Na Douglas Majwala
K
|
atika
makala hii ya mafundisho ninawaletea hoja ngumu nzito zenye kuhitaji tafakuri,
utulivu na umakini wa kutosha kuelewa mgogoro huu mkongwe duniani wenye mwanzo
lakini unaonekana hauna mwisho, lakini wenye asili yake katika Agano la
Kimbingu. Mimi binafsi nimelazimika kufanya maombi kabla ya kuanza kuandaa
makala hii ya mafundisho; jambo ambalo ni nadra katika uandishi. Nikusihi na
wewe mpenzi msomaji sasa utwae shajala zako [stationery] kama kalamu na note
book au daftari lako na Biblia yako pia unapoanza kusoma mafundisho haya ambayo
wengi wanayaonea aibu au hawana ujasiri wa kuyafunua wazi kwa umma ijapo
wanafahamu ukweli wake katika maandiko, labda kwa kuogopa gharama za mahusiano
na upande wa pili wa imani.
Lakini ajabu ni kwamba licha ya Biblia kuwa wazi kuhusu nani ni mmiliki
halali wa maeneo husika hasa Yerusalemu lakini ni mara chache sana au hakuna
kabisa maandiko haya kufundishwa au kuhubiriwa madhabahuni. Mimi mwenyewe
ninakiri kuwa toka tumboni mwa mama yangu sijawahi kusikia habari hii
iliyoandikwa kwenye Biblia ikihubiriwa au ikifundishwa kwenye madhabahu za
Kanisani, semina na mikutano ya Injili. Katika kuandika makala hii, ninafanya
hivi nikijuwa pia kuwa ninajitoa muhanga kufikisha ujumbe huu mahsusi kabisa wa
mgogoro ambao umegharimu amani ya dunia, umegharimu amani ya Kanisa la MUNGU
alilolinunua kwa damu yake mwenyewe Mdo.20:28, umegharimu rasilimali za dunia
katika kuandaa mikutano ya kuuongelea na zaidi umegharimu roho za wahanga wa
pande mbili husika.
Madai ya Wayahudi juu ya
ardhi hii yanaegemezwa kwenye ahadi ya Kibiblia kwa Ibrahimu na kizazi chake,
juu ya ukweli kwamba ardhi hii ilikuwa ni alama ya kihistoria ya falme za
zamani za Kiyahudi za Israel na Yudea, na juu ya uhitaji wa Wayahudi kupata
hifadhi salama dhidi ya Wakoloni wa Ulaya waliopingana na mila na desturi zao.
Waarabu wa Kipalestina wanaegemeza madai yao kwenye kuendelea kuishi katika ardhi
hiyo kwa maelfu ya miaka na ukweli kwamba waliwakilisha idadi kubwa ya watu
hadi mwaka wa 1948. Wanakataa madai kuwa kuwepo ufalme wa nyakati za Kibilia
hakuhalalishi madai ya nyakati za leo. Kama Waarabu wakihusisha madai ya
Kibiblia, wanasisitiza kuwa madhali mtoto wa Ibrahimu aitwaye Ishmail ni baba
mwanzilishi wa Waarabu, basi ahadi ya MUNGU ya kumilikisha ardhi hiyo kwa
watoto wa Ibrahimu inaunganisha pia Waarabu kwa sababu Ishmail ambaye ni baba
mwanzilishi wa Waarabu ni mtoto wa Ibrahimu huyo ambaye MUNGU anamilikisha
ardhi hiyo kwa watoto wake. Hawaamini kwamba wanastahili kuachia ardhi yao kuwa
fidia kwa Wayahudi kwa uhalifu uliotendwa na Wakoloni wa Ulaya kwa Wayahudi.
Naomba niweke wazi kuwa sitaongelea mikataba ya kisiasa kama ya Camp
David, Roadmap and the Quartet,
The United Nations Partition Plan ya Novemba 29, 1947 iliyogawa
Wapalestina katika dola mbili za Wayahudi wa Palestina na Waarabu wa Palestina,
wala sitaongelea vita ile ya mwaka 1949 baina ya Israel na dola za kiarabu
vilivyoishia kuingia mkataba wa kuigawa Palestina katika dola tatu wakapewa
Israel, Misri na Jordan; dola la Kiarabu la Palestina halikutambuliwa na
mkataba wa mgawanyo huu wa UN; mkataba tata uliozaa vita vya 1947–1949 na kuzaa
wakimbizi wa Kipalestina wapatao 700,000 waliokimbilia Israel ambapo Israel
iliwabakisha Wapalestina 150,000 wenye asili ya Kiarabu na kuwafanya kuwa raia
wa Israel na Israel ikawapa uraia wa daraja la pili na kuwekwa chini ya utawala
na udhibiti wa kijeshi huku wakikosa haki za msingi kabisa kama raia na hawa
ndiyo walikuja kuzaa kikundi cha Hamas ambao kwa kitendo cha kuwekwa chini ya
mamlaka na udhibiti wa jeshi la Israel, walipata mianya ya maarifa ya kivita na
Israel haikupata maono kuwa hawa siku moja watarudi na kuigeuka Israel kama
tunavyoona sasa Hamas ikiongoza Palestina baada ya kurudi huko kwao kufuatia
mikataba ya kisiasa isiyo na tija kutoa fursa ya kubadilishana wakimbizi ambao
wengine wao kama hawa, walijikuta Israel kufuatia mgawanyo wa eneo
lililogombewa kwa njia ya vita mwaka1947–1949.
Wala sitaongelea vita ya Juni
1967, pia sitaongelea azimio namba 242 la baraza la usalama la UN, ambalo pia ni azimio tata kwa sababu
lilitoa agizo kwa Israel kuachia maeneo iliyoyateka katika vita hiyo na kutoa
haki kwa dola zote zinazohusika na eneo hilo. Hili ni azimio
tata kwa sababu tafsiri yake katika lugha ya Kifaransa inasema Israel inapaswa kuondoka katika maeneo hayo
huku tafsiri ya lugha ya Kiingereza ikitoa mwito
wa kuondoka kwenye maeneo hayo [Kifaransa na Kiingereza zote ni lugha rasmi
za UN].
Israel na Marekani zinatumia
tafsiri ya Kiingereza kubisha kuwa Israel iondoke kwenye baadhi tu ya maeneo
lakini siyo maeneo yote ili kukidhi matakwa ya azmio hilo. Kwa miaka mingi
Palestina iliendelea kukataa azimio hilo kwa kuwa halitambui uwepo wa utaifa wa
Palestina na wakataka wakimbizi kupewa makazi ya haki ambako hawatasumbuliwa
lakini zaidi kuwa azimio hilo lililotaka utambuzi wa kila dola katika eneo
husika, linatoa mwito kwa Palestina kutambua Israel bila Israel kutambua haki
za kitaifa za Palestina. Sitaongelea pia The October 1973 War and the Role of Egypt, wala sitaongelea mikataba ya
Oslo, sitaongelea The 2002 Arab Peace Plan, sitaongela
pia Palestinian Statehood and the UN.
Ifahamike kwamba mikataba hiyo yote haijazaa matunda tarajali. Makatibu
Wakuu wote wa UN wamekuta mgogoro, wamejaribu kuutanzua na wakastaafu wakauacha
ungali mbichi. Katika kutambua yote yaliyojiri kwenye
mgogoro huu ambao mimi binafsi nimekuja duniani nikaukuta uliishakuwepo kwa
miongo mingi, naomba nitoe azimio la kuwa na maslahi [declaration of interest] na
upande wa Israel kwa sababu za ushahidi wa maandiko ya kitabu kitakatifu cha
Biblia, na pia nikizingatia ukweli kuwa siwezi kutangua Agano la MUNGU
aliloliweka na taifa lake la Israel [ambalo hata YESU mwenyewe hakulitangua],
lakini zaidi nikiheshimu agizo la MUNGU la baraka na laana juu ya mtu awaye
yote atakayeibariki au kuilaani Israel.
Lakini ni budi watu wote wakafahamu kuwa asilima
kubwa ya usuluhishi wa kesi/migogoro chini ya jua huwa kanuni inayotumika siyo ya
kutoa haki sawa kwa pande zote [Win-win situation badala yake ni kanuni ya Zero-sum
ndiyo inatumika]. Ni Mbinguni tu ndiko kuna kanuni ya Win-win lakini chini ya
jua kanuni ni Zero-sum kwa asilimia kubwa ya migogoro, na kwa hiyo napata
ujasiri wa kusema kuwa suala la Mashariki ya Kati kanuni ya utatuzi wake lazima
iwe ni Zero-sum ambapo mmoja akose na mmoja apate. Vinginevyo dunia itaendelea
kushuhudia mashindano ya silaha na mbinu za kivita katika uwanja wa mapambano
huku vikao vya kimataifa vya meza za duara vikiendela kupamba vyombo vya habari
kwa ripoti za maazimio yanayoendeleza tu uhasama.
Ni
bahati mbaya kuwa historia ya eneo linalogombewa haiainishwi wazi wazi
[inafichwafichwa tu] kwa sababu ambazo nafikiri ama ni za uoga tu au ni za
maslahi vikundi na hii inazidi kurefusha mgogoro huu. Nitajitahidi kudurusu
historia kwa ushahidi wa maandiko. Ni katika mkondo huu wa uelewa [school of
thought] wa muktadha wa jambo hili, kwamba tutaweza kubashiri mustakabali na
hatima yake.
Lakini ili kujuwa kuwa maeneo
yanayogombewa [Ukanda wa gaza, Yerusalemu na Ukanda wa Magharibi wa mto Yordani
ambayo yote haya yako kwenye nchi ya ahadi ya Kibiblia ya Kaanani ambayo ndiyo Israel ya leo, ambapo waliishi watoto
wa Kaanani Mwa.10:15-18 ambao ni Sidoni, Hethi, Myebusi, Mwamori, Mgirgashi,
Mhivi, Mwarki, Msini, Mwarvadi, Msemari, Mhamathi] na mpaka wa Wakanani ulianza
kutoka Sidoni kwa njia ya Gerari hata Gaza Mwa.10:19. Kwanza ni budi tujuwe
Kaanani ni nani? Mwa.10:1,6 inadhihirisha kuwa Kaanani ni mjukuu wa Nuhu
kupitia mtoto wa Nuhu aitwaye Hamu. Hapo pia utagundua siri ya ajabu sana kuwa
hata Misri ni jamaa katika ukoo wa Nuhu [sasa ardhi ya Misri nayo kwa mujibu wa
Biblia ni ya Waisraeli, kwa maana hata Ishmail ni mtoto wa Ibrahimu kupitia kwa
mjakazi Hajiri Mmisri, kwa hiyo Ibrahim alimposa Hajiri ambaye anatoka katika
ukoo wa Nuhu kupitia kwa mtoto wa Nuhu aliyeitwa Hamu ambaye tumeona ni baba wa
Kaanani]. Kwa mujibu wa mafungamano ya koo hizi za Kaanani ni dhahiri kuwa
Mpalestina [ambaye ana mafungamano makubwa ya kisiasa, kidini na mila/utamaduni
na nchi ya Misri ni Mmisri pia kupitia uarabu wao, Misri ndiyo chimbuko la
uarabu] kwa vigezo hivyo ndani ya mabano anatoka katika ukoo mmoja na mzee
Kaanani na katika ardhi moja ya Kaanani [ambako ndiko Israel ya leo pia, ambayo
ndiyo nchi ya maziwa na asali na nchi ya ahadi, nchi ya Agano] kwa maana kwa
mujibu wa Mwa.10:6, Misri na Kaanani ni watoto wa Hamu na ni wajukuu wa Nuhu.
Mvutano uliopo unatokana na ukweli kwamba
hizi koo zilikuja kutawanyika Mwa.10:18,32 wengine baada ya gharika na ule
msitari wa 31 unasema kuwa hata Shemu ambaye ni ndugu yake Kaanan kwa Nuhu,
walikuja kugawanyika katika lugha zao, katika nchi [ardhi] zao na wakafuata
mataifa yao. Sasa MUNGU anapotoa ahadi kuwa nchi yao anawapa Wayahudi/Waisrael;
wanakuwa hawaelewi lugha anayoongea MUNGU ambaye ndiye mwenye ardhi hiyo kwa
sababu yeye ndiye aliyeiumba kwa mikono na utashi wake, na vitu vyote ni vya
kwake Zab.24:1na sawa na mzazi anapogawa urithi kwa watoto huwa hakuna
anayeweza kumpangia kinyume na matakwa yake maana ardhi ni yake na watoto ni
wake pia, na sababu kubwa ya wao kutoelewa lugha na iliyofanya nchi yao wapewe
Wayahudi/Waisraeli ni kuwa walijiingiza kuabudu miungu wakamwacha MUNGU wa
Israel ambaye ndiye MUNGU wa kweli, na MUNGU wa Israel mwenye wivu alipoona
miungu inaabudiwa; alijitenga nao na alipojitenga nao ile nguvu ya MUNGU iliyokuwa ndani yao wakati anawapa
hiyo nchi [kabla hawajageukia miungu] ilihama ikaenda kwa Wayahudi/Waisrael na
kutoa mwanya kwa Wakaanan, Sidoni, Hethi, Myebusi, Mwamori, Mgirgashi, Mhivi,
Mwarki, Msini, Mwarvadi, Msemari, Mhamathi kuwa wadhaifu kwa kiwango cha
kutomudu vita iliyoweka Kaanan katika milki ya Waisrael na ndiyo maana hata leo
Palestina ambaye ametoka katika ukoo dhaifu uliopungukiwa na nguvu za MUNGU
kutokana na uasi wa kugeukia miungu ameendelea kukosa nguvu na ushindi kila
vita vinapoibuka dhidi yake na Israel ambaye nguvu za MUNGU zilihamia kwake.
Mgogoro kati ya Waarabu wa
Kipalestina na Wazayoni [Israeli] ulianza kama mapambano kuhusu ardhi. Kuanzia
mwisho wa vita kuu ya pili ya dunia hadi mwaka 1948, eneo ambalo makundi yote mawili
yalidai milki yake yalijulikana kimataifa kama Palestina. Jina hilo moja pia
lilitumiwa kuelezea eneo ambalo halikutambulika sana “Ardhi Takatifu” na dini
tatu za monotheistic [Mungu mmoja]. Kufuatia vita ya mwaka 1948–1949, ardhi hii
iligawanywa katika maeneo matatu: dola la Israel, Ukingo wa Magharibi [wa mto
Yordani] na Ukanda wa Gaza. Ni eneo dogo la wastani wa maili za mraba 10,000 au
takriban ukubwa wa jimbo la Maryland nchini Marekani, kwa
mujibu wa
Middle East Research and Information Project ya
Washington DC.
Ebu tafakari juu ya miujiza ambayo Israel
inapata inapokwenda vitani huwa inatokana na uwezo wa kibinadamu kweli au uwezo
wa MUNGU? Dunia inapaswa kujiuliza kuwa iweje kila vita vikilipuka hata ambavyo
dunia nzima ya Waarabu wakiungana pamoja lazima Israel ishinde? Iweje Israel
inapomaliza vita huwa haitetereki kiuchumi? Iweje mataifa makubwa duniani
yanaogopa kuitenga Israel? Iweje Israel imudu kupiga hatua ya kimaendeleo na
usalama hata pale ambapo inawekewa vikwazo vya kiuchumi na jumuiya za kimataifa
na kubaki kama kisiwa? Iweje Marekani dola kubwa duniani ni mwepesi kuliwekea
taifa lolote duniani vikwazo ikiwemo Urusi hata bila kupitia UN wakati fulani,
lakini Marekani hiyo hiyo haithubutu kuiwekea Israel vikwazo ila itaiachia UN
ifanye hivyo?
Itaendelea
ambapo nitadurusu maandiko kadhaa yanayoonyesha jinsi MUNGU anavyotamka
waziwazi kuwa ardhi hiyo inayogombewa amewapa Waisrael na kwamba maadui
zake [Waarabu] hawana chao katika eneo hilo. Tena zaidi nitawapeleka
kuona jinsi MUNGU anavyoagiza Israel kuwashughulikia kwa kulipiza maadui
zake hao wanapomshambulia, hapa MUNGU anatumia lugha kali kabisa isiyo
na huruma hata kidogo, na kwa vile ni maandiko ambayo lazima yatimie,
ndiyo maana tunaona Israel ikishambulia maadui zake kwa viwango vya kutisha kabisa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni