Jumatano, 17 Desemba 2014

SOMO LA PIMA KIWANGO CHAKO KUTOKA KWA FRANK PHILIP


 
Katika mwaka wa ishirini na saba wa Yeroboamu mfalme wa Israeli Uzia mwana wa Amazia mfalme wa Yuda akaanza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia. Ila mahali pa juu hapakuondolewa, nao watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. BWANA akampiga mfalme, akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee. Na Yothamu mwana wa mfalme alikuwa juu ya nyumba, akiwahukumu watu wa nchi” (2 Wafalme 15:1-5).
 
                                          
Yuko mmoja ambaye ni kiwango cha kupima hatua zako, naam wapo wawili: Daudi mwana wa Yese (3 Fal. 14:3) na Yeroboamu mwana wa Nebati (2 Fal. 13:2). Daudi kwa sababu ya wema wake, na Yeroboamu kwa sababu ya uovu wake, hasa ibada ya sanamu. Daudi alimpenda Mungu na BWANA alimwita “MWEMA” (1 Samweli 15:28). Yeroboamu aliwakosesha wana wa Israel kwa kutengeneza sanamu na kuwafanya waabudu sanamu na kusema, “tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri” (1 Fal. 12:28).
 
Nimesoma habari za wafalme wa Israel, nikaona kuna mahali pa kujipima, nami sasa nakupa habari hii ili upate kujua kwamba papo mahali pa kuangalia na kujua mwenendo wako. Katika zama za Agano Jipya, Mtume Paulo akasema “nifuateni mimi kama ninavyomfuata Kristo”, Naam, hapo zamani, wafalme wa Israel walipimwa kwa waliowatangulia pia. Walijiuliza je! Mmoja alitenda kwa mfano wa nani, Daudi au Yeroboamu? Kumbuka siku zote, lengo ni kumfuata Kristo, ila wapo walio hirimu zetu, watu walitutangulia katika imani, nao wamewekwa kwetu kama mifano ili tujue itupasavyo kumfuata BWANA.
 
Nakupa mfano wa Uzia mwana wa Amazia, mfalme wa Israel, yeye alitenda mema, ILA sio kama Daudi. Ni kweli alimfuata BWANA lakini bado kulikuwa na ibada za sanamu katikati ya Israel. Angalia hapa “….Ila mahali pa juu hapakuondolewa, nao watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Hata leo, je! Hatumtumikii BWANA? Je! Hatusemi kwamba sisi ni wa Kristo? Umewahi kujiuliza kwa habari ya “matendo mafu/ibada ya sanamu” katikati yako?  Kweli umemfuata BWANA ila kuna “MAHALI  PA JUU” hapajaondolewa, bado unatoa sadaka huko! Kwani hujui mwili wako ni sadaka takatifu? Angalia mahali unapopeleka viungo vya mwili wako kisha ujue kama uko katika fungu la Daudi mwana wa Yese au Yeroboamu mwana wa Nebati. Angalia, haikumsaidia Uzia kuwa katikati (nusu mfano wa Daudi na nusu mfano wa Yeroboamu), yeye alifanya mema (kama Daudi), ila kulikuwa na ibada za samu pia (kama Yerobuamu), hatua zake zikawa nzuri ILA sio kama za Daudi mwana wa Yese, akapigwa ukoma hata kufa kwake.
 
Angalia hatua zako vyema, laiti ungefanya mambo si kwa sababu ya kuogopa ukoma, ila kwa kumpenda BWANA. Laiti ungelisimama katika saa ya kujaribiwa kwako, na kujua jinsi ya kusimama, kwa maana wengi wamebaki na visingizio na sababu za kuabudu sanamu katikati ya BWANA, huku wakitaja majina ya watu vinywani mwao, je! Watakuwa salama kwa sababu hiyo? Eti, “kama isingekuwa fulani, nisingekuwa kama nilivyo”! Kama haikumsaidai Uzia, jua haitakusaidia wewe pia. Ayubu alijua imempasa kusimama peke yake, hata kama mkewe yuko kiyume naye. Je! Yusufu alipoteswa alimwacha BWANA kwa sababu ya mateso? Kwani Danieli hakusubiri tu hadi alipotupwa kwenye tundu la simba? Je! Yuko mtu wa kusingizia, kwamba kama sio yeye usingemtenda Mungu dhambi? Je! Si kiburi na tamaa zako vimekuponza tu? Kwani hukujau kwamba imekupasa kumtwika BWANA fadhaha zako? Bwana anajua ulimwenguni tunayo dhiki nyingi, ila ametuachia Jina ili tulindwe na hilo, na akiisha kututia moyo akaenda kutuandalia makao, je! Akirudi ataikuta imani duniani?
 
Frank Philip.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: