mungu. 27Utamwomba yeye naye atakusikia; Nawe utazitimiliza
nadhiri zako. 28 Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga
utaziangazia njia zako. 29Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena;
Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa. 30Atamwokoa na huyo asiye na hatia; Naam,
utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako." (Ayubu 22:21-30)
Katika maombi kuna nguvu na ushindi.
Maombi ni silaha, njia ya kupata mahitaji yetu na kuinuliwa, lakini MAOMBI yetu
hayana maana kama TUNAISHI (enenda), yaani kuwaza, kunena na kutenda KINYUME na
tuombavyo! kwa maana imeandikwa “imani
bila matendo haizai” (Yakobo 2:20).
Angalia hapa, watu wengi wanadhani
WANAFANIKIWA sana kwa sababu wameomba! Sawa, hiyo ni sehemu tu, lakini
nakwambia leo, ukichunguza maandiko yanazungumzia habari ya utaua, kumcha
Mungu, kumjua Mungu, kumpenda Mungu, mtu mwema, nk. Maombi ni muhimu na LAZIMA,
ila maombi bila matendo yako ni sawa na kujaza maji kwenye gunia, halitajaa kamwe.
Je! waweza kuomba ukafanikiwa pasipo imani? na je! unaweza kusema una imani
pasipo matendo (mwenendo wa imani)?
Mmoja atasema, "maombi ni jambo la
kwanza kabla ya matendo", nami nasema, "huwezi kutenganisha maombi na
matendo, ila cha kwanza ni matendo yako". Ndipo Yakobo akasema, “nioneshe imani yako kwa pasipo matendo nami
nitakuonesha kwa matendo” (Yakobo 2: 18), Je! Atendaye kwa sababu anaamini
si mkuu kuliko aombaye bila kutenda? Angalia
tena, kinachokuathiri zaidi ni mwenendo wako au maombi yako?
Ukiangalia katika Ayubu 22:21-30 utaona
msisitizo wa maisha (lifestyle) na KIU ya ndani ya kumjua Mungu SANA, ndipo
mema yatakapokujilia. Ukizidi kusoma utaona habari ya KUJENGWA kama utamrudia
Mwokozi. Je! utajuaje kama haya yamo ndani yako? Dalili ya kwanza, angalia
kiwango chako cha maombi? Jiulize, wewe ni mwombaji? Imekupasa kuomba angalau
mara kadhaa kila siku na angalau kwa dakika chache, au unakumbuka kuomba wakati
wa chakula na kulala, au ukibanwa na shida tu? Pili, angalia kiwango chako cha
kusoma Neno. Ukiona unasahau kusoma neno hadi wiki inapita, jua ile HAMU ya “kumjua Mungu sana” haipo. Tatu, je! kuna
uhusiano wa IMANI yako na maisha ya KILA SIKU? Yaani katika biashara, shule, na
mambo ufanyayo, je! iko hofu ya Mungu? kwa lugha nyingine, je! kuna mambo
huwezi kufanya kazini kwako kwa sababu tu unamcha Mungu? Je! kwa maisha yako tu
bila kusema neno na kushuhudia, watu watajua kwamba umeokoka? Je! yupo
atakayevutwa kwa BWANA au KUMSHUKURU Mungu kwa ajili ya matendo yako? Je! wajua
kwamba Injili ni mfumo wa maisha na wala sio kuhubiri tu?
Sasa ufanyeje kama umepungua katika
hayo? Kwanza, Toba ya kweli, Pili, Omba BWANA akurudishe tena katika njia zake,
soma neno na litafakari kila siku, mchana na usiku. Anza kufanya yakupasayo
(mwenendo wa Kitaua), hapo utaona faida kubwa.
Frank Philip Seth.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni